Serikali kufanikisha mradi mkubwa wa maji Dar

NA LILIAN LUNDO-MAELEZO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kuwa, serikali inaenda kutekeleza mradi mkubwa wa maji wa Bwawa la Kidunda ambao utawezesha kuwepo kwa uhakika wa maji katika kipindi chote cha mwaka katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo ya mkoa wa Pwani.
Rais Samia amesema hayo Machi 22, 2022 alipokuwa akitoa hotuba yake katika kilele cha maadhimisho ya wiki wa maji Mlimani City jijini Dar es Salaam.

“Tunakwenda kujenga Bwawa la Kidunda ni la gharama na litachukua muda, takribani miaka mitatu. Kama tutaanza mwaka huu, nadhani tutakwenda kumaliza mwaka 2025, litachukua muda lakini Dar es Salaam tutakuwa na uhakika wa kupata maji. Maji ya bwawa hilo yatatumika kwa ajili ya matumizi ya binadamu, mifugo na kilimo,”amefafanua Rais Samia.

Vilevile amesema kuwa, ameielekeza Wizara ya Maji kufanya utafiti wa kuweza kutumia maji ya mto Rufiji ili uweze kusambaza maji Pwani, Rufiji hadi Dar es Salaam, ambao pia ni mradi mkubwa na utatekelezwa na serikali ya awamu ya Sita kwani maji ni Uhai na hakuna mbadala wa maji.

Aidha, ameipongeza Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa kazi nzuri inayofanya kwa mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Pwani, Chalinze, ambapo kwa sasa upatikanaji wa maji katika maeneo hayo upo katika viwango vya juu na kwa upande wa Dar es Salaam upatikanaji wa maji umefikia asilimia 96.

Rais Samia amesema kuwa, serikali anayoiongoza itaendelea kuiwezesha Wizara ya Maji ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo, ambapo kwenye fedha za Uviko-19 serikali ilitoa shilingi Bil. 139 kwenda sekta ya maji, kwani maji ni uhai na ni kipaumbele cha serikali ya awamu ya Sita.

Pia ametoa wito kwa Watanzania, kutunza mazingira hasa uoto wa asili kwa kuepuka kukata au kuchoma miti ovyo au kufyeka misitu ovyo, "tuepuka shughuli nyingine za kibinadamu karibu na vyanzo vya maji, hizi shughuli zinapaleke vyanzo kukata maji" alisisitiza Rais Samia.

Kwa upande wake Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja tangu Rais Samia ameingia madarakani Wizara ya Maji imekamilisha jumla ya miradi 463, pia inakwenda kutekeleza miradi 1176 ya maji vijijini na miradi 114 ya mjini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news