Simanzi zatawala Chuo Kikuu Mzumbe, kifo cha Profesa Ngowi na dereva wake

*Baraza, Menejimenti, Wafanyakazi na Jumuiya nzima ya Chuo Kikuu Mzumbe watoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

CHUO Kikuu cha Mzumbe kimesema Kaimu Mkuu wa Chuo hicho Ndaki ya Dar es Salaam, Prof. Prosper Ngowi ambaye amefariki dunia pamoja na dereva, Innocent Mringo, kwa ajali ya gari alikuwa mhimili muhimu katika Menejimenti ya chuo hicho.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chuo Kikuu Mzumbe,Bi. Rose Joseph.

Amesema,Makamu Mkuu wa chuo hicho, Prof. Lughano Kusiluka amebainisha kuwa,Prof. Ngowi alikuwa muhimili wa chuo hicho hususani katika usimamizi wa shughuli za kitaaluma Ndaki ya Dar es Salaam, mbunifu, na msimamizi mahiri wa miradi ya maendeleo, utafiti, machapisho na elimu kwa umma.
"Baraza, Menejimenti, Wafanyakazi na Jumuiya nzima ya Chuo Kikuu Mzumbe, tunatoa pole kwa Familia ya Marehemu Prof. Prosper Honest Ngowi, na Innocent Gerson Mringi, Ndugu, Jamaa na Marafiki wote waliogushwa na msiba huu mzito, Daima tutawakumbuka na kuuenzi mchango wao mkubwa kwa kipindi chote cha utumishi wao katika kuendeleza Chuo Kikuu Mzumbe,"imeeleza taarifa hiyo.

Pia taaarifa hiyo imethibitisha kuwa Profesa Ngowi na dereva Mringo wamepata ajali hiyo katika eneo la Mlandizi katika mkoa wa Pwani, wakiwa njiani wakitokea Dar es Salaam, kwenda Kampasi Kuu ya Chuo hicho, Morogoro kwa ajili ya shughuli za kikazi.

"Mipango ya mazishi inaendelea kwa kushirikiana na familia za marehemu, na mara taratibu zitakapokamilika, Umma utajulishwa,"imesema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imesema, Prof. Ngowi aliajiriwa na Chuo Kikuu Mzumbe mwaka 1994 kuwa Mkufunzi Msaidizi, baada ya kuhitimu Stashahada ya Juu ya Mipango na Uchumi.

Baadae alijiendeleza na kupata Shahada ya Kwanza, Shahada ya Umahiri katika Biashara na Uchumi, na baadae mwaka 2014 alihitimu Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Uchumi.

Mwaka 2015 alipandishwa cheo na kuwa Profesa Mshiriki, na kuongoza Idara mbalimbali za Chuo Kikuu Mzumbe kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Ndaki ya Dar es Salaam hadi umauti ulipomkuta, leo.

Mbali na kushika nafasi za uongozi Prof. Ngowi amekuwa Mjumbe wa Bodi mbalimbali za Taasisi za Umma na Binafsi, Bodi za Kitaaluma, Mshauri na mchambuzi wa masuala ya kiuchumi na biashara, Mtafiti, Mshauri na Mwandishi wa Makala mbalimbali za uchumi, na mtoa mada katika makongamano ya kitaifa na kimataifa.
Kwa upande wa dereva, Innocent Gerson Mringo, taarifa imesema, aliajiriwa na Chuo Kikuu Mzumbe kuwa Dereva Daraja la Pili mwaka 2017 hadi umauti ulipomkuta leo.

Alipata mafunzo yake ya udereva na kuhitimu Chuo cha Taifa cha Usaririshaji mwaka 2016, na VETA mwaka 2017.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news