Waziri Dkt.Biteko aanika mafanikio ya Sekta ya Madini nchini kuelekea Mwaka Mmoja wa Uongozi wa Rais Samia madarakani

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WIZARA ya Madini imetaja mafanikio nane ambayo imeyapata katika kipindi cha mwaka mmoja wa Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ikiwemo kusaidia kuongezeka kwa Pato la Taifa.
Waziri wa wizara hiyo, Dkt. Doto Biteko ameyasema hayo leo Machi 10,2022 jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya wizara hiyo kuelekea Mwaka Mmoja wa Uongozi wa Rais Samia madarakani.

Dkt.Biteko amesema, chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa umekuwa ukiongezeka kutoka robo moja ya mwaka hadi nyingine.

Mchango wake

Dkt.Biteko amesema, katika kipindi cha Januari hadi Septemba, 2021 wastani wa mchango wa sekta hiyo umekuwa hadi kufikia asilimia 7.3 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na wastani wa asilimia 6.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2020.

Aidha, katika robo ya tatu (Julai Hadi Septemba) mwaka 2021, mchango wa Sekta ya Madini umeongezeka hadi kufikia asilimia 7.9 ya Pato la Taifa kutoka asilimia 7.3 ya Pato la Taifa katika kipindi kama hicho mwaka 2020.

“Matokeo haya yanaakisi dhamira ya Serikali kuhakikisha sekta hii inaimarika na kuweza kuchangia Pato la Taifa kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2025 kama ilivyotangazwa kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa na Mpango wa Maendeleo,”amesema.

Mauzo Trilioni 8.3

Amesema, kwa kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, sekta ya madini imeweka historia kwa kushuhudia mauzo ya moja kwa moja yenye thamani ya shilingi trilioni 8.3 kutokana na mauzo ya madini ya aina mbalimbali.

Amesema, mauzo hayo yanatokana na madini ya dhahabu, fedha, shaba, makaa ya mawe,kinywe, madini ya vito na madini ya ujenzi na viwandani.

Maduhuli

Waziri Dkt.Biteko amesema, kutokana na biashara ya madini hayo, wizara imekusanya Shilingi Bilioni 597.53 kama maduhuli ya Serikali yaliyokusanywa kupitia wizara hiyo.

Vile vile, ushiriki wa Watanzania kwenye shughuli za madini umekuwa kutoka asilimia 48 hadi asilimia 63 na hivyo kuongeza thamani ya huduma migodini kufikia thamani ya dola za Marekani milioni 579.3 sawa na Shilingi Trilioni 1.33 kutokana na huduma zilizotolewa migodini.

“Kwa sasa wizara imeongeza usimamizi kwenye madini ya ujenzi na viwandani ambapo tayari mifumo ya kielekroniki imeanza kutumika katika usimamizi wa mapato ya Serikali yatokanayo na madini hayo,"amesema Dkt.Biteko.

Amesema, katika juhudi za kusimamia upatikanaji wa mapato kutokana na madini ya ujenzi na viwandani, Wizara ya Madini imeanza ushirikiano na Wizara ya TAMISEMI ili kuweza kuwafikia wananchi wanaotumia madini hayo waweze kuchangia fedha zitokanazo na shughuli za uchimbaji.

Wachimbaji wadogo

Waziri Dkt.Biteko amesema, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeendelea kusimamia na kuhakikisha wachimbaji wadogo wanashiriki kikamilifu na kwa ufanisi kwenye uzalishaji madini hapa nchini.

Amesema, katika usimamizi huo, kwa sasa wachimbaji wadogo wanachangia zaidi ya asilimia 30 kwenye mapato yatokanayo na madini.

“Kiasi hiki ni cha juu ikilinganishwa na kiasi kidogo (asilimia 4 kabla ya marekebisho ya Sheria) kilichokuwa kikichangiwa na kundi hili muhimu katika Sekta ya Madini,”amesema.

Amesema, mafanikio hayo ni juhudi za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa Mheshimiwa Samia Suluhu, Rais wa Jamhuri ya Tanzania katika kuhakiksha wananchi wa kipato cha chini wanashiriki kwenye shughuli za madini na kunufaika na rasilimali za madini.

“Mchango huu wa wachimbaji Wadogo kwenye Sekta ya Madini unatokana na juhudi za Serikali ya awamu ya sita kuhakikisha huduma muhimu kwa wachimbaji kama masoko zinapatikana,”amesema.

Amesema, hadi sasa kuna masoko 44 na vituo vidogo vya kununulia madini ya dhahabu 70 ambapo amedai masoko hayo na vituo vya kununulia dhahabu vimeongeza uaminifu kwa wachimbaji wadogo kwa kuwa biashara sasa inafanyika kwa uwazi na uaminifu zaidi.


Taasisi za fedha

Waziri Dkt.Biteko amesema uwepo wa masoko umeongeza imani kwa taasisi za fedha katika kutoa huduma za kifedha kwa wachimbaji wadogo.

Amezitaja taasisi hizo ni Benki ya NMB, CRDB, NBC,Stanbic,Azania,Ecobank na Standard Chartered.

Amesema, jwa sasa benki za NMB, CRDB zimeanza kutoa mikopo kwa wachimbaji madini ambapo amezipongeza benki hizo.

“Hii ni dalili nzuri na ya kutia moyo katika maendeleo ya Sekta ya Madini na nchi yetu,"amesema Dkt.Biteko.

Leseni 8,172

Dkt.Biteko amesema, wameshuhudia utoaji wa leseni mbalimbali kwenye shughuli za madini ukiongezeka ambapo jumla ya leseni 8,172 zimetolewa, kati ya leseni hizo, leseni 5,937 ni za uchimbaji mdogo wa madini (Primary Mining Licence), leseni 282 ni za utafutaji wa madini (Prospecting Licence).

“Leseni 5 ni za uchimbaji wa kati wa madini (Mining Licence); leseni 2 ni za uchimbaji mkubwa wa madini (Special Mining Licence); leseni 49 ni za uchenjuaji wa madini (Processing Licence); leseni 2 ni za usafishaji wa madini (Refinery Licence).

“Leseni 1,531 ni za biashara ndogo ya madini (Broker Licence) na leseni 364 kubwa za biashara ya madini (Dealer Licence) zilitolewa kwa wawekezaji na wananchi, ikilinganishwa na jumla ya leseni 6,334 zilizotolewa katika kipindi cha kuanzia Machi 2020 mpaka hadi Februari 2021,"amesema.

Amesema,kati ya leseni zilizotolewa, takribani leseni 6 zenye uwekezaji mkubwa na kati zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji miradi hiyo.

Ameitaja miradi ambayo ipo tayari kuanza shughuli za uzalishaji ni ule wa Uchimbaji dhahabu wa Shanta Singida, mgodi wa Jumbo Lindi wa Uchimbaji Madini ya Kinywe (graphite) ambayo ipo katika hatua za ujenzi wa miundo mbinu, mgodi wa Tembo Lickel ambao umepata leseni kubwa ya uchimbaji madini ya Nickel.

Miradi mingine ni ule wa Nyanzaga ambao baada ya kusainiwa makubaliano umeshaanza shughuli za ujenzi wa mgodi.

Aidha, kati ya leseni nne za Usafishaji madini (refining) tayari leseni tatu zimekamilisha ujenzi wa miundombinu ya Usafishaji ambapo Refinery ya Mwanza imeshaanza shughuli za usafishaji madini ya dhahabu baada ya Mheshimiwa Rais kufungua mradi huo mkoani Mwanza mwezi Juni, mwaka 2021.

Mikataba

Dkt.Biteko amesema katika mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani, kwa mara ya kwanza katika historia ya Sekta ya Madini, Serikali ilifanikiwa kusaini mikataba mipya minne ya uchimbaji na uanzishwaji wa migodi mikubwa na ya kati ya madini kwa wakati mmoja.

“Ilikuwa tarehe 13 Desemba, 2021 ambapo dunia ilishuhudia Serikali ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na yeyé mwenyewe akiwepo kwenye tukio, ikisaini mikataba ya uwekezaji wenye thamani ya dola za Marekani milioni 735.79,”amesema.

Amesema, mikataba hiyo ilihusisha uchimbaji wa madini muhimu ya viwandani yanayotokana na mchanga wa baharini, madini ya dhahabu, almasi na madini ya kinywe (Graphite).

Tozo

Waziri Biteko amesema, juhudi mbalimbali zimefanyika kuwapunguzia adha za tozo zisizokuwa na tija kwa wananchi na wawekezaji katika sekta ya madini.

Amesema,marekebisho yamefanyika katika Sheria ya Madini, Sura 123 kwa vipengele ambavyo vilikuwa vinaleta mkwamo katika ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali.

Waziri huyo amesema, Tume ya Madini sasa inatoa leseni ndogo za biashara ya madini ya ujenzi na ya viwandani ambazo zitachochea na kuhamasisha wananchi kushiki kwenye uchimbaji na biashara ya madini haya na hivyo kuongeza wigo wa ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kupitia madini ujenzi na viwandani.

Pia amesema marekebisho mengine ya kisheria yaliyofanyika ni pamoja na kuruhusu Tume ya Madini kuruhusu uingizwaji wa madini kutoka nje ya nchi kuuzwa katika masoko ya ndani bila kutozwa VAT.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news