Watakiwa kurejesha mikopo kwa wakati na wengine wanufaike

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WANAWAKE wajasiriamali ambao wako kwenye majukwaa ya uwezeshaji kiuchumi kwenye Halmashauri ya Mji Kibaha wametakiwa kurejesha fedha za mikopo kwa wakati ili wengine nao waweze kukopa.
Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Diwani wa Viti Maalum, Shufaa Bashari wakati wa Uzinduzi na Ufunguaji Mfuko wa Jukwaa la Uwezeshaji kwenye Kata Picha ya Ndege.

Bashari amesema kuwa, fedha ambazo hutolewa kwa ajili ya kukopeshana lazima wakopaji warejeshe marejesho yao kwa muda waliopangiwa ili na wengine waweze kukopa.

"Waliokopa wasikimbie madeni yao badala yake warejeshe fedha kwani wanapokimbia husababisha biashara kufa na kuwakwamisha wakopaji wengine,"alisema Bashari.

Alisema kuwa, wanampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhamasisha vikundi vya uwezeshaji kwani wanaweza na wasijitie unyonge na wasikate tamaa.

"Hata kama mitaji yenu ni midogo anzeni hapo hapo kwani biashara nzuri ni ile inayoanza kwa udogo na hukuwa na kuwa kubwa na kuweza kufikia ndoto zenu," alisema Bashari.

Awali akisoma risala ya jukwaa hilo katibu wa jukwaa, Akothlilian Bake alisema kuwa malengo ya kuanzishwa jukwaa hilo ni kuwainua kiuchumi wanawake kwenye kata ya Picha ya Ndege.

Bake alisema kuwa pia ni kutoa mikopo yenye riba nafuu na kuwawezesha wanachama kwa kuwaunganisha na taasisi za mikopo kuwatafutia masoko ya biashara.

Kwa upande wake mwakilishi wa Benki ya CRDB, Elia Mapunda akitoa elimu juu ya ukopaji fedha alisema kuwa ili mkopaji aweze kunufaika na mkopo ni vema akatoa asilimia 60 na asilimia 40 ndiyo iwe ya kukopa.

Mapunda alisema kuwa kikubwa ni fikra au mawazo ya biashara na siyo fedha kwani mtaji mkubwa ni namna gani ya kutumia fursa zilizopo na kuzifikia na pia wanapaswa kuzijua biashara zao kwa asilimia 100.

Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Msaada wa Kisheria (KPC), Catherine Mlenga alisema kuwa ili waweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi wasikubali kunyanyasika kwa kutoa taarifa mara wanapofanyiwa vitendo vya ukatili.

Mlenga alisema kuwa baadhi wanafanyabiashara wakiwa na msongo wa mawazo hivyo biashara zinakwama hivyo wanapaswa kupaza sauti na kutokaa kimya wanapofanyiwa.

Mwenyekiti wa jukwaa hilo, Zawadi Salim alisema kuwa changamoto kubwa ni baadhi ya wanawake kutoona umuhimu wa kujiunga kwenye mabaraza hayo.

Salim alisema kuwa moja ya malengo ni kuwa na biashara za pamoja ambazo zitatengenezwa kwa kuzingatia ubora na kuzipeleka sokoni ili zishindane na nyingine.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news