Serikali yaitaka TARI kukuza uzalishaji wa ngano nchini

NA MWANDISHI MAALUM-TARI

NAIBU Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Anthony Mavunde amekitaka Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) Seliani kuhakikisha kinakuja na mkakati na ubunifu katika uzalishaji wa mbegu bora.
Sambamba na kuongeza maeneo zaidi ya uzalishaji mbegu ili kusaidia kukuza zao la ngano hapa nchini kwa kuongeza uzalishaji kutoka tani laki moja zinazozalishwa hivi sasa.
Naibu Waziri Mavunde ameyasema jijini Arusha wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za Kituo cha TARI Seliani ambacho kina jukumu la msingi la utafiti wa mazao ya ngano,shayiri na maharage.

“Lazima tuhakikishe tunapunguza uingizwaji wa ngano nchini, kwa sisi kama nchi kuzalisha ngano kwa wingi,na ninyi TARI Seliani ndio mna jukumu hili kubwa la utafiti na ugunduzi wa mbegu bora kwa lengo la kuongeza tija na uzalishaji wa ngano nchini,"amesema.
Pia amesema kuwa, "Wataalamu na watafiti mliopo hapa kama kuna heshima kubwa mtaipata ni kusaidia uzalishaji wa ngano hapa nchini kukua na kuipunguzia nchi gharama kubwa ya fedha ya kuagiza ngano nje ya nchi.Lazima utaalamu wenu na elimu mlizonazo zikatafsiriwe katika maendeleo ya mkulima na kilimo cha nchi hii.

"Hakikisheni mnatenga eneo kubwa zaidi la shamba za uzalishaji mbegu bora za ngano,mtenge bajeti ya mifumo ya umwagiliaji badala ya kutegemea mvua ilivyo hivi sasa, na maeneo hayo yatafutieni hati miliki zake na lazima yawekewe uzio ili kuyatenganisha na shughuli za kibinadamu na wanyama.
"Sisi kama wizara tutakuwa tayari kutoa ushirikiano mkubwa ili malengo haya ya kukuza sekta ya kulima kupitia zao la ngano kuona yanafanikiwa,na hasa katika eneo la bajeti ya kusimamia vituo hivi vya utafiti wa kilimo,"amesema Mavunde.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Seliani, Rose Ubwe ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuongeza bajeti ya fedha za utafiti hadi kufikia shilingi bilioni 11.7 kwa mwaka 2021/22 na kuahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa kwa mustakabali wa maendeleo ya zao la ngano hapa nchini na hasa katika kuongeza uzalishaji kupitia tafiti mbalimbali na kanuni bora za kilimo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news