Maji safi na salama yawafikia wanakijiji cha Tulieni mkoani Lindi, Wamshukuru Rais Samia

NA DIRAMAKINI

WANANCHI wa kijiji cha Tulieni kata ya Londo, wilayani Lindi mkoani Lindi, wamesema watamchagua Rais Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi mkuu wa 2025, kama shukrani yao yakupatiwa maji ya bomba kijijini hapo baada ya miaka 30 kupita.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lindi, Mhandisi Iddi Pazi akipanda ngazi kukagua ujenzi wa Mradi wa Maji Tulieni kata ya Londo.

Mradi huo wa Maji Tulieni unatekelezwa kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19, kwa fedha za mkopo usio na riba Sh.trilioni 1.3 za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ambapo zaidi ya Sh.milioni 421 zimetumika kutekeleza mradi huo.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hii, baadhi ya wananchi watakaonufaika na maji hayo wamesema uamuzi wa Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), kuwapatia maji ni wa kuungwa mkono na kupongezwa.

Kaimu Mwenyekiti wa kijiji cha Tulieni Asha Nalika amesema kwa zaidi ya miaka 30 wamekuwa wakitumia maji ya visima ambayo sio safi na salama

Nalika amesema walikuwa wanatumia muda mrefu kufuata maji hali ambayo ilikuwa inakwamisha shughuli za maendeleo, hivyo ujio wa maji hayo watakuwa wamekomboka.

“Niseme kweli maji haya yametoa uhakika kwa wananchi wa kijiji cha Tulieni kumpa kura za ndio Rais Samia Suluhu Hassan, kwani alichofanya hakina kifani,” amesema.

Mwanakijiji Zeinab Ndembo amesema kukamilika kwa mradi huo, kutawaondolea adha ya kutumia muda mwingi kufuata maji.

Amesema wamekuwa wakipanda vilima na mabonde kufuata maji, hivyo ni imani yake kuwa kwa sasa watachota maji safi na salama katika maeneo ya karibu.

“Maji masafi na salama yalikuwa ni mpaka mvua zinyeshe, sasa tunaamni kuwa kuanzia mwezi ujao tutakunywa maji safi na salama mwaka mzima,” amesema.

Naye Fundi wa mradi huo, Elisha Kaumbi amesema mradi huo umekuwa neema kwake kwa kuwa ameweza kuhudumia familia yake bila hofu yoyote.

“Mimi nimetoka Mwanza hadi huku Lindi kufuata kazi, hivyo namshukuru Rais Samia kuiwezesha RUWASA tukapata ajira hii, kwani tunahudumia familia zetu vizuri, tunaomba miradi mingine iendelea,” amesema.

Fundi Hamisi Chamchuzi amesema miradi hiyo imechochea shughuli za kiuchumi na mzunguko wa fedha, hivyo mumuomba Rais Samia kuendelea kutoa fedha za miradi mingine.

Kwa upande wake Fundi Hassan Chinganalile amesema kupitia miradi hiyo wananchi watanufaika kwa kupata maji safi na salama, ila na vijana wanapata kazi.

Mkandarasi anayetekeleza mradi huo kwa niaba ya RUWASA, Mhandisi Shaibu Mushi amesema wamejipanga kutekeleza mradi kwa wakati ambapo hadi sasa ameshafikia asilimia 60 ya ujenzi.

Mushi amesema kazi ambazo anapaswa kufanya ni kujenga tenki lenye uwezo wa kuweka lita 100,000, kuchima mtarao na kusambaza bomba, kujenga vituo vya kuchotea maji.

Akizungumzia miradi hiyo ya ustawi katika majimbo mawili ya Mtama na Mchinga mkoani Lindi, Meneja wa RUWASA Mhandisi Iddi Pazi, amesema ujenzi wa miradi hiyo umefikia asilimia 59 kwa ujumla.

“Miradi hii miwili Moka Mchinga na Tulieni Mtama inatekelezwa kwa fedha za ustawi ambapo zaidi ya Sh.milioni 800 zitatumika. Tulioeni Sh.milioni 421 na Moka Sh.milioni 437,” amesema.

Mhandisi Pazi amesema takribani watu 2,000 watanufaika na maji ambayo yatatoka katika miradi hiyo miwili ya Moka na Tulieni, hivyo kuwataka wanakijiji kuitunza ili iwe endelevu.

Meneja huyo amesema Lindi inapata maji kwa asilimia 73, huku wakiendelea kutekeleza miradi mingine sita ambayo ni Mnyangala, Milola, Navaunga, Nyangao Mtama, Kiwawa na Mputwa, ili mwishoni mwa 2023 maji yapatikane kwa asilimia 80 na lengo la 2025 lakupatikana maji asilimia 85 kwa Lindi litafikiwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news