NHC kutekeleza vipaumbele 11 vinavyohakisi mwelekeo mpya

*Kipaumbele cha tatu ni kujenga nyumba za kuuza na kupangisha katika maeneo mbalimbali ya mikoa kwa kutumia ardhi itakayopatikana au kwa kutumia ardhi nafuu

NA GODFREY NNKO

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limeainisha vipaumbele 11 ambavyo wanatarajia kuvitekeleza ili kuongeza ufanisi katika miradi mbalimbali na kukuza mapato yatakayosaidia kutoa huduma bora kwa Watanzania.

Vipaumbele hivyo ni sehemu ya mikakati inayohakisi mwelekeo mpya wa uongozi wa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Bw.Nehemiah Kyando Mchechu ambaye aliteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Hayo yamesemwa leo Aprili 4,2022 na Meneja Habari na Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa, Bw.Muungano Saguya wakati akitoa taarifa ya mwelekeo mpya wa shirika kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Bw.Saguya amesema kuwa, miongoni mwa vipaumbele hivyo ni pamoja na kukamilisha miradi mikubwa iliyosimama ya Morocco Square na Kawe 711 jijini Dar es Salaam.

Miradi hiyo ilisimama tangu mwaka 2018 kutokana na upungufu wa fedha. "Shirika limepewa kibali cha awali na Serikali ya Awamu ya Sita cha kukopa shilingi billioni 173.9 ili kumalizia miradi hiyo.

"Na tayari Hazina imeshaidhinisha mkopo wa shilingi billioni 44.7 na tayari utekelezaji wa miradi hiyo unaendelea,"amefafanua Bw.Saguya.

Katika hatua nyingine, Meneja huyo amesema sambamba na mpango wa awali wa biashara wa eneo la Kawe, pia shirika hilo limeandaa mpango wa kujenga nyumba 360 za makazi ya watu wa kipato cha kati na maduka ya biashara katika eneo hilo.

Kipaumbele cha pili, Bw.Suguya amesema, katika kusaidia suala la makazi na kuunga mkono juhudi kubwa za Serikali za kuhamia jijini Dodoma, wataendelea kujenga nyumba jijini humo.

Amebainisha kwamba, ujenzi utakaofanyika ni pamoja na nyumba za makazi za Medeli Awamu ya III, Iyumbu Awamu ya III za ghorofa na baada ya kupata ardhi ya uendelezaji.

"Pia, tuna kipaumbele cha tatu ambacho ni kuendelea kujenga nyumba za kuuza na kupangisha katika maeneo mbalimbali ya mikoa kwa kutumia ardhi itakayopatikana au kwa kutumia ardhi nafuu,"amesema Bw.Suguya.

Amefafanua kuwa, shirika litaendelea kuimarisha maeneo ya mipaka ya Tanzania kwa kujenga majengo makubwa ya biashara kama ilivyofanyika eneo la Mtukula, ambalo ni mpaka wa Tanzania na Uganda.

Meneja huyo ameongeza kuwa, kipaumbele kingine ni kuendelea kukamilisha majengo nane ya wizara mbalimbali za Serikali katika mji wa Mtumba jijini Dodoma katika awamu ya pili.

Amebainisha kuwa, miradi hiyo itakapokamilika itagharimu jumla ya shilingi bilioni 186.83. "Na msisitizo umewekwa katika kuikamilisha miradi hiyo kwa wakati kwa kuongeza usimamizi na udhibiti ubora wa majengo hayo,"amesema.

Bw.Suguya amesema, kipaumbele cha tano cha shirika hilo ni kukaribisha wawekezaji kutoka sekta binafsi ili kufanya uendelezaji wa majengo ya biashara na makazi.

"Uwekezaji huo utafanyika katika viwanja vya shirika ambavyo vipo wazi kwa sasa, lengo ni kuongeza mapato ya shirika, mapato ya Serikali, kukuza uchumi na ajira kwa Watanzania,"amesema.

Pia amefafanua kuwa, mpango wa kushirikiana na sekta binafsi tayari umeshaandaliwa na utawekwa wazi kwa umma hivi karibuni huku ukizingatia vigezo na masharti yenye tija kwa shirika, wawekezaji na Taifa.

"Kipaumbele cha sita tutaendelea kukusanya madeni ya kodi ya nyumba yanayofikia shilingi bilioni 22 na madeni mbalimbali yatokanayo na uuzaji wa nyumba na viwanja yanayofikia shilingi bilioni 11.1.

"Msisitizo utakuwa kuhakikisha kila anayedaiwa analipa deni lake ili kuliwezesha shirika kuendelea kuwahudumia Watanzania wote kwa kutumia rasilimali hizi za umma,"amefafanua Bw.Suguya.

Ameongeza kuwa, ni jukumu la kila mteja wa shirika anayedaiwa kuhakikisha analipa deni lake kwa wakati, kwa kuwa kulipa deni bila shuruti kunaendelea kuimarisha uhusiano mwema kati ya shirika hilo na wateja wake ili waweze kupanua na kuboresha huduma zaidi nchini.

Wakati huo huo, NHC imedhamiria kushirikiana na taasisi wakiwemo wadau mbalimbali nchini ili kurahisisha utekelezaji wa miradi yao.

"Ushiriki huo unalenga pia upande wa kuweka miundombinu muhimu katika miradi yetu kama vile barabara, maji, umeme na mingineyo,"amesema.

Akizungumzia kipaumbele cha nane, Bw.Suguya amesema kuwa, wamejipanga kuendelea kusimamia miliki ya nyumba za shirika hilo ambazo ni zaidi ya 18,622 nchini.

Usimamizi huo unalenga kuzifanyia matengenezo kupitia Mpango wa Matengeneo ya nyumba wa miaka mitano (2021/22-25/26). "Katika kufanikisha hili, shirika limetenga shilingi bilioni 50 kutekeleza mpango huo.Huu ni ukarabati mkubwa,utakaohusisha kubadilisha mapaa, vyoo na madirisha chakavu,"amefafanua Bw.Suguya.

Pia amesema, kipaumbele cha tisa ni kuangalia uwezekano wa kupunguza gharama za ujenzi kwa kuanzisha viwanda vitakavyosaidia kuzalisha vifaa vya ujenzi vinavyotumiwa na shirika.

Amesema, viwanda hivyo vitakuwa vinazalisha saruji, mabati, nondo na kokoto kwani wanaamini mpango huo ukifanikiwa utaongeza ufanisi mkubwa katika utekelezaji wa miradi yao nchini.

"Kipaumbele cha 10 kwa shirika letu ni kupitia upya Muundo wa Mpango Mkakati wa shirika ili muundo na mpango huo uwe na wigo mpana wa kusaidia kuleta ufanisi na kubeba majukumu makubwa ya sekta nyumba, Ilani ya Uchaguzi ya CCM na Mpango wa Taifa wa Maendeleo. Muundo na mpango mkakati unapitiwa na umma utataarifiwa ukikamilika,"amesema Bw.Saguya.

Amesema, kipaumbele cha 11 ni kuendelea kushirikiana na vyombo vyote vya habari nchini kama muhimili muhimu wa upashanaji wa habari kwa wananchi, uelimishaji na kujenga taswira ya shirika hilo la umma ambalo lina mtaji wa shilingi trilioni 5.01.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news