Tanzania yapokea Sinovac dozi milioni 1 za UVIKO-19 kutoka Uturuki

NA MWANDISHI WETU

WIZARA ya Afya imepokea jumla ya dozi milioni 1 za chanjo ya UVIKO-19 aina ya Sinovac kutoka nchini Uturuki.
Akizungumza leo Machi 23, 2022 wakati wa mapokezi ya chanjo hiyo yaliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ameishukuru Serikali ya Uturuki kwa ufadhili huo.

Waziri Ummy amesema kuwa, jumla ya dozi milioni nne za chanjo aina ya Sinovac zinatarajiwa kupokelewa kutoka nchini uturuki kwa awamu nne huku zikitarajiwa kuchanja watu milioni mbili.

"Tunaishukuru Serikali ya Uturuki kwa kutupatia ufadhili wa chanjo aina ya Sinovac, jumla ya dozi 1,000,000 kati ya 4,000,000 zinazotarajiwa kupokelewa kwa awamu nne. Chanjo hizi zinatarajiwa kuchanja watu 2,000,000,"amesema Waziri Ummy.
Ameongeza kuwa hii ni mara ya kwanza kwa nchi ya Tanzania kupokea chanjo aina ya Sinovac tangu zoezi la kuchanja lilipozinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan mnamo Julai 28,2021.

Waziri ummy amesema kuwa, hadi sasa jumla ya chanjo zilizopokelewa nchini ni dozi 10,845,774 zikijumuisha aina ya Sinopharm, Janssen, Moderna,Pfizer na Sinovac ambazo zinatosha kuchanja watu 6,381,327.

Amesema kuwa, hadi kufikia Machi 21, 2022 zaidi ya watu milioni 3 wamepata chanjo kamili kati ya zaidi ya watu milioni 30 wenye umri wa kati ya miaka 18 na kuendelea.

"Watu milioni 3,016,551 wamepata chanjo kamili kati ya watu milioni 30,740,928 wenye umri wa miaka 18 na kuendelea, hii ni sawa na asilimia 9.8," amefafanua Waziri Ummy.

Ameongeza kuwa hadi kufikia mwisho wa mwaka 2022, Serikali inalenga kuchanja asilimia 70 ya Watanzania kuanzia umri wa miaka 18.

"Niendelee, kuwasihi Wananchi, wajitokeze kwa wingi kwenda kupata chanjo na waendelee kuchukua tahadhari zote za kinga dhidi ya UVIKO-19," amesisitiza Waziri Ummy

Aidha, ametoa wito kwa viongozi na watendaji wa ngazi zote kuendelea kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaendelea kuhimizwa kwenda kwenye vituo vya huduma za afya ili wakapate elimu kuhusu umuhimu wa chanjo na kisha kuchanja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news