Serikali:Hakuna muda wa nyongeza miradi ya maji fedha za UVIKO-19

NA DERICK MILTON

NAIBU Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi amewaagiza mameneja wa wilaya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) nchi nzima kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa kwa fedha za maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi UVIKO-19 inakamilika kabla ya mwezi Juni, mwaka huu.
Naibu Waziri wa Maji,Maryprisca Mahundi akizungumza na viongozi na Wilaya ya Busega mkoani Simiyu pamoja na watendaji wa RUWASA Wilaya na Mkoa, katika siku yake ya kwanza ya ziara yake mkoani humo.

Amesema kuwa hakutakuwa na nafasi ya maelezo kwa meneja yeyote ambaye atashindwa kukamilisha miradi hiyo kwa muda muafaka, ambapo ameagiza miradi yote inatakiwa kukamilika mwezi Mei, mwaka huu.

Naibu Waziri huyo ametoa maagizo hayo leo katika siku yake kwanza ya ziara yake mkoani Simiyu ambapo akiwa wilayani Busega amemtaka Meneja wa RUWASA wilayani humo ambao wanatekeleza miradi miwili ya UVIKO-19 kuhakikisha inakamilika kwa muda.

Amesema kuwa, miradi yote ya UVIKO-19 mbali na kukamilika ujenzi wake, inatakiwa kutoa maji na wananchi wanaanza kutumia na siyo kukamilika kwa kujengwa tu bali inatakiwa kabla ya muda huo ianze kutoa maji.

Amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameleta fedha hizo kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa UVIKO-19, ambapo moja ya njia za mapambano ni wananchi kunawa mikono kwa maji safi na tiririka.

“Kunawa maji safi na tiririka ni lazima kila mradi ukamilike ujenzi wake kwa asilimia 100 na siyo kukamilika,halafu tunaambiwa kuna kitu fulani hakijakamilika, hapana…tunataka maji yatoke na wananchi waanze kutumia.
“Kwenye hii miradi kama wizara hatuna excuse (udhuru) kwa Meneja yeyote wa wilaya, wala hatuna muda wa ziada kwa ambaye mradi utashindwa kukamilika kwa muda, tunataka miradi ikamilike kabla ya mwezi wa tano na itoe maji kwa wananchi,”ameongeza Naibu Waziri.

Amewataka mameneja kuhakikisha wanawasimamia wakandarasi wanaojenga miradi hiyo kwani muda uliobaki ni mchache sana na inatakiwa kukamilika ndani ya muda muafaka.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maji ndani ya Wilaya ya Busega, Meneja wa RUWASA wilaya hiyo, Mhandisi Samson Gagala amesema kuwa walipokea zaidi ya shilingi milioni 450 fedha za UVIKO-19 kwa ajili ya kutekeleza miradi miwili ya maji.

Mhandisi Gagala amesema kuwa, miradi hiyo inatekelezwa katika vijiji vya Badugu na Kalemela ambapo ujenzi wake kwa miradi yote miwili umefikia kiwango cha asilimia 25.

“Kukamilika kwa miradi hii yote miwili itahudumia zaidi ya wananchi 8000, lakini katika wilaya tunayo mingine ambayo inajengwa kwa fedha za lipa kulingana na matokeo (P4R) zaidi ya sh.milioni 900,"amesema.

Naye Mkuu wa wilaya hiyo, Gabriel Zacharia amesema kuwa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi ni asilimia 65 kutoka asilimia 39 wakati RUWASA inaanzishwa.

Amemshukuru Rais Samia kwa kuwaleta fedha nyingi katika miradi ya maji, kwani kukamilika kwa miradi hiyo kutaifanya Wilaya hiyo asilimia kubwa ya wananchi ndani ya Wilaya hiyo kupata maji safi na salama.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news