CWT Musoma yashtushwa na kifo cha Mwalimu Mkuu, mwili wake ulikutwa Butiama

*Waiomba Polisi kufanya uchunguzi wa kina

NA FRESHA KINASA

CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) Manispaa ya Musoma kimeliomba Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara kufanya uchunguzi wa kina kufuatia kifo cha aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Rwamulimi' A', Isaiah Ombori.
Mwalimu Ombori (pichani), hakuonekana nyumbani kwake toka Jumapili ya Machi 28,2022 ambapo Aprili Mosi, 2022taarifa zilitolewa na wananchi wa eneo la Kirumi Wilaya ya Butiama wakisema kuna maiti imeonekana eneo hilo na vitambulisho vyake vina jina la mwalimu Isaiah Ombori.

Mwakilishi wa CWT Manispaa ya Musoma, Mwalimu Kunyara Edward akizungumza Aprili 4, 2022 wakati wa utoaji wa salamu za chama hicho nyumbani kwa marehemu Mtaa wa Songe kwa ajili ya kusafirishwa kwenda kuzikwa Kijiji cha Mika Kata ya Bukwe Wilaya ya Rorya Aprili 5, 2022, Kunyara amesema kuwa, Jeshi la Polisi lina wajibu wa kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini waliohusika wafikishwe katika vyombo vya sheria.

Amesema kuwa, Mkoa wa Mara ni eneo salama kwa wafanyakazi na watumishi wote kufanya kazi, hivyo watu wachache wenye nia mbaya na wanaoharibu taswira ya mkoa huo kwa kufanya matukio ya mauaji na vitendo vingine viovu wasiachwe bila kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

"Polisi wafanye uchunguzi wa kina, kitendo hiki cha Mwalimu kukatishwa uhai wake hakitakiwi kufumbiwa macho hata kidogo. Tukio hili linasikitisha sana kwa hiyo matumaini yetu ni kuona kwamba waliofanya kitendo cha mauaji ya Mwalimu huyu wanawajibishwa,"amesema Mwalimu Kunyara.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, Deus Nyakiriga amesema kuwa, Mwalimu Isaya alifanya kazi kwa weledi, bidii na kujituma kwa dhati katika kuhakikisha anatimiza vyema wajibu wake. Hivyo kitendo cha kukatishwa uhai wake ni kosa kubwa na vyombo vya dola vina wajibu wa kuhakikisha wahusika wanatiwa nguvuni.

"Tunashindwa hata kuongea juu ya tukio hili, Isaya alikuwa mtumishi wetu mwaminifu na mchapakazi, Alikuwa ni mtumishi anayestahili kuishi mpaka pale Mungu angemchukua mwenyewe. Tulipata taarifa zake amepotea tukiwa katika kikao. taarifa zilitolewa polisi na tulipata ushirikiano, ofisi ya mkurugenzi kwa kushirikiana na Polisi waliendelea kushirikiana kumtafuta hadi siku ya tarehe moja mwezi wa nne,2022 tulipopata taarifa kuwa ametambulika kuwa ni Mwalimu Isaya ambaye amekufa eneo la Kirumi na ndipo tulipokwenda na kukuta ndiye,"amesema Deus.

"Inasikitisha sana, ni binadamu ambaye alistahili heshima. Hakufa katika mazingira mazuri. Tunaamini Jeshi la Polisi litafanya kazi juu ya tukio hili,"amesema.

Nicksoni Mwandala ni Diwani wa Kata ya Bweri Manispaa ya Musoma ameieleza DIRAMAKINI BLOG kuwa, Mwalimu Isaiah alikuwa na ushirikiano mzuri na wananchi katika masuala ya kijamii na maendeleo hivyo kuondoka kwake ni pengo kubwa kwa wakazi wa mtaa wa Songe na jamii.

Mwalimu Isaiah Ombori alizaliwa mwaka 1986 na amehitimu Shahada ya Ualimu katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na aliajiriwa mwaka 2011 Manispaa ya Musoma, ambapo alifundisha katika shule za Sekondari Iringo na Nyabisare zilizopo katika manispaa hiyo.

Mwaka 2019, alihamishiwa elimu msingi na kupangiwa Shule ya Msingi Songambele na baadaye Rwamulimi 'A' ambapo mpaka mauti yanamkuta alikuwa Mwalimu mkuu katika shule hiyo na ameacha mke mmoja na watoto watano.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news