OR-TAMISEMI yatoa maelekezo muhimu Halmashauri ya Butiama

NA OR-TAMISEMI

NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dkt. Switbert Mukama amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kushirikiana na wakuu wa idara katika kuimarisha usimamizi wa miradi itakanayo na fedha za mapato ya halmashauri.
Dkt. Mukama ametoa wito huo leo Aprili 10,2022 alipotembelea utekelezaji wa ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Butiama unaogharimu shilingi Bilioni 3 ambao upo katika hatua ya umaliziaji.

“Kumekuwa na mazoea ya watendaji wa halmashauri kutoshirikiana katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo hasa inayotokana na mapato ya ndani na kupelekea miradi hiyo kutotekelezwa kwa viwango vinavyohitajika,”amesema Dkt. Mukama.

Dkt. Mukama amemtaka mkurugenzi kuhakikisha anatumia fedha za mapato ya ndani kutekeleza miradi yenye tija inayolenga kuleta maendeleo katika halmashauri hiyo huku akimtaka kuzingatia ubora na viwango, lakini pia thamani ya fedha ionekane katika miradi inayotekelezwa.
Wakati huo huo amemtaka Afisa Maendeleo ya Jamii kuhakikisha anazingatia kanuni na taratibu wakati wa utoaji wa mkopo wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na kuwachukulia hatua wanufaika ambao wanakwenda kinyume na taratibu za mkopo huo hasa katika suala zima la ucheleweshwaji wa marejesho ya mkopo.

“Jamani huu mkopo unatakiwa kurejeshwa ili wengine wanufaike, nakuagiza afisa maendeleo ya jamii zingatia kanuni unapotoa mkopo, lakini mnufaika ambaye anakiuka taratibu achukuliwe hatua,tusiende kwa mazoea,”amesema Dkt. Mukama.

Pia amemtaka afisa huyo kuhakikisha anatoa elimu ya kutosha juu ya usimamizi wa fedha na uendeshaji wa miradi kwa vikundi kabla ya kutoa mkopo ili kuibua miradi itakayonufaisha jamii na kuleta maendeleo katika Halmashauri ya Butiama.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Bi. Patricia Kabaka ameishukuru Serikali kwa utekelezaji wa ujenzi wa jengo la halmashauri na amemhakikishia Naibu Katibu Mkuu (TAMISEMI) kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati na kwa ubora zaidi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news