Yusuph Kileo:Dunia inapaswa kuwekeza zaidi kwenye maarifa ya usalama mtandaoni

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

IKIWA ni Karne ya 21, hapa duniani kampuni na taasisi binafsi na Serikali zimewekeza zaidi katika uchumi wa teknolojia ili kuendana na kasi ya maendeleo kwa ajili ya kukuza uchumi shindani.

Hata hivyo, katika utumiaji wa teknolojia kupitia mfumo wa intaneti au Data kumekuwa na mashambulizi mbalimbali ya kimtandao yanayoleta athari za moja kwa moja.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha Mawasiliano cha AfICTA (Africa Information and Communication Technologies Alliance-AfICTA) imeonesha namna shambulio la kimtandao lilivyoathiri utendaji wa kampuni kubwa ya usafirishaji ya Kimataifa hivi karibuni.

Kampuni ya Expediors, Februari 20, mwaka huu seva yake ilishambuliwa na kusababisha kusitisha shughuli za usafirishaji na utendaji wake katika maeneo mengi.

Aidha, wataalamu wamerejesha mifumo ya taasisi hiyo binafsi kurejea katika utendaji baada ya shambulio ila bado hawajajua ni lini itarejea kwenye kasi kama ilivyokuwa awali.
Mshauri na Mtaalamu wa Masuala ya Usalama Mtandaoni barani Afrika, Mtanzania Bw.Yusuph Kileo ameieleza DIRAMAKINI BLOG kuwa,kuna haja ya kupata funzo kubwa kutokana na shambulio hilo lililotokea mapema mwaka huu.

"Kwa kuwa wavamizi na wezi wa mtandao wamekuwa wakiiba fedha kutoka kwenye taasisi,wanaiba taarifa binafsi na wakati mwingine wanazuia taarifa ili kupata kikombozi (katika uhalifu mtandao aina ya Ransomware). Kuna haja ya kuwekeza zaidi kwenye maarifa ya usalama mtandaoni ili kuepuka madhara ya namna hiyo,"amesema Bw. Kileo.

Kileo ambaye ni Mtanzania aliyebobea katika masuala ya usalama mtandao na uchunguzi wa makosa ya kidigitali ameongeza kuwa, kwa sasa hali inazidi kuwa mbaya zaidi, kwani wavamizi wa mtandao, wameanza kushambulia hadi mifumo ya ziada ya chelezo data na hii ni hatari zaidi.

"Mfano wa hivi karibuni ni shambulio la mfumo wa Bomba la mafuta la Marekani maarufu kwa jina la Clonial Pipeline ambapo likikumbwa na shambulizi mtandao mwaka jana. Shambulio hilo lilisababisha kampuni hiyo kubwa ya nchini Marekani kushindwa kufanya kazi na wahalifu mtandao walidai kikombozi ili kuirudishia uwezo wa kufanya kazi kampuni hiyo,"amesema Bw.Kileo.

Aidha, anasema ingawa kampuni hiyo ilikua na chelezo Data mpya na ya kisasa bado haikua msaada kwa kampuni hiyo.

Kutokana na hali hiyo, mtaalamu huyo wa masuala ya mtandao anaona kwa sasa taasisi zinaweza kuwa na mfumo mbadala wa chelezo data ili kuziba athari za shambulio.

Bw.Kileo amesema wamekuwa akitoa elimu ya kuongeza uwezo wa taasisi kujilinda zaidi na uhalifu mtandao.

Ameshauri kampuni na taasisi mbalimbali kuandaa mpango kazi wa namna ya kukabiliana na hatari ya kushambuliwa.

Pia Kileo anazishauri taasisi hizo ambazo zimewekeza zaidi kwenye teknolojia basi ni lazima ziwekeze zaidi kwenye mpango mkakati wa kukabiliana na mashambulizi ya kimtandao. "Yaani taasisi zinapaswa kulinda watu wake, shughuli za kiuendeshaji na teknolojia kwa pamoja,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news