NA FRESHA KINASA
MKUU wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Ally Hapi amezitaka taasisi za umma na viongozi wote wa Serikali mkoani humo kuwathamini waandishi wa habari wa mkoa huo kutokana na mchango wao mkubwa katika kufichua maovu, kutangaza kazi na miradi mbalimbali ya maendeleo inayofanywa na Serikali, hivyo amesisitiza wapewe ushirikiano katika uwajibikaji wao kwa manufaa ya wananchi.
Amebainisha kwamba, waandishi wa habari mkoani humo wameendelea kufanya kazi nzuri ikiwemo kiripoti shughuli mbalimbali zinazofanywa na Serikali na kufichua maovu, hatua ambayo inaisaidia pia Serikali kufanya ufuatiliaji na kuchukua hatua katika maeneo husika.
Amewaasa viongzozi katika maeneo mbalimbali mkoani Mara kujenga ushirikiano thabiti na waandishi wa habari, hatua ambayo pia itaimarisha uwajibikaji kwa viongozi katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Hapi ameongeza kuwa, ataendelea kuwathamini, kuwapa ushirikiano na kushirikiana na waandishi wa habari katika kutangaza kazi mbalimbali za maendeleo zinazofanywa na Serikali mkoani humo ili fursa mbalimbali za mkoa wa zifahamike na zizidi kuchangia kuleta mapinduzi chanya ya kimaendeleo katika nyanja za kiuchumi na kijamii.