🔴LIVE:Uzinduzi wa Filamu ya Utalii Tanzania (The Royal Tour)

NA GODFREY NNKO

HIKI ni kipindi cha runinga ambacho kimerekodiwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kati ya Agosti 2021 na Septemba 2021, ambacho kinazinduliwa rasmi leo jijini New York na Aprili 21, 2022 itakuwa huko Los Angeles nchini Marekani ikiwa ni njia moja wapo ya kuliteka soko kubwa la utalii duniani.
Soko la Marekani, kupitia kipindi hiki linatarajiwa kuyafikia kwa haraka masoko ya Ujerumani, Italia, Uingereza, Ufaransa, Hispania, Uholanzi, Australia, Canada na mengineo.

Baada ya hapo uzinduzi utafanyika jijini Dar es Salaam Aprili 28,2022 na Zanzibar mwezi Mei 7,2022 baada ya hapo filamu hii ambayo inaongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan itaanza kuoneshwa duniani kote.

Mfululizo huu muhimu wa vipindi maalum vya runinga, vilivyotayarishwa na kuratibiwa na mwandishi wa habari wa Kimataifa aliyeshinda Tuzo ya Emmy, Bw. Peter Greenberg,vitaionesha Dunia vivutio vya asili vilivyopo hapa Tanzania kwa njia ambayo hakuna mgeni amewahi kuviona hapo awali.

Emmy ni miongoni mwa tuzo kubwa duniani ambayo inashabihiana kwa karibu na tuzo ya Oscar. Tofauti kuu kati ya Oscar na Emmy ni kwamba tuzo za Oscar hutolewa kila mwaka kwa ubora katika tasnia ya filamu, wakati Emmy hutolewa kwa utendaji mzuri katika tasnia za televisheni mwaka mzima. Jambo kuu ni kwamba, tuzo zote mbili hutolewa kwa maonesho bora katika sinema na runinga.

Uzinduzi huu wa Tanzania The Royal Tour una faida nyingi ikiwemo kukuza utalii kwa kutangaza nchi Kimataifa, kuongeza pato la Taifa, hivyo kuimarisha uchumi.

Faida nyingine ni kuongeza fursa za ajira kwenye Sekta ya Utalii na sekta mbalimbali za uwekezaji, ulinzi wa rasilimali zetu, kubadilisha mtazamo wa baadhi ya alama za kihistoria za Tanzania, kukuza na kuenzi utamaduni wetu, hizo ni kwa uchache. 

Tanzania ikiwa na vivutio vingi vya utalii kwa uchache ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti,Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro na visiwa vya karafuu na marashi Zanzibar, kupitia filamu hii inatarajiwa kuleta matokeo makubwa katika sekta ya utalii na uwekezaji.

Mheshimiwa Rais Samia akiwa amevalia vazi la safari na Hijab,kupitia filamu hii anatumia hekima na maarifa ya kipekee kuwapeleka watazamaji katika safari ya kuvutia kuona baadhi ya vivutio vya kipekee vya utalii wa asili vya Tanzania.

Aidha, kipindi cha Royal Tour ni sehemu ya mpango kabambe wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuongeza idadi ya watalii wanaofika kutoka milioni 1.5 kwa mwaka hadi milioni tano kama ilivyoainishwa katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano wa nchi, ambao pia ni mwongozo wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 hadi 2025.

Kila mmoja anatambua nguvu ya Sekta ya Utalii nchini, kwani,ina uwezo wa kuongeza nafasi za ajira, na hivyo kuinua uwezekano wa sekta hiyo wa kuongeza nafasi za ajira hadi wastani wa ajira milioni 1.8 hadi milioni mbili kutoka milioni 1.3 za sasa hadi milioni 1.5.

Hivyo,utalii unatarajiwa kuchangia pato la taifa kutoka asilimia 17 ya sasa hadi asilimia 25 katika miaka michache ijayo.

Onesho la kwanza la kipindi hiki duniani pia linatarajiwa kuionesha Tanzania zaidi ya utalii kwa kuangazia sekta zingine ambazo ni muhimu katika kuwavutia wawekezaji kutoka kila kona ya Dunia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news