Karatu, DC apongezwa kwa usimamizi mzuri wa miradi

NA SOPHIA FUNDI

KAMATI ya Siasa Mkoa wa Arusha imepongeza Halmashauri Wilaya ya Karatu pamoja na mkuu wa wilaya kwa kusimamia vizuri miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.
Kamati hiyo ambayo inaongozwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC) wa Mkoa wa Arusha, Daniel Palangyo imetoa kauli hiyo walipotembelea baadhi ya miradi yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja.

Palangyo amesema kuwa, Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo na hiyo ni baadhi tu ya miradi iliyotolewa fedha na serikali, hivyo ni jukumu la viongozi kuwaeleza wananchi serikali imefanya nini na wapi na kwa fedha kiasi gani ili wananchi wajue serikali yao inafanya nini.

"Rais wetu mama Samia Suluhu ametoa fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo kwa wilaya ya Karatu,lakini wananchi bado wengine hawajui hilo, hivyo naomba viongozi tokeni maofisini nendeni kwa wananchi wajue serikali yao inafanya nini,"alisema Palangyo.

Kamati hiyo ilimpongeza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo pamoja na madiwani kwa kusimamia bajeti ya halmashauri ya asilimia 40 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya maendeleo ambapo katika ziara hiyo walitembelea mradi wa Kituo cha Afya Buger iliyotengewa kiasi cha sh.milioni 400 kutoka mapato ya ndani.

Akizungumza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri, Karia Magaro alisema kuwa mafanikio ya utekelezaji wa miradi hiyo ni ushirikiano wa uongozi mzima wa wilaya wakiwemo mkuu we wilaya,madiwani pamoja na wataalam.

Magaro aliahidi kutekeleza ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyojikita kuwaletea wananchi maendeleo.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Karatu, Dadi Kolimba alishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutoa fedha nyingi katika wilaya hiyo kwa ajili ya maendeleo ambapo amewahakikishia kamati kuwa serikali ya wilaya itahakikisha miradi yote inatekelezwa kwa weledi na kwa usimamizi mkubwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news