TARURA kuanza kutumia Mfumo wa Maegesho Kidigitali mkoani Kilimanjaro

*RC Kagaigai atoa wito kwa wananchi, utekelezaji kuanza Aprili Mosi, 2022

NA MWANDISHI MAALUM

WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) unatarajia kuanza kutumia Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji Ushuru wa Maegesho mkoani Kilimanjaro kuanzia Aprili 1, 2022.
Akizungumza katika semina ya kuwajengea uwezo wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Mhe Stephen Kagaigai amewataka wananchi wa mkoa huo kuupokea na kuutumia mfumo huo mara utakapoanza ili kuwezesha malipo yote yatakayofanyika kwenda moja kwa moja serikalini.
Kiongozi huyo amefafanua kuwa, mfumo huo ni mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji ushuru wa maegesho ya vyombo vya moto, matumizi ya hifadhi za barabara pamoja na tozo za adhabu kutokana na ukiukwaji wa matumizi ya hifadhi za barabara zinazosimamiwa na TARURA.

Aidha, Mkuu wa Mkoa amesisitiza kuwa ni wajibu wa TARURA kutoa elimu kwa wananchi wawe na uelewa wa kutosha ili malipo yote yatakayofanyika TARURA yafanyike Kidigitali kwa kutumia Kumbukumbu namba ya malipo ambapo malipo yote yataenda moja kwa moja serikalini na kuondoka mianya ya upotevu wa fedha ya Serikali.
Ameongeza kuwa mfumo huo una faida nyingi ikiwemo kuongeza ufanisi wa ukusanyaji mapato ya serikali yatakayosaidia maboresho na maendeleo ya miundombinu ya barabara, utasaidia wateja kufanya maombi na kulipia huduma kwa njia ya mtandao bila kufika ofisi ya TARURA, utampa mteja fursa kulipia ushuru wa maegesho kwa saa moja na zaidi.

Kwa siku,wiki au mwezi, utatoza ushuru wa vyombo vya moto vilivyoegeshwa kwenye maeneo ya maegesho tu kwani mfumo ni rafiki, rahisi na salama na mtumiaji atatumia mtandao wowote wa simu ya mkononi, benki ya NMB na CRDB au kupitia kwa mawakala.
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ulianza rasmi matumizi ya mfumo wa maegesho Kidigitali mwezi Aprili 2021 ambapo hadi sasa mfumo unafanya kazi katika Mikoa ya Iringa, Singida, Mwanza, Dodoma na Dar es Salaam.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news