Wizara yatoa onyo kali kwa wavunaji rasilimali mchanga Zanzibar

NA DOREEN ALOYCE

NAIBU wa Waziri wa Maji,Nishati na Madini Zanzibar, Mhe. Shaaban Ali Othman ametoa onyo kali kwa yeyote atakayekiuka sheria za uvunaji wa rasilimali za nchi hususani mchanga kwani atachukuliwa hatua ikiwemo kuwajibishwa bila kujali cheo chake.

Pia ametahadharisha baadhi ya watendaji wa wizara hiyo ambao wanahusika kujua wanaofanya vitendo hivyo vya uvunaji holela wa rasilimali na kunyamaza jambo ambalo halitafumbiwa macho.
Ameyasema hayo wakati alipokuwa kwenye semina elekezi kwa wakuu wa wilaya, maafisa wa maliasili lengo likiwa ni kukumbushana na kujengeana uelewa wa pamoja kuhusiana na masuala ya sheria ambazo zinatumika katika kudhibiti na kuratibu masuala ya maliasili.
Amesema, semina hiyo ni baada ya kubaini kuwa kuna uelewa tofauti kwenye maeneo yale ya kiutawala hasa wizara inapopanga taratibu zake na utekelezaji haufanikiwi kadri ilivyokusudia.

Aidha, amesema kutokana na kinachoendelea hasa cha uvunjifu na ukiukwaji wa taratibu katika maeneo yao hasa uvunaji wa rasilimali mchanga wakaona ni vyema wakae pamoja ili wawe na mwelekeo wa mmoja namna ya kudhibiti rasilimali hizo.
Amesema kuwa,kumekuwa na ukiukwaji mkubwa ambapo fedha nyingi za Serikali zinapotea kutokana na mashimo mengi ambayo sio rasmi na wasafirishaji,wanunuzi ambao hawako kwenye mfumo.

"Wizara tumejipanga kusimamia hilo, hatutamfumbia macho atakayebainika kuvunja sheria, niwaombe warudi katika mfumo ambao umewekwa kisheria na sio vinginevyo lengo ni kuvuna na kuratibu na hatimaye kuwa na uelekeo mmoja kama Serikali.

"Nakuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara kuhakikisha kamati zitakazoundwa na wakuu wa wilaya yao watakaounda kamati za kutusaidia sisi kukamata rasilimali hizo na kuletwa hapa wizarani na wale wa kupigwa faini, wapigwe ili wapewe asilimia ili kuweka motisha kwao kutokana na gharama walizozitumia,"amesema.
Kwa upande wao wakuu wa wilaya walíiopata semina hiyo wamesema itaenda kuleta tija kuokoa rasilimali za nchi na kwamba wananchi watambue kuwa Zanzibar ni ndogo kama watachimba bila mpangilio itakuwa hasara kwa Taifa na vizazi vijavyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news