RAIS SAMIA KUZINDUA MRADI WA MAJI WA MLANDIZI-CHALINZE - MBOGA ULIOGHARIMU BILIONI 18/- RC KUNENGE ASEMA JITAHADA ZA RAIS ZINAPASWA KUUNGWA MKONO NA WANANCHI

*Amshukuru Rais kwa kutoa fedha nyingi kufanikisha miradi ya maendeleo

NA ROTARY HAULE

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara Machi 22,2022  mkoani Pwani kwa ajili ya kuzindua mradi mkubwa wa maji wa Mlandizi-Chalinze-Mboga uliogharimu kiasi cha sh.Bilioni 18.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge ametoa taarifa hiyo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali katika ofisi zake zilizopo Mjini Kibaha ambapo amesema Rais atafanya ziara hiyo Machi 22,2022 ambayo ni Siku ya Jumanne.
Kunenge amesema kuwa, Rais Samia anazindua mradi huo ikiwa ni muendelezo wa jitihada zake za kuboresha huduma ya maji katika maeneo mbalimbali yenye changamoto ya upatikanaji wa maji.

Amesema,mradi huo wa bomba kuu unatarajiwa kusafirisha kiasi cha lita za ujazo milioni tisa na laki tatu( 9,300,000) kwa siku na zitawezesha kuwahudumia wakazi wapatao 120,912.

Amesema, ujenzi wa mradi huo utakuwa na vituo viwili vya kusukuma maji (Boosting Stations) vilivyojengwa katika Kijiji cha Chamakweza na Msoga ambapo pampu sita ikiwa pampu tatu kwa kila kituo za kusukuma maji zimefungwa.
"Mheshimiwa Rais ametupa heshima kubwa ya kuja kuzindua mradi wetu mkubwa wa maji unaogharimu fedha nyingi kiasi cha shilingi bilioni 18 hii inaonyesha jinsi gani anavyowapambania wananchi wa Pwani kwahiyo lazima tumpongeze na kumshukuru kwa jitihada hizi kubwa anazofanya," amesema Kunenge.

Amesema kuwa, Rais Samia anazindua mradi huo ikiwa ni sehemu ya kilele cha wiki ya maji yanayofanyika Machi 22 Siku ya Jumanne huku akisema kazi anayofanya Rais ni kubwa na anapaswa kuungwa mkono.

"Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya Kujenga mradi huu mkubwa wa maji ambao utasaidia kumaliza changamoto ya maji kwa wananchi wa Mlandizi-Mboga na Chamakweza,"amesema Kunenge.
Kunenge amesema kuwa Rais atazindua mradi huo katika eneo la Msoga na baadae kuzungumza na wananchi katika viwanja vya Polisi vilivyopo Chalinze ambapo amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kumlaki Rais.

"Baada ya Rais kuzindua mradi huo katika eneo la Msoga ataelekea  katika eneo la viwanja vya Polisi Chalinze kwa ajili ya kuzungumza na wananchi kwahiyo nawaomba wananchi wa Mkoa wa Pwani wajitokeze kwa wingi katika mkutano huo," amesema Kunenge.

Hata hivyo, Kunenge amewaomba wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuja kwa wingi katika kumlaki Rais kwakuwa mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya chama.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news