Kamati ya Bunge yaridhishwa na utoaji wa mikopo asilimia 10 kutoka halmashauri

*Ni baada ya kutembelea miradi ya vikundi vinavyonufaika jijini Mbeya

NA ANGELA MSIMBIRA, OR-TAMISEMI

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa imetembelea miradi ya vikundi vinavyonufaika na mikopo ya asilimia 10 katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya na kuridhishwa na utoaji wa mikopo kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Hayo yalisemwa Machi 14, 2022 na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Abdallah Chaurembo wakati wa ziara ya kamati hiyo katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuangalia miradi inayotekelezwa na Serikali hasa katika suala zima la utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kutoka katika halmashauri ya jiji hilo.
"Kamati imeridhishwa na utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, mikopo ambayo ina tija na kusaidia vikundi hivyo kujikwamua kiuchumi,"amesema Mhe. Chaurembo.

Mhe. Chaurembo ameipongeza Serikali kwa kuhakikisha wanatoa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambayo imesaidia katika kuongeza pato la mtu binafsi na taifa kwa ujumla.

Mhe. Chaurembo amezitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatoa mikopo yenye tija kwa vikundi hivyo ili viweze kujikwamua kiuchumi.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amesema Serikali inayoongozea na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuhakikisha fedha zinatengwa kwa ajili ya kuleta chachu ya uzalishaji na shughuli za maendeleo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu nchini.

Aidha, Waziri Bashungwa amewagiza maafisa maendeleo ya jamii katika jalmashauri zote kuhakikisha wanatoa elimu ya usimamizi wa fedha kwa vikundi vyote vilivyonufaika na vinavyoendelea kunufaika na mikopo ya aslimia 10.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera amesema katika kipindi cha 2018/19 hadi Februari 2022 Halmashauri za Mkoa wa Mbeya zimeweza kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 7.7 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wwnye ulemavu 950 ambapo wanawake ni 583,vijana 329 na watu wenye ulemavu 38

Aidha. Kamati ya ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa inaendelea na ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Mkoa wa Mbeya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news