Mweka Hazina CWT Taifa awapiga jeki walimu Sekondari ya Nyumbu, atoa motisha ya fedha kwa kufaulisha vizuri

NA ROTARY HAULE

MWEKA HAZINA wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Abubakar Allawi ametoa msaada wa viti 30 katika Shule ya Sekondari Nyumbu iliyopo Kibaha mkoani Pwani ikiwa ni sehemu ya kupunguza changamoto ya ukosefu wa viti vya kukalia kwa walimu wa shule hiyo.
Aidha,mbali na msaada huo lakini Allawi ameahidi kuwachangia walimu wa shule kiasi cha sh.milioni moja kwa ajili ya kutoa motisha kwa walimu hao kutokana na shule yao kufaulisha kwa kiwango cha juu matokeo ya kidato cha Kwanza ya mwaka 2021.

Allawi,ametoa msaada huo shuleni hapo mbele ya viongozi mbalimbali wa CWT ngazi ya Wilaya na Mkoa,Mkuu wa Shule hiyo,diwani wa Kata ya Mkuza, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi pamoja na walimu.

Akiwa shuleni hapo Allawi amesema kuwa, mapema mwaka huu alipokea barua kutoka kwa Mkuu wa Shule ya Nyumbu, Abubakar Ombeni juu ya changamoto ya ukosefu wa viti vya kukalia walimu shuleni hapo.
Amesema,baada ya kupokea barua hiyo alilazimika kuona namna ya kusaidia walimu hao ambapo amesema kwa hatua ya awali ameona ni vyema akaanza kusaidia viti 30 na kisha ataendelea kuchangia kulingana na mahitaji ya shule hiyo.

Allawi amesema, Serikali ya Awamu ya Sita inafanya kazi nzuri katika kuboresha miundombinu ya elimu na kwamba changamoto nyingine ndogondogo zinazowagusa walimu lazima CWT izifanyie kazi.

"Kazi ya kuboresha miundombinu hususani ya kujenga madarasa,majengo ya utawala ni ya Serikali, lakini sisi Chama Cha Walimu tunawajibika kusaidia changamoto zinazowagusa moja kwa moja walimu kama hivi Viti tunavyochangia leo,"amesema Allawi.
Katika hatua nyingine Allawi amewapongeza walimu hao kwa kufanya kazi kubwa na nzuri ya kufaulisha wanafunzi wa kidato cha nne mwaka 2021 kwa asilimia 99.46 na kuwataka waendelee na kuongeza jitihada zaidi.

"Nichukue fursa hii kuwapongeza walimu wa Sekondari Nyumbu kwa kazi nzuri na mtambue kuwa kazi ya walimu ni kufundisha lakini kazi ya kudai haki ibaki kwa CWT kwakuwa ndio kazi ya chama kutetea wanachama wake,"amesema Mwalimu Allawi.

"Wakati nafika hapa nilijua nakuja kutatua changamoto ya viti, lakini nimekutana na changamoto nyingine ya kuwapongeza walimu kwa kazi nzuri ya kufaulisha kwa hiyo na mimi nitachangia shilingi milioni moja kwa ajili ya kuwapongeza walimu wa shule hii na motisha hivi zinawafanya walimu kuongeza juhudi ya kufundisha,"amesema Allawi.

Allawi ameiomba Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya walimu kwani asilimia 20 ya walimu hawana sehemu ya kukaa ambapo kwa kuboresha mazingira hayo yataongeza morali ya ufundishaji.

Mkuu wa Shule hiyo, Abubakar Ombeni, amemshukuru Mwalimu Allawi pamoja na CWT kwa ujumla kwa jinsi ambavyo wamejitoa kupunguza changamoto ya viti vya kukalia kwa walimu hao.

Ombeni amesema kuwa, shule yake ina jumla ya walimu 130 na kwamba hiyo ni shule yenye walimu wengi Mkoa wa Pwani huku ikiwa na wanafunzi wa 1,886 wa kidato cha kwanza na kidato cha nne.
Amesema,mwaka 2021 ufaulu ulikuwa ni asilimia 99.46 ikiwa Shule ya tano Kimkoa na Shule ya nne kwa Halmashauri ya Kibaha Mjini na kwamba mafanikio hayo yanatokana na juhudi za walimu baada ya kulipwa maslahi yao na kupandishwa vyeo walimu 82.

Katibu wa CWT Mkoa wa Pwani Mwajuma Mgonze,amesema kuwa walimu ndio daraja kubwa la Taifa na kwamba CWT inatambua juhudi zao huku akimshukuru Mwalimu Allawi kwa jinsi anavyojitoa kusaidia wanachama wake.
Mgonze amesema, CWT inatambua changamoto ni nyingi, lakini walimu wasikatishwe tamaa kwakuwa CWT ipo na Kila siku inashughulikia malalamiko yao na kwamba wajitahidi kusaidia kuboresha chama kwa kukosoa na kushauri.

Hata hivyo,Diwani wa Kata ya Mkuza, Focus Bundala, amemshukuru Mwalimu Allawi kwa namna alivyojitoa huku alimuomba aendelee kusaidia na changamoto nyingine za Shule hiyo pale watakapomuomba.

Post a Comment

0 Comments