CAG abaini kasoro mashirika 14,wanaume kuingizwa katika huduma ya kujifungua

NA DIRAMAKINI

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG Charles Kichere ametaja mashirika 14 ya kibiashara yaliyopata hasara kwa miaka miwili kuanzia mwaka wa fedha 2019/20 na 2020/21.

CAG Kichere ameyasema hayo leo Aprili 12,2022 jijini Dodoma baada ya asubuhi kuiwasilisha ripoti yake kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30,2021 bungeni.

"Mashirika 14 ya kibiashara yalipata hasara mfululizo, hali hiyo ilisababishwa na hasara kwenye uwekezaji uliofanywa, ufanisi duni wa mashirika husika, na udhibiti hafifu wa mapato na matumizi.

CAG amesema, Kampuni ya Biotech Production kwa mwaka 2020-2021 imepata hasara ya sh.milioni 14,779.56 na mwaka 2019-2020 ilipata hasara ya sh.milioni 15,073.79.

Ameyataja makampuni mengine yaliyojiendesha kwa hasara ni Kampuni ya Mkulazi,Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL),Kiwanda cha Kimataifa cha bidhaa za ngozi Kilimanjaro (KILC),Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), EPZA.

Pia amesema, Kampuni ya Kuzalisha nguo za Umeme za Zege Tanzania (TCPM),Shirika la Posta Tanzania (TPC),Watumishi Housing,Kampuni ya T-PESA kampuni tanzu ya TTCL,Kampuni ya uwekezaji ya PPF,DCC,Kampuni ya uchapishaji ya Chuo Kikuu Dar es salaam (DUP) na Kampuni ya Umeme ya Kikuletwa.

"Mashirika hayo ni ATCL, Mkulazi, TTCL, Kituo cha Mikutano Arusha, EPZA, Watumishi Housing na Kampuni ya Uchapishaji ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

"Naomba nifafanue kuhusu mwenendo Kampuni ya Ndege Tanzania, mwenendo wake umeimarika ukilinganisha na mwaka uliopita kwa sababu kwa mwaka 2020/21, kampuni iliongeza mapato kwa asilimia 11 na kupunguza matumizi kwa asilimia tatu.

"Hivyo, kampuni ilipunguza hasara ya jumla kutoka sh.bilioni 60.25 mwaka 2019/20 hadi kufikia sh.bilioni 36.18 mwaka 2020/21,"amesema.

CAG Kichere amesema hali hiyo ilisababishwa na hasara kwenye uwekezaji uliofanywa, ufanisi duni wa mashirika husika, na udhibiti hafifu wa mapato na matumizi.

Akitoa taarifa ya ripoti hiyo mbele ya waandishi wa habari, CAG Charles Kichere amebainisha kuwa, alipopita katika taarifa za fedha za NHIF, amebaini kuwa wanaume wamepewa huduma ya kujifungua kwenye vituo vya afya.

Ameyataja mapungufu ya udhibiti kwenye mfumo wa madai wa Mfuko wa Bima ya Afya ikiwemo madai 56 yanayoonesha wanaume walipata huduma ya upasuaji (C/S) au huduma za kawaida za kujifungua wakati huduma hizo hutolewa kwa wanawake.

Pia wanachama 444 waliopata huduma ya kuchunguzwa picha kamili ya damu (full blood picture) zaidi ya mara moja kwa siku moja (hadi mara 30) kwenye kituo kimoja.

"Aidha, kuwapo kwa malipo ya madai yaliyorudiwa, pamoja na madai yanayoonesha wanachama wa NHIF waliopokea miwani ya kusomea zaidi ya mara moja wakati utaratibu unaruhusu kutoa miwani mara moja kwa mwaka.

"Udhaifu huu umesababishwa na kukosekana kwa udhibiti katika mfumo wa madai iliyosababisha hasara ya sh. milioni 14.41 kwa mfuko.

"Ninapendekeza kwamba Mfuko wa Bima ya Afya: (a) Kurejesha kiasi kilichopotea kutoka kwa watoa huduma za afya husika; na (b) Kuboresha mfumo wa madai wa CMIS ili kuhakikisha kuwa unasaidia maafisa wanaohusika kuangalia uhalali wa madai yaliyowasilishwa,"amesema.

Aidha CAG amesema kati ya hati 999 zilizotolewa 185 za mamlaka za serikali za mitaa 195 mashirika ya umma na 308 za Serikali Kuu.

CAG Kichere akizungumzia ukaguzi kwa upande wa vyama vya siasa amesema kati vya vyama tisa vilivyokaguliwa vinne vina hati mbaya vikiwamo Chauma na TLP.

Akizungumzia kuhusiana na ukaguzi maalum 56 uliofanyika mwaka 2021 mamlaka ya serikali za mitaa inaongoza kwa kaguzi 37, Serikali Kuu 12 na mashirika ya umma sita.

Amesema, mashirika ya umma 195 yenye hati zinazoridhisha ni 185 zenye shaka nane hati mbaya hakuna na kushindwa kutoa maoni mawili.

Wakati huo huo, kwenye Serikali Kuu amesema, kati ya hati 308 hati zinazoridhisha ni 305 zenye shaka mbili,hati mbaya moja na hakuna ambayo imeshindwa kutoa maoni.

Amesema, halmashauri zilizopata hati zenye mashaka ni ya Wilaya ya Kisarawe,Longido,Mlele,Musoma,Halmashauri ya Sengerema na Bunda.

Kwa upande wa mashirika ya umma ameyataja yenye hati zenye mashaka ni pamoja na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Geita,Taasisi ya Mifupa Muhimbili,Mamlaka ya Bandari Tanzania,Kampuni ya Magazeti ya Tanzania,Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).

Amesema kwa, upande wa Serikali kuu,Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) imepata hati yenye mashaka pamoja na Hesabu Jumuifu za Taifa huku Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT) likipata hati mbaya.

CAG amesema, wakusanya mapato katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 147 hawakuwasilisha benki makusanyo yanayofikia jumla ya shilingi bilioni 17.

Pia,Mawakala wa kukusanya mapato katika Mamkala za Serikali za Mitaa 12 hawakupeleka benki makusanyo ya shilingi bilioni 3.31 kinyume na mikataba yao.

“Ninapendekeza kwamba TAMISEMI iongeze usimamizi wa mapato na kuhakikisha makusanyo yanapelekwa benki bila kuchelewa,”amesema.

Vilevile,amesema Mamlaka ya Serikali za Mitaa 24 zilitumia sh.milioni 664 katika matumizi yasiyo na manufaa kama vile malipo kwa riba na adhabu za kuchelewesha malipo na posho kwa watumishi wasiostahili.

Aidha,Mamkala za Serikali za Mitaa 61 ziliagiza na kulipa sh bilioni 8.44 kwa ajili ya bidhaa ambazo hazikuwasilishwa  na wazabuni kwa muda wa hadi kufikia miezi 24.

Walimu

Amesema,katika ukaguzi wake, tathmini ya uwiano wa walimu na wanafunzi katika mamlaka 48 za serikali za mitaa na ilibainisha kuwa kati ya walimu 40,458 wanaohitajika kwa shule za msingi walikuwepo walimu 23,881 tu ikimaanisha upungufu wa walimu 16,571 sawa na asilimia 41.

“Hali hii inadidimiza juhudi za Serikali katika kuboresha elimu ya msingi na sekondari,”amesema Kichere.

Pia amesema,alifanya kaguzi maalumu 37 katika halmashauri 36 na kubaini jumla ya sh.bilioni 19.72 zilikusanywa kutoka vyanzo mbalimbali lakini hazikupelekwa benki; kati ya hizo, kiasi cha Sh. bilioni 10.13 (asilimia 51) zinahusiana na iliyokuwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.

Amefafanua kuwa, kati ya sh.bilioni 10.13, Sh. bilioni 4.64 hazikupelekwa benki na mawakala 20 wakati kiasi cha Sh. bilioni 5.49 hakikupelekwa benki na watumishi 19 waliokuwa wakikusanya mapato.

“Ninapendekeza Serikali ichukue hatua stahiki kwa watumishi na mawakala waliosababisha hasara hiyo na kuhakikisha kiasi hicho kinarejeshwa,”amesema.

Usimamizi

Wakati huo huo, CAG amesema mamlaka za serikali za mitaa 25 zililipa sh.milioni 556.84 kwa watumishi waliostaafu, waliofariki, waliotoroka, walioachishwa kazi na watumishi waliokuwa likizo bila malipo.

CAG Kichere amebainisha kuwa, Mamlaka za Serikali za Mitaa tano zilitozwa Sh. bilioni 180.70 kama adhabu kwa kushindwa kuwasilisha makato ya watumishi kama michango kwenye Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ya Watumishi wa Umma, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Kodi ya Mapato na Bima ya Afya.

Amefafanua kuwa, ulipaji wa mishahara kwa watumishi wasiostahili husababisha upotevu wa fedha za Umma.

Pia, amesema kutopeleka makato ya kisheria ya watumishi kwa wakati huvutia tozo ambayo ni malipo yasiyo na manufaa.

“Ninapendekeza OR-TAMISEMI izisimamie mamlaka za serikali za mitaa kuepuka kulipa malipo ya mishahara yasiyokuwa na manufaa pia iwasiliane na hazina ili kupeleka michango ya kisheria kwa wakati kwenye Mifuko ya Pensheni na kuepusha tozo zisizo za lazima na kuhakikisha malipo ya mishahara ya wafanyakazi kwa watumishi wanaostahili,”amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news