RUWASA: Miradi 41 ya maji safi na salama inatekelezwa mkoani Mara

NA FRESHA KINASA

MENEJA wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Mara, Mhandisi Tulinumpoki Mwakalukwa amesema, kwa mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya miradi 41 yenye thamani ya shilingi Bilioni 16.7 inatekelezwa mkoani humo.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 13, 2022 ofisini kwake, ambapo pia amesema kati ya wananchi 1,827,532 wanaoishi vijijini kati yao 1,297,548 wanapata maji safi na salama sawa na asilimia 65 huku ifikapo mwezi Juni, 2022 akisema upatikanaji wa maji safi na salama utafikia asilimia 72 baada ya miradi inayoendelea kutekelezwa hivi sasa kukamilika.

Ameongeza kuwa, hadi kufikia mwakani watakuwa wamefikia asimimia 81 katika kuelelekea malengo ya Serikali ifikapo 2025 wafikie asilimia 85 ya upatikanaji wa maji safi na salama vijijini.

Amesema, RUWASA inaendelea na utoaji wa elimu kwa wananchi ili washiriki kuitunza miradi katika maeneo yao pamoja na kuilinda iwe endelevu, sambamba na kuwashirikisha kuanzia ngazi ya usanifu wa miradi katika maeneo yao.

Sambamba na kuwajengea moyo wa kuthamini miradi hiyo ambayo Serikali inatumia fedha nyingi kwa manufaa yao.
"Tangu RUWASA ilipoanza mwaka 2019, Mkoa wa Mara upatikanaji wa maji umeongezeka kutoka asilimia 50-65, miradi ya maji tisa kati ya 11 imefufuliwa iliyokuwa imesimama kwa muda mrefu, miradi mipya 19 inatekelezwa. RUWASA pia inajipanga kuwezesha ajira kwa miezi sita kwa watumishi watakaosimamia miradi ambapo Makatibu, wahasibu, mafundi watakuwa wakilipwa kwa muda wa miezi sita kusudi kuwezesha miradi inayoanza iimarike kiuchumi ndani ya muda huo,"amesema Mhandisi Mwakalukwa.

Akizungumzia changamoto Mhandisi Mwakalukwa amesema kuwa, RUWASA inakabiliwa na ukosefu wa usafiri yakiwemo magari na pikipiki katika kuwezesha kufanya ufuatiliaji wa miradi yake kwa ufanisi.

"Usafiri bado ni changamoto kubwa, ingawa tumejipanga kuona namna ya kutatua changamoto hii walau kwa kupata pikipiki ambazo zitasaidia katika ufuatiliaji wa miradi kwa bajeti ya mwaka huo ujao," amesema Mhandisi Mwakalukwa.

Ameongeza kuwa, RUWASA Mkoa wa Mara itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kushirikisha wananchi, viongozi wa ngazi za chini, wakuu wa wilaya pamoja na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi katika kuhakikisha wananchi wa vijijini wananufaika na huduma ya maji safi na salama kukidhi dhamira ya Serikali ya kumtua mama ndoo kichwani.
Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini ( RUWASA) umeanzishwa chini ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Namba 5 ya mwaka 2019. 

RUWASA ilianza rasmi shughuli zake Julai 1, 2019 makao makuu yake yakiwa jijini Dodoma.Ambapo dira ni kuwa na Jamii ya Wananchi waishio vijijini inayopata huduma za maji safi na salama ya kutosha na ya uhakika pamoja na huduma ya usafi wa mazingira.

Dhima ya RUWASA ni kutoa huduma ya maji Safi na Salama na kuhakikisha usafi wa mazingira kwa jamii iishio vijijini kwa kufanya usanifu, ujenzi kusaidia uendeshaji wa matengenezo ya miundombinu na utoaji wa huduma kwa ajili ya kuboresha maendeleo ya kiuchumi na kijamii. 

Huku ikisisitiza watumishi wake kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia tunu ikiwemo uadilifu, Ubunifu, huduma bora, ushirikiano na weledi.

Baadhi ya majukumu ya RUWASA ni kufanya matengenezo makubwa ya miundombinu ya maji vijijini, kuendeleza vyanzo vya maji kwa kufanya utafiti wa maji chini ya ardhi, kuchimba visima na kujenga mabwawa, kuandaa mipango kusanifu miradi ya maji kujenga na kusimamia uendeshaji wake, kuzijengea uwezo CBWSOs kwa kutoa mafunzo na utaalamu wa uendeshaji na matengenezo ya miradi ya maji vijijini.Majukumu mengine, ni kuhamasisha jamii na kutoa elimu ya usanifu wa mazingira katika ngazi ya kaya na masuala ya uhifadhi wa utunzaji wa vyanzo vya maji, kutafuta fedha za uendeshaji na kuiwezesha RUWASA kutekeleza majukumu yake na kushirikiana na wadau mbalimbali katika masuala yanayohusu utoaji wa huduma za maji na Usafi wa Mazingira vijijini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news