Maagizo ya Waziri Dkt.Mabula kwa Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi nchini

>Asema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuboresha mazingira ya utendaji kazi,mabadiliko ya sheria

NA MUNIR SHEMWETA-WANNM

SERIKALI imewataka Wenyeviti wa Mbaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kujiepusha na tabia ya uwekaji mazuio yasiyo na tija dhidi ya uuzaji wa nyumba za wadaiwa wa benki.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akitoa maelekezo katika chumba cha Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza mara baada ya kulizindua rasmi.

Akizungumza wakati wa kuzindua Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya ya Sengerema tarehe 21 Machi 2022 jijini Mwanza, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula amesema, baadhi ya mazuio huwekwa na kisha shauri hupangiwa tarehe ya mbali bila sababu ya msingi.

“Jambo hili halikubaliki hata kidogo kwani linarudisha nyuma shughuli za kimaendeleo na kukuza uchumi wan chi yetu” amesema Dkt. Mabula.

Amesema, Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kutoa kipaumbele katika kuyawezesha Mabaraza ya Ardhi kufanya kazi vizuri na tayari imeanza kufanya maboresho ya muundo wa wizara utakaowezesha kila mkoa kuwa na Msajjili Msaidizi wa Mabaraza kwa ajili ya usimamizi wa karibu wa utendaji kazi wa Mabaraza.

Vile vile, kwa mujibu wa Dkt. Mabula Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ambapo katika kuboresha mazingira ya utendaji kazi imefanya mabadiliko ya sheria ili kuwawezesha Wenyeviti wa Mabaraza kuwa na ajira za kudumu.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wananchi ambao wameshika Muongozo wa Mabaraza ya Ardhi wakati wa uzinduzi wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza mara baada ya kuzindua rasmi.

Amewakumbusha watumishi wote wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya nchini kutimiza majukumu yao kwa weledi na kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozi iliyopo na ile itakayokuwa ikitolewa ili kuboresha utoaji huduma ya utatuzi wa migogoro itokanayo na matumizi ya ardhi.

Pia Waziri wa Ardhi, Dkt. Mabula aliwataka Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi kuwafuata wananchi kwa kutembelea mabaraza mapya ili kusikiliza mashauri kwenye wilaya husika wakati Wizara ikiendelea kukamilisha taratibu za ajira za wenyeviti wa mabaraza hayo.

Kwa upande wake Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya Stella Tullo alisema, ofisi yake imejipanga na kuhakikisha migogoro ya ardhi inapofika kwenye Mabaraza inasikilizwa kwa haki na kwa haraka na kusisitiza kuwa, hawatopenda kuchelewesha mashauri bila sababu za msingi.

“Sisi tunataka shauri linapofika kwenye Baraza liweze kuanza kusikilizwa mapema baada ya taratibu za awali za kisheria kukamilika ili tuweze kukamilisha kwa wakati,’’amesema Stella. Uzinduzi wa Baraza la Ardhi la Wilaya ya Sengerema uliwakilisha pia uzinduzi wa mabaraza mengine mapya katika wilaya za Nachingwea, Ruangwa, Liwale, Kilwa, Serengeti, Kongwa, Kishapu na Mlele.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news