Rais Samia aridhia nyumba za Magomeni Kota kuuzwa kwa wapangaji

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameridhia ombi la wakazi wa Magomeni Kota kuuziwa nyumba kwa utaratibu wa mpangaji mnunuzi huku akiwataka waliokuwa tayari kuanza kulipia mara moja.
Mheshimiwa Rais Samia ameridhia hayo Machi 23, 2022 wakati akizindua nyumba 644 za waliokuwa wakazi wa Magomeni Kota katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Rais Samia amefafanua kuwa, wakazi hao watatakiwa kurejesha gharama za ujenzi pekee na hawatatozwa gharama ya ardhi ili wapate nafuu za kuzinunua.

“Nimeridhia wananchi hawa kuuziwa nyumba kwa utaratibu wa mpangaji mnunuzi na kurejesha gharama za ujenzi pekee, hatutawatoza gharama za ardhi kwa sababu tukifanya hivyo mtashindwa.

"Kwa wale wanaotaka kulipa polepole, wanaweza wakaanza sasa mchakato huo ili ikifika miaka mitano, kama umemaliza au unaendelea kulipa na kubaki katika nyumba. Mnaweza kuanza kulipa sasa na mkianza wote kwa pamoja itakuwa vizuri zaidi, niwaombe muanze kulipa sasa,”amesema Rais Samia.

Pia amewaasa wananchi hao kuanza kulipa fedha polepole ili Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wapate fedha za kumalizia palipo bakia.

“Mnaweza kuanza kulipa sasa na mkianza wote kulipa sasa itakuwa vizuri zaidi kwa sababu mtawasaidia TBA wakusanye fedha ya kumalizia eneo lililobakia, kwa hiyo niwaombe sana muanze kulipa sasa,”amesisitiza Rais Samia.

Mwakilishi wa wakazi 644 wa Magomeni Kota, George Abel amedai kuwa asilimia 80 ya wakazi wa nyumba hizo ni wazee, wajane na kipato chao ni cha chini.

“Mama ameagiza katika zile huduma muhimu hatutalipia ndani ya miezi mitatu. Pia tutakaa miaka mitano bure. Leo umetufuta machozi, hayawi hayawi sasa yamekuwa,”amesema Abel.

Mradi wa Magomeni Kota ulianza mwaka 2016 katika Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 52 ambapo kila jengo linabeba kaya 128 ambapo zimejengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news