Rais Dkt.Mwinyi ataja faida za ujio wa Rais wa Shirikisho la Mchezo wa Kuogelea Duniani (FINA) Zanzibar

*FINA yaahidi mambo mazuri kupitia mchezo huo 

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa ujio wa Rais wa Shirikisho la Mchezo wa Kuogelea Duniani (FINA) hapa Zanzibar utasaidia kwa kiasi kikubwa kuitangaza Zanzibar kiutalii hasa katika utalii wa michezo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa zawadi maalum ya Jahazi na mgeni wake Rais wa Shirikisho la Mchezo wa Kuogolea Duniani (FINA), Bw.Husain Al Musallam, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo Machi 15,2022.(Picha na Ikulu).

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo alipokutana na Rais wa Shirikisho la Mchezo wa Kuogelea Duniani (FINA), Hussain Al Musallam akiwa na ujumbe wake wa viongozi mbalimbali wa shirikisho hilo kutoka ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiwemo waliotoka makao makuu ya FINA nchini Switzerland.

Katika mazungumzo hayo Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa mchezo huo ni maarufu duniani na ujio wa kiongozi huyo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Zanzibar na shirikisho hilo la mchezo wa kuogelea duniani.

Ameongeza kuwa, hatua hiyo itaisaidia sana Zanzibar ambayo imezungukwa na bahari, na kwa vile ipo katika mikakati ya kuimarisha Sera ya Uchumi wa Buluu ambapo miongoni mwa malengo iliyojiwekea ni kuimarisha sekta ya utalii kwa kupitia utalii wa michezo.

"Tumefurahishwa kwa kiasi kikubwa na ujio wa Rais wa Shirikisho la Mchezo wa Kuogelea Duniani (FINA), Hussain Al Musallam ambapo kuja kwake hapa Zanzibar kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha ushirikiano katika sekta ya michezo nchini,"amesema Dkt.Mwinyi.

Aidha, amesema kuwa ujio wa kiongozi huyo ni mwanzo mzuri wa ushirikiano katika kukuza sekta ya michezo ikiwemo utalii wa michezo ambao kutokana na mazingira ya Zanzibar mafanikio makubwa yanaweza kupatikana.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na mgeni wake Rais wa Shirikisho la Mchezo wa Kuogolea Duniani (FINA), Bw.Husain Al Musallam (kulia kwa Rais) alipofika Ikulu jijini Zanzibar na ujumbe wake kwa mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo. (Picha na Ikulu).

Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa, ziara ya kiongozi huyo ni nafasi nzuri kwa Zanzibar kwani itasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha sekta ya michezo ambayo hivi sasa imewekewa mikakati maalum.

Ameeleza haja kwa Zanzibar kuwa mwanachama wa Shirikisho hilo la Mchezo wa Kuogelea Duniani (FINA), hatua ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kujifunza mambo kadhaa kutoka shirikisho hilo ambalo limepata mafanikio makubwa.

Sambama na hayo, Rais Dkt. Mwinyi ametumia fursa hiyo kumkaribisha Zanzibar Rais wa Shirikisho la Mchezo wa Kuogelea Duniani (FINA) Hussain Al Musallam na kumueleza mikakati na malengo yaliyowekwa na Serikali anayiongoza katika kuimarisha sekta ya michezo hapa nchini ukiwemo utalii wa michezo.

Naye Rais wa Shirikisho la Mchezo wa Kuogelea Duniani (FINA), Hussain Al Musallam amemueleza Rais Dkt. Mwinyi kwamba kuogelea si mchezo tu bali ni sehemu ya maisha ambapo vijana walio wengi wamekuwa wakiufuatilia.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Rais wa Shirikisho la Mchezo wa Kuogolea Duniani (FINA), Bw.Husain Al Musallam (kulia kwa Rais) alipofika Ikulu jijini Zanzibar na Ujumbe wake kwa mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo, na kushoto kwa Rais ni Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mhe. Simai Mohammed Said na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali.(Picha na Ikulu).

Amesema kuwa, miongoni mwa sababu kubwa ya ziara yake ya kuja Zanzibar ni pamoja na kuja kumuunga mkono Rais Dkt. Mwinyi katika mikakati yake ya kuimarisha uchumi kupitia Sera ya Uchumi wa Buluu ambao sekta ya utalii wa michezo imejikita ndani yake.

Kiongozi huyo wa Shirikisho la Mchezo wa Kuogelea Duniani (FINA), alimueleza Rais Dkt. Mwinyi hatua mbalimbali zilizowekwa na shirikisho hilo katika kuhakikisha inaweka programu mbalimbali za mafunzo ya kuogelea kwa ajili ya vijana ambapo na vijana wa Zanzibar nao watafaidika.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi zawadi maalum ya Mlango wa Zanzibar mgeni wake Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Kuogolea (FINA), Bw.Husain Al Musallam, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar leo.(Picha na Ikulu).

Pamoja na hayo, Rais wa Shirikisho la Mchezo wa Kuogelea Duniani (FINA), Hussain Al Musallam alieleza azma ya Shirikisho hilo ya kusaidia kuimarisha sekta ya utalii hapa Zanzibar hatua ambayo itaweza kuitangaza Zanzibar kimichezo Kimataifa.

Nao viongozi katika ujumbe huo walieleza kuvutiwa na mazingira ya Zanzibar ambayo yanauwezo wa kutoa vipaji kadhaa vya mchezo wa kuogelea sanjari na kuitangaza Zanzibar kiutalii kwani mchezo huo ni maarufu duniani na hapa Zanzibar umekuwa ukipendwa na vijana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news