Elimu, Afya zapewa kipaumbele ajira mpya nchini

NA DIRAMAKINI

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Jenista Mhagama amesema ajira mpya 32,604 zinazotarajiwa kutangazwa kabla ya kufikia mwisho wa mwaka huu wa fedha, zitaigharimu serikali shilingi bilioni 315 kwa mwaka.
Mheshimiwa Mhagama ametoa kauli hiyo leo Aprili 12, 2022 jijini Dodoma wakati akizungumza kuhusu utoaji wa vibali vya ajira kwa watumishi wa umma nchini mbele ya waandishi wa habari.

Amesema, kati ya ajira hizo 32,604, sekta zilizopewa kipaumbele ni Elimu iliyopewa nafasi12,035, Afya 10,285 na sekta zingine nafasi 2,392.

Mheshimiwa Mhagama amesema, katika nafasi 12,035 za sekta ya elimu, nafasi 9,800 ni kwa wa walimu wa shule za msingi na sekondari, ambapo mchakato wake utasimamiwa na OR-TAMISEMI,huku nafasi 2,235 ni kwa ajili ya wahadhiri wa vyuo vikuu, vyuo vya elimu ya juu na wakufunzi wa vyuo vilivyopo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ambapo mchakato utasimamiwa na taasisi husika kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

Kwa upande wa Sekta ya Afya, Mheshimiwa Mhagama amesema imekasimiwa nafasi za ajira 10,285 zinazojumuisha nafasi 7,612 kwa ajili ya hospitali, vituo vya afya na zahanati zilizopo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, ambapo mchakato utasimamiwa na OR-TAMISEMI.

"Mchakato wa ajira hizi utasimamiwa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI ambapo nafasi 2, 235 kwa ajili ya Wahadhiri wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Elimu ya Juu pamoja Wakufunzi wa Vyuo vilivyopo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,mchakato wa ajira hizi utasimamiwa na Taasisi husika za elimu kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma,"amesema.

Pia amesema, nafasi 1,650 kwa ajili ya watumishi wa kada za afya katika Hospitali za Kanda, Hospitali za Rufaa za Mikoa ambapo mchakato wake utasimamiwa na Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Mhagama amezitaja nafasi 1,023 kwa ajili ya vyuo vya afya, hospitali nyingine za kimkakati na zile za Mashirika ya Dini na hiari zenye mkataba na serikali.

Amefafanua nafasi 2,392 zinazotarajiwa kujazwa kwenye sekta zingine za kipaumbele kuwa katika kada za kilimo nafasi za ajira ni 814, kada za mifugo nafasi 700, kada za uvuvi nafasi 204, kada za maji nafasi 261 na kada za sheria nafasi 513.

Mheshimiwa Mhagama amesema, mchakato wa ajira hizo utasimamiwa na wizara husika pamoja na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

Ameongeza kuwa, zipo nafasi 7,792 kwa ajili ya watumishi wa kada nyingine kwenye wizara, idara zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa na taasisi nyingine za umma nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news