Rais Samia arejesha tozo ya 100/- kwenye mafuta, CAG awasilisha ripoti

*Taasisi zilizopata hati zenye mashaka ni Dar es Salaam, halmashauri za Wilaya ya Kisarawe, Longido, Mlele, Musoma, Sengerema na Bunda

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amerudisha tozo ya shilingi 100 iliyokuwa ikitozwa katika mafuta ya petroli, dizeli nchini kutokana na kuendelea kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la Dunia kunakosababishwa na vita kati ya Urusi na Ukraine.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea Taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2020/2021 kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, CAG Charles Kichere katika hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Jijini Dodoma leo Machi 30, 2022.

Ametoa agizo hilo leo Machi 30,2022 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma wakati wa hafla ya kupokea taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2020/2021 pamoja na ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Februari 28, 2022 Waziri wa Nishati, Mheshimiwa January Makamba alitangaza uamuzi wa kuondoa tozo hiyo ili kuwapa unafuu wananchi na kubaki senti 56.

Mheshimiwa Rais Samia amesema, suala la upandaji wa bei za mafuta yamekuwa yakipanda tangu katikati ya mwaka jana na kwamba walichukua hatua ya kupunguza tozo kwa mara ya kwanza ili kushusha bei ya mafuta kwa wananchi.

“Lakini (Waziri) hakuangalia kwa upana zaidi. Kwamba hiyo ilikuwa tayari katika bajeti iliyopitishwa na Bunge kulikuwa na utata kidogo. Kwa hiyo tumekaa kama Serikali tumerekebisha kwa hiyo ile shilingi (100) nimeagiza irudishwe,”ameagiza Mheshimiwa Rais Samia.

Amesema, tathimini waliyoifanya imeonyesha hata kama shilingi 100 wangeiondoa kwa mwenendo wa upandaji wa mafuta bado isingekuwa na athari ila wangejikosesha kile ambacho wanakusanya.

Pia Mheshimiwa Rais Samia amewataka wabunge, mawaziri wanaosimamia sekta hiyo kuwaambia ukweli wananchi kuwa vita ya Urusi na Ukraine imepandisha bei ya mafuta.

Amesema, mafuta yanapopanda ndio kila kitu kinapanda ikiwemo nauli, usafirishaji wa bidhaa pia utapanda.

"Sasa hivi kutoa kontena la bidhaa kutoka China kuleta Tanzania, kwa kontena nadhani la futi 40 lilokuwa dola (Kimarekani) 1500 sasa hivi ni dola (Kimarekani) 8,000 hadi 9,000,”amesema Mheshimiwa Rais Samia.

Amesema na hilo linaenda kuathiri bei za bidhaa na kuwataka viongozi kuwaeleza sababu za kupanda kwa bei ya bidhaa nchini.

Mheshimiwa Rais Samia amewataka wawaambie wananchi ukweli ili wasikae kusema kuwa Serikali inakaa kimya na haichukui hatua.

Wakati huo huo, kuhusu mafuta ya kula, Mheshimiwa Rais amemuagiza Waziri wa Fedha na Mipango,Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Nchemba kuangalia upya uamuzi waliouweka kwa ajili ya kulinda viwanda vya ndani nchini.

Amesema, uamuzi huo ulilenga kulinda viwanda vya nchini, lakini imeonekana badala ya kulinda, baadhi ya viwanda vimekufa na hivyo kusababisha bei ya mafuta ya kula kuwa juu.

“Sasa mmezuia mafuta ya nje hayaingii, viwanda vya ndani havizalishi. Bila shaka wananchi watapiga kelele kwa sababu bei itakuwa kubwa,”amesema Rais Samia.

MSD

Katika hatua nyingine Rais Samia ametoa agizo la kufanywa mabadiliko katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kwenye ngazi zote za utendaji kazi.

Mheshimiwa Rais Samia amesema, mabadiliko hayo ni kutokana na bohari hiyo kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo katika kuhudumia soko la nchi za Jumuiya ya Maendeleo za Kusini mwa Afrika (SADC).

Pia ameagiza kufanyike ukaguzi na tathimini ya mashirika ya umma na kuyafuta ambayo hayana tija kwa Taifa, kwani mpaka sasa mashirika 38 yanaendeshwa bila Bodi ya Wakurugenzi.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Samia ameitaka Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) kuzisimamia halmashauri ipasavyo na kuwachukulia hatua watumishi wenye matumizi mabaya ya fedha za Serikali.

Kwa upande mwingine, Rais Samia ameipongeza TAKUKURU kwa kuweza kudhibiti matumizi mabata ya fedha na kuitaka taasisi hiyo kujielekeza zaidi katika kuzuia kuliko kupambana na rushwa.

Aidha, amempongeza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa kuweza kupunguza kiwango cha hati chafu na kuweza kudhibiti usimamizi wa rasilimali za umma.

CAG

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG),Charles Kichere katika hafla hiyo amesema kuwa, taasisi 19 za umma kati ya taasisi 999 katika mwaka mwaka wa fedha 2020/2021 zimepata hati zenye mashaka.

CAG Kichere amesema, katika mwaka 2020/21 amefanya kaguzi maalumu 56, kaguzi 37 zikiwa za mamlaka za Serikali za Mitaa, 12 Serikali Kuu na sita mashirika ya umma na moja ya mifumo ya TEHAMA.

“Katika mwaka 2020/21 nimetoa jumla ya hati 999 za ukaguzi, kati ya hizo, hati 185 za mamlaka za Serikali za Mitaa, 195 mashirika ya umma, hati 308 serikali kuu, hati 19 vyama vya siasa, hati 292 miradi ya maendeleo,”amesema CAG.

Amesema, kati ya hati 999 nilizotoa, hati zinazoridhisha ni 970, sawa na asilimia 97.1, hati zenye mashaka ni 19, sawa na asilimia 1.9, hati mbaya ni sita na nilitoa hati 4 za kushindwa kutoa maoni. Amesema hati mbaya na mashaka zimepungua katika ukaguzi huo ikilinganishwa na mwaka jana.

CAG Kichere amesema, kuna ongezeko la hati safi kutoka asilimia 89 kwa mwaka jana hadi asilimia 98.01 mwaka 2020/2021.

Amezitaja taasisi zilizopata hati zenye mashaka kuwa ni Jiji la zamani la Dar es Salaam, Halmashauri za Wilaya ya Kisarawe (Pwani), Longido (Arusha), Mlele (Rukwa), Musoma (Mara), Sengerema (Mwanza) na Bunda (Mara).

Kichere amesema, kwa upande wa mashirika ya umma, taasisi zilizopata hati yenye mashaka ni Mamlaka ya Maji na Ustawi wa Mazingira Geita, Muleba, Ngara (Kagera), Tabora, Taasisi ya Mifupa Muhimbili na Mamlaka ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).

Nyingine ni Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) huku Shirika la Masoko Kariakoo na Shirika la Reli Tanzania akisema walishindwa kutoa maoni katika ukaguzi huo.

Wakati huo huo, CAG Kichere amesema vyama vinne vimepata hati mbaya, vitatu hati yenye mashaka na viwili walishindwa kutoa maoni.

Amevitaja vyama hivyo vilivyopata hati mbaya katika ukaguzi huo ni ADC, Chaumma, UMD na TLP huku vyama vya CUF, UDP, SAU vikipata hati zenye mashaka.

CAG Kichere amesema chama cha Demokrasia Makini na AFP walishindwa kutoa maoni katika ukaguzi huo.

Katika hatua nyingine,CAG Charles Kichere amebaini kwa miaka mitatu mfululizo, mafao ya pensheni ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Sekta ya Umma yalizidi mapato yanayotokana na michango kwa mwaka husika.

CAG amesema mifuko hiyo ina changamoto na kwamba pamoja na Serikali kuongeza uwezo wa mfuko wa PSSSF hadi kufikia asilimia 30, bado kiwango hicho kiko chini ya asilimia 40 inayopendekezwa

“Mifuko ya hifadhi ya jamii ina changamoto mbalimbali kwa miaka mitatu mfululizo, mafao ya pensheni ya mfuko wa hifadhi ya jamii kwa sekta ya umma yalizidi mapato yanayotokana na michango kwa mwaka husika,”amesema CAG Kichere.

Pia amesema, mwaka wa fedha 2020/21 mafao yalizidi kwa shilingi bilioni 767, mwaka 2019/2020 yalizidi kwa shilingi bilioni 232 na 2018/19 yalizidi kwa shilingi bilioni 307.

CAG Kichere amesema kuwa,hadi kufikia Juni 30, 2021 mfuko huo ulikuwa na madeni ya shilingi bilioni 323.98 kutoka kwa taasisi za Serikali na mashirika mengine.

Aidha, Kichere amesema Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii wa Sekta binafsi (NSSF) ulitoa mikopo ya shilingi trilioni 1.17 kwa taasisi 10 za Serikali ambayo haijalipwa tangu mwaka 2007.

Mbali na hayo, CAG Kichere amesema, deni la Serikali limeongezeka kutoka shilingi trilioni 56.76 mwaka uliopita hadi kufikia shilingi trilioni 64.52 kufikia Juni 30, 2021.

CAG Kichere amesema, kuna ongezeko la shilingi trilioni 7.76 sawa na asilimia 13.7 ambapo kwa mujibu wa kipimo cha deni la Serikali kinachotumia pato la Taifa, kinaonesha deni hili bado ni himilivu.

Amesema, miradi ya kujenga na kuboresha viwanja vya ndege 12 yenye thamani ya shilingi trilioni 1.02 iliyotekelezwa katika kipindi cha kati ya mwaka 2016/17 hadi 2020 2021 ilikaguliwa.

CAG Kichere amesema,ukaguzi ulibaini kuwa kuna mwingiliano wa mamlaka na majukumu ya uendelezaji wa viwanja vya ndege mwingiliano kati ya Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) unaosababisha mapungufu na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi hiyo nchini.

Vilevile amesema, wamebaini kuna ongezeko la gharama ya shilingi bilioni 22.35 kutokana na kutolipa fidia kaya 1,125 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa zaidi ya miaka 23.

Amesema, kuna watu wanatakiwa kulipwa fidia lakini kuna taratibu hazijakamilika kwa hiyo tangu mwaka 1997 na kwamba tathmini inaonyesha deni linaongezeka kutoka shilingi bilioni 7 hadi shilingi bilioni 29.

TAKUKURU

Wakati huo huo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) imefuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo 1,188 katika sekta za ujenzi, maji, afya, elimu, fedha na kilimo yenye thamani ya shilingi bilioni 714.17. Thamani hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa mikataba ya kazi husika.

Hayo yamesemwa leo Machi 30,2022 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, CP Salum Rashid Hamduni wakati akikabidhi taarifa ya utendaji kazi ya mwaka 2020/2021 kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

CP Hamduni amesema, TAKUKURU katika kipindi cha mwaka 2020/21 ilitekeleza majukumu yake ya msingi ya kuzuia na kupambana na rushwa kama yalivyoaiishwa katika Mpango Mkakati wake wa miaka mitano kuanzia mwaka 2017/2018 hadi 2021/2022.

"Miradi 966 yenye thamani ya shilingi bilioni 635.09 ilibainika kuwa na mapungufu madogo madogo hivyo, watekelezaji wake walishauriwa namna bora ya kuboresha utekelezaji wa miradi hiyo kupitia vikao kazi. Miradi 222 yenye thamani ya shilingi bilioni 79.14 iliyoonekana kuwa na viashiria vya ufujaji na ubadhirifu wa fedha, uchunguzi umeanzishwa na unaendelea,"amefafanua CP Hamduni.

Kwa upande wa uchambuzi wa mifumo, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU ameema kuwa, jumla ya kazi za uchambuzi 683 zilifanyika kwa lengo la kubaini mianya ya rushwa na kushauri namna bora ya kuiziba mianya ya rushwa iliyobainika.

Amesema, kazi hizo zilihusu mfumo wa ukusanyaji wa ushuru wa huduma (service levy) katika halmashauri 141 nchini,mfumo wa utoaji na urejeshaji wa mikopo inayotolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu,mfumo wa utoaji wa vibali vya ujenzi katika halmashauri 102 nchini.

Pia kuna mfumo wa utoaji huduma ya mikopo inayotolewa na makampuni binafsi kwa wananchi na Mfumo wa malipo wa EPICOR katika halmashauri mbili.

"Matokeo ya chambuzi za mifumo yaliainishwa na kuwasilishwa kwenye warsha na vikao vya wadau 437, ambapo mikakati ya kuiziba mianya iliyobainishwa iliwekwa na wahusika kutakiwa kuiziba mianya hiyo.

"Mheshimiwa Rais,kutokana na kazi za uzuiaji rushwa zilizofanyika, vitendo vya rushwa ambavyo vingeweza kutokea na kusababisha ubadhirifu na ufujaji wa rasilimali za umma vilidhibitiwa, miradi ya maendeleo iliyofuatiliwa iliweza kutekelezwa kwa ubora uliokusudiwa na wananchi kuweza kupata huduma stahiki kwa wakati,"amesema CP Hamduni.Soma kwa kina hapa>>>

Post a Comment

0 Comments