Maagizo mapya ya Waziri Bashungwa yazigusa halmashauri,makatibu tawala wote

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Innocent Bashungwa ameziagiza halmashauri zote nchini katika mwaka wa fedha 2022/2023 kuhakikisha zinatenga bajeti ya maeneo ya kujenga Vituo vya Walimu (Teachers’ Resource Centres- TRCs) ambavyo ni mahususi kwa ajili ya kufanikisha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Hayo ameyasema leo Aprili 25, 2022 katika Shule ya Sekondari ya Benjamin William Mkapa iliyopo Ilala jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuzindua usambazaji wa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa ajili ya vituo vya TRCs 150 vilivyopo katika halmashauri 144 za mikoa 26 ya Tanzania Bara.

Mheshimiwa Bashungwa amesema,vituo hivyo ni muhimu katika kipindi hiki ambacho Dunia inapitia katika mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia.

"Sasa tumeamua kuvifufua vituo hivyo na tayari halmashauri 144 zimeanza kutekeleza Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA). Walimu 12,544 tayari wameshapatiwa mafunzo, na lengo ni kuwafikia walimu 30,957 katika mwaka huu wa fedha,nilipewa maelekezo na Mheshimiwa Rais kwamba anataka kuona Ofisi ya Rais-TAMISEMI inaviimarisha vituo hivi ili viweze kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa. "Malengo haya ni kusaidia walimu kubadilishana uzoefu, hali kadhalika wataalamu wabobezi kupeana mbinu za ufundishaji wakiwa na walimu,"amesema Mheshimwa Bashungwa.

Pia Mheshimiwa Waziri Bashungwa amewaagiza Makatibu Tawala wa Mikoa nchini kuhakikisha vifaa vya TEHAMA ambavyo vimetolewa na Serikali vinafika katika vituo kwa kuzingatia mgao uliotolewa na OR-TAMISEMI.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri Bashungwa ameishukuru Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambayo ndio wizara ya mama katika utoaji wa elimu nchini.

"Na tumekuwa tukishirikiana katika kutekeleza majukumu mbalimbali. Aidha, ninaishukuru Taasisi ya Global Partnership for Education (GPE) kwa kuunga mkono juhudi za Rais, ninamuahidi Mheshimiwa Rais Samia na Watanzania kuwa, tutaendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi, ubunifu, uaminifu na utiifu kwake, na kwa nchi yetu, katika kumsaidia kusimamia shughuli za elimu katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

"Naomba nichukue fursa hii kuwaelekeza Makatibu Tawala wa Mikoa Kuhakikisha vifaa vinafika katika vituo kwa kuzingatia mgao uliotolewa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI na ninawaelekeza Makatibu Tawala wa Mikoa kusimamia kwa karibu ufundishaji na ujifunzaji ili matokeo ya Mitihani ya Taifa na Ubora wa Elimu viendane na kiwango kikubwa cha uwekezaji unayofanywa na Serikali.

"Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea na juhudi za kuboresha utoaji wa elimu nchini. Hii ni katika utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka, 2014 ambayo pamoja na mambo mengine, imeweka malengo ya kuwa na idadi ya kutosha ya wananchi walioelimika katika Sayansi

"Ninamshukuru Rais kwa kututengea shilingi bilioni 55.57 katika bajeti ya mwaka 2022/23 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 809 za walimu zenye uwezo wa kuchukua kaya 1,916. Kati yake, nyumba za walimu wa shule za msingi ni 298 za (tatu kwa moja-3 in 1) ambazo zitajengwa,"amesisitiza Mheshimiwa Waziri Bashungwa.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Waziri Bashungwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwapa heshima kubwa walimu na sekta ya elimu nchini.

"Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia kwa kuwapandisha madaraja walimu 126,346 ambao walikaa muda mrefu bila kupandishwa madaraja ambayo ni haki yao ya msingi.

"Naomba niwatake walimu kutambua kuwa pamoja na kupandishwa madaraja, Serikali inategemea walimu kuendelea kujituma, Mheshimiwa Rais Samia toka ameingia madarakani ameshatoa ajira za walimu 6,949 wa shule za msingi na sekondari, na wiki iliyopita ametupatia kibali cha kuajiri walimu 9,800 kwa maana ya walimu 4,800 wa shule za sekondari na walimu 5,000 wa shule za msingi. Hivyo kufanya jumla ya walimu 16,749
"Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuonyesha upendo wake wa dhati kwa wanafunzi na walimu nchini. Pamoja na kwamba leo tumekutana kwa ajili ya uzinduzi wa usambazaji wa vifaa hivi, Mheshimiwa Rais amefanya pia mambo makubwa sana katika sekta ya elimu.

"Uwekezaji huu utawezesha walimu wote sasa kupata fursa ya kushiriki kikamilifu katika Mafunzo ya Walimu Kazini, kwa kutumia vituo hivi ukilinganisha na awali, ambapo walimu waliokuwa wanateuliwa kwa ajili ya kupewa mafunzo walikuwa wachache.

"Tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu kwa kuendelea kutafuta na kutoa fedha kwa ajili ya uimarisha wa elimu nchini. Fedha hizi zote amezielekeza kwa walimu kuhakikisha wanakuwa na mazingira bora ya kujiendeleza kitaaluma na kitaalamu,"amesema Mheshimiwa Bashungwa.

Katika hafla hiyo, Mheshimiwa Waziri Bashungwa amesema, vifaa ambavyo vimetolewa ni mashine za kudurufu 150, kompyuta za mezani 600,printa 150 na projekta 150. "Na vifaa hivi vimegharimu jumla ya shilingi bilioni 2.5,"amesema Mheshimiwa Waziri Bashungwa.

Pia Mheshimiwa Bashungwa amesema, ataendelea kushirikiana na Tume ya Utumishi wa Walimu, Chama cha Walimu Tanzania kuhakikisha wanaendelea kuyasimamia kikamilifu maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuboresha miundombinu ya walimu, maslahi na kupandishwa madaraja.
 
Naye Naibu Katibu Mkuu wa OR-TAMISEMI katika Sekta ya Elimu, Gerald Mweli, alisema serikali imeamua kufufua vituo vya kujifunzia walimu kwa kutoa mashine hizo za kisasa za TEHAMA.

Amewataka walimu wote wanaolengwa kufikiwa na huduma hiyo ili nao watoe elimu inayoendana na viwango vya kimataifa.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Hassan Rugwa amesema Mkoa wa Dar es Salaam, unatarajia kujenga shule ya kisasa ya sekondari ya wanafunzi mchanganyiko, kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita itakayokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 4,000.

Rugwa amesema, shule hiyo itakuwa ya bweni na inatarajia kujengwa katika mwaka mpya wa fedha wa 2022/23 na itakamilika mwisho mwa mwaka huu.

"Nikudokeze Waziri Bashungwa unaweza kuona shule hii ya Benjamin Mkapa ni kubwa sana kwa mkoa wetu kwa sababu inachukua wanafunzi zaidi ya 1,700, lakini tuna mpango wa kujenga shule bora ya kisasa ya mkoa itakayochukua wanafunzi wengi zaidi na ujenzi utaanza muda wowote kuanzia sasa,” amesema Rugwa.
 
Wizara ya Elimu

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo amesema kuwa, baada ya walimu kupata ujuzi kupitia vituo hivyo, wanatarajia kuona mabadiliko makubwa katika matokeo ya elimu.

"Hivi vifaa mvitunze, viweze kudumu muda mrefu ili kuwawezesha kupata ujuzi ambao utakuwa na manufaa kwa wadau wetu ambao ni wanafunzi.

"Ninapenda kuwahakikishia kwamba, wizara yetu inaendelea kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI bega kwa bega, kwa kila hatua, kwani tunajiita sisi ni wizara pacha, kwa kile ambacho kinatokea Wizara ya TAMISEMI ndicho hicho hicho ambacho Wizara ya Elimu inakisimamia kuhakikisha ubora wa elimu unaimarika,"amesema.

Shukurani

Kwa upande wake Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro, Germana Mungalo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Maafisa Elimu Mikoa ya Tanzania akitoa neno la shukurani kwa niaba ya wenzake,amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri Bashungwa kwa namna ambavyo wameonesha juhudi kubwa za kuhakikisha miundombinu ya elimu na walimu inaendelea kupewa uzito mkubwa.

Amesema, yeye na wenzake wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanatafanya kazi kwa bidii ili kuwezesha matokeo bora katika sekta hiyo hapa nchini.

"Miundombinu imeboreshwa sana, madarasa ya UVIKO-19 yanang'aa Tanzania nzima, nani kama Mama? ..Na kweli hakuna kama Rais wetu wa Awamu ya Sita Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

"Sisi tunakuahidi, hivi vifaa mabavyo umetupa maelekezo kwamba tuhakikishe vinafika katika sehemu ambazo zinatakiwa, vituo vile 150 ambavyo vinapelekwa hivi vifaa katika awamu ya kwanza,tunaahidi tutavifikisha, tutavitunza, tutahakikisha vinatumika kwa manufaa ya walimu wetu waliopo shuleni ili waweze kuvitumia katika mafunzo ambavyo wakati mwingine huwa tunayaita Jumuiya za Ujifunzishaji kwa Walimu, lakini pia vitatumika kwa mafunzo mengine mbalimbali, hatuwezi kuwazuia wenzetu wa kilimo wakitaka kuja kujifunza.
"Tunaenda kuvitunza ili kuhakikisha kwamba vinatumika muda mrefu, na vinatumika kwa makusudi yaliyokusudiwa, nimeshukuru sana kwa sababu umetuhakikishia kwamba katika bajeti ijayo zitengwe fedha zile halmashauri ambazo hazikupata mgao katika awamu ya kwanza, kutokana na mapungufu ambayo yalikuwepo katika vituo vinafikiwa, tunashukuru sana Mheshimiwa Waziri,"amesema Bi.Mungalo.

Amesema, walimu wanaendelea na mafunzo na huko walipo wameonesha uchang'amfu kwa kuwa wamepewa nafasi ya kupata maarifa mapya kupitia vituo hivyo.

Post a Comment

0 Comments