Mheshimiwa Kinyaiya:Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ni kimbilio la wengi nchini

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

KATIBU Tawala wa Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Mhe. Arnold Kinyaiya amesema, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ni kimbilio la wengi nchini katika suala zima la kujiendeleza kielimu.
Mhe. Kinyaiya ameyasema hayo Machi 18, 2022 wakati akifungua mkutano wa Bazara la Nane la Wafanyakazi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania jijini Dar Es Salaam akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Godwin Gondwe.

“Kutualika kuhudhuria mikutano kama hii ni fursa kwa Serikali kukifahamu vyema chuo hiki, natambua fika mchango wa chuo hiki hasa katika kuwaendeleza wafanyakazi waliopo makazini, wasio na uwezo wa kujiunga vyuo vya bweni,”amesema.
Akizungumzia baraza hilo,Mhe. Kinyaiya amesema baraza alilolizindua ndiyo sehemu pekee ya kujadiliana na kuridhiana kuweka mambo sawa, kwani hata kukiwa na sera, sheria na kanuni nzuri mahali pa kazi, lakini kama hakuna ushirikiano baina ya Menejimenti na Watumishi itakuwa vigumu kwa taasisi kutimiza malengo yake.

Akizungumza katika Baraza hilo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu huria cha Tanzania, Prof.Elifas Bisanda alitaka jamii kutambua mchango wa chuo hicho katika kutoa elimu ya teknolojia kwa watu wenye uhitaji maalum hasa kuzungumza, kusikia na kuona.
Alisema kuwa, chuo hicho kimekuwa kikitoa mafunzo kwa kundi hilo la watu, lakini jamii bado haifahamu na kwa wale wachache waliopitia chuo hicho wamekuwa na manufaa kwa jamii zinazowazunguka kwa kutumia ipasavyo vifaa vya rununu.

“Chuo hiki kina mambo mengi ya kijamii inayoyafanya na tusipoyasema, hakuna atakayejua, mambo mengine tunaona kama ni madogo lakini yana faida kubwa kwenye jamii zetu,”amesema.
Prof. Bisanda, aliongeza kuwa baraza hilo linalobeba wajumbe kutoka pande zote za nchi lina wajibu wa kutathmini changamoto zinazokabili chuo na kupendekeza majibu ya changamoto hizo lakini pia baraza lina wajibu wa kujadili mpango mkakati na kupata taarifa ya utekelezaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news