Askofu Michael Msonganzila awataka Watanzania kutenda mema, kujiepusha na maovu

NA FRESHA KINASA

ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Musoma mkoani Mara, Mhashamu Baba Askofu Michael Msonganzila amewaasa waumini wa kanisa hilo na Watanzania kwa ujumla kudumu katika kutenda matendo mema ikiwemo kuwasaidia watu wenye uhitaji na kujiepusha na vitendo viovu na vya kikatili, ambavyo ni kinyume cha sheria za nchi.
Ameyasema hayo Aprili 3, 2022 katika maadhimisho ya Misa Takatifu iliyofanyika katika Parokia ya Huruma ya Mungu Kiabakari wilayani Butiama ambapo pia, miradi mikubwa mitatu ya kimkakati ya Parokia hiyo ilizinduliwa.
Amesema kuwa, Wakristo wa kanisa hilo na Watanzania wote wanapaswa kuishi maisha ya ushuhuda mwema na kuwa kielelezo cha kusomeka vyema na kutoshiriki kufanya matendo maovu ambayo ni chukizo kwa Mungu. Bali waenende katika upendo kwa kusaidia watu wenye uhitaji na kumcha Mungu katika unyoofu wa moyo.

Pia, Mhashamu Baba Askofu Msonganzila amewasisitiza waumini wa kanisa hilo, kuendelea kuitunza na kuithamini miradi mbalimbali ya maendeleo inayojengwa na wafadhili iweze kudumu na kuwa na manufaa endelevu kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
Miradi hiyo iliyozinduliwa, imejengwa kwa ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Serikali ya Jamhuri ya Poland kupitia Mpango wa Polish Aid 2021 kwa kushirikiana na Kiabakari Foundation.

Mradi wa kwanza ni hosteli ya ghorofa mbili kwa ajili ya wanafunzi 200 yenye vyumba 20 katika Shule ya Msingi Edmond Blessed. Jengo hilo limewekewa miundombinu ya kisasa inayowezesha upatikanaji wa huduma za maji na umeme na huduma zote muhimu.
Hosteli hiyo pia imewekewa matenki 14 ya maji yenye ujazo wa lita 5,000 kila moja na taa za barabarani zinazotumia mwanga wa jua ndani ya mazingiara ya shule.

Mradi wa pili ni kituo cha Afya chenye jina la Mvua na Jua Lengo Moja ambacho kimejengwa kisasa kikiwa na miundombinu ya kuteketeza taka, mifumo thabiti ya maji na Umeme wa jua ambao unaotosheleza mahitaji ya kituo katika kutoa huduma za matibabu.

Mradi wa tatu ni kituo cha kisasa cha kilimo na ufugaji chenye mabanda ya nguruwe, kuku, ng'ombe wa maziwa, trekta, mitambo mbalimbali na vifaa vingine kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji.
Kwa upande wake Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Poland chini Tanzania Mheshimiwa Katarzyna Sobiecka amesema kuwa, nchi hiyo imeendelea kushirikiana na Tanzania katika kuwezesha miradi mbalimbali ikiwemo ya elimu, miundombinu kwa ustawi bora wa wananchi.

Aidha, amepongeza pia uongozi wa Parokia ya Kiabakari kwa kazi nzuri na ushirikiano walio nao na jamii hali ambayo imewezesha miradi iliyotekelezwa kufanyika kwa ufanisi mkubwa na kwamba, itakidhi malengo yaliyokusudiwa.
Mgeni Rasmi aliyezindua miradi hiyo ni Meja Jenerali mstaafu wa Jeshi la Kujenga Taifa nchini (JKT), Michael Isamuyo ambapo ameshukuru hatua ya Poland kutoa fedha ambazo zimewezesha kutekelezwa kwa miradi hiyo itakayokuwa na manufaa makubwa kwa jamii huku akiomba pia waumini wa kanisa hilo kuendelea kujitoa kufanikisha shughuli za maendeleo ya kanisa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news