SERIKALI YA KOREA YATOA MILIONI 232/- KUFADHILI UKARABATI CHUMBA CHA UTAKASAJI VIFAA TIBA HOSPITALI YA RUFAA TUMBI,BALOZI WA KOREA AAHIDI KUSAIDIA ZAIDI TANZANIA

NA ROTARY HAULE

SERIKALI ya Korea kupitia taasisi yake ya Korea Foundation for International Healthcare (KOFIH) imetoa kiasi cha Sh.milioni 232 kwa ajili ya kufadhili ukarabati wa chumba cha kutakasia vifaa tiba katika Hospitali ya Rufaa ya Tumbi iliyopo Kibaha mkoani Pwani.
Ukarabati wa chumba hicho ulianza mapema mwaka huu na tayari kimekamilika wiki iliyopita ambapo Balozi wa Korea hapa nchini, Kim Sun Pyo alikuwa mgeni rasmi katika makabidhiano na uzinduzi wake.

Akiwa katika hafla ya uzinduzi huo uliofanyika juzi hospitalini hapo Balozi Pyo amesema kuwa, Serikali ya Korea inatambua changamoto zilizopo katika Sekta ya Afya hapa nchini ndio maana wanajitoa katika kusaidia.

Pyo amesema kuwa, msaada huo sio wa kwanza bali Serikali ya Korea kupitia taasisi yake ya KOFIH ilianza kusaidia Hospitali ya Tumbi katika kukarabati wodi ya watoto mahututi (ICU ya watoto) chini ya siku 28 (Neonatal Intensive Care Unit).
Aidha,amesema kutokana na umuhimu wa sekta ya afya nchini Serikali ya Korea itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha wanaendelea kutatua changamoto zote zilizopo katika sekta afya.

"Msaada huu tuliotoa hapa hospitali ya Rufaa ya Tumbi utakuwa endelevu, lakini tutafika katika hospitali nyingine zilizopo hapa nchini kwa kuwa lengo letu ni kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kutatua changamoto za afya,"amesema Pyo.

Pyo ameongeza kuwa, uchumi imara wa nchini unajengwa na wananchi wenye afya njema ndio maana taasisi yake imejikita katika masuala ya afya na kwamba anaamini kupitia ushirikiano huo Tanzania itakuwa na watu imara katika kujenga uchumi.
Awali Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi,Dkt.Amaani Malima, ameishukuru Serikali ya Korea kupitia Taasisi ya KOFIH kwa ufadhili mkubwa waliohufanya hospitalini hapo.

Dkt .Malima amesema kuwa, kutokana na ongezeko la uhitaji wa vifaa tiba safi na salama vilivyotakaswa kwa kufuata sheria na taratibu za kitabibu na kukidhi mahitaji ya wagonjwa uongozi wa Hospitali uliona kuna umuhimu wa kuwa na chumba cha kutakasia vifaa tiba.

Amesema, upatikanaji wa chumba hicho utasaidia kurahisisha utoaji wa huduma kwa wagonjwa ambao ni majeruhi,wahitaji wa huduma za upasuaji,huduma za kusafisha vidonda na huduma nyingine zinazohusiana.
"Natumia fursa hii kuishukuru Serikali ya Korea kupitia Taasisi ya KOFIH kwa msaada huo muhimu ambao umekuja wakati muafaka,chumba hiki cha kutakasia vifaa tiba kitarahisisha upatikanaji wa utakasaji wa vifaa kwa wagonjwa ili kupunguza maambukizi,"amesema Dkt.Malima.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani Dkt.Gunini Kamba,amesema kuwa katika fedha hizo vifaa na ukarabati wa vyumba vya kutakasia imetumika Sh. milioni 52.6 huku ununuzi wa mashine na kusimika ni Sh. milioni 179.9.
Dkt.Kamba, amesema chumba cha kutakasia vifaa tiba kimegawanyika katika vyumba vinne kikiwemo chumba cha kupokelea vifaa vilivyotakaswa kwa wagonjwa na kuvisafisha,chumba cha kuchemshia vifaa,chumba cha kuandalia vifaa tayari kwenda kuchemshwa na chumba cha kuhifadhia na kutolea vifaa vilivyosafi na salama.

Hata hivyo,Dkt.Kamba ameiomba Taasisi ya KOFIH kuendelea kusaidia hospitali hiyo katika ujenzi wa wodi ya mama na watoto ili kurahisisha utoaji wa huduma pindi wanapokuja hospitalini hapo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news