Njooni mjifunze mengi kuhusu Dodoma Jiji-Mafuru

NA DENNIS GONDWE

WANANCHI wameshauriwa kutembelea banda la Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika kilele cha maonesho ya Usalama na Afya mahala pa kazi yanayofanyika katika viunga vya ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alipokuwa akitoa taarifa ya Katibu katika mkutano wa kawaida wa Baraza la Madiwani uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Mafuru alisema kuwa katika viunga vya ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center yanaendelea maonesho yanayoratibiwa na Wakala wa Usalama na Afya mahala pa kazi. 

“Halmashauri ya Jiji la Dodoma ina banda katika maonesho hayo. Hivyo, nitumie nafasi hii kuwaalika wananchi wa Dodoma kutembelea banda hilo na kujionea na kusikiliza mambo mazuri yanayoendelea kutekelezwa katika Jiji la Dodoma na fursa mbalimbali zilizopo,”alisema Mkurugenzi Mafuru.

Kwa upande wa Mchumi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Roseria Hhari alisema kuwa wananchi wanakaribishwa kutembelea banda la Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kupata elimu na ushawishi wa kufikia fursa zilizopo katika Jiji la Dodoma. 

“Katika banda letu, mwananchi atapata fursa zilizopo katika Jiji la Dodoma, viwanja vilivyopo na maeneo ya kimkakati ya uwekezaji. Mfano, tuna viwanja katika maeneo ya Mtumba, Kikombo na eneo la viwanda Nala. Lakini pia tuna mashamba ya mjini eneo la Zuzu,”alisema Roseria.

Post a Comment

0 Comments