Rais Dkt.Mwinyi aipongeza India kwa kuunga mkono miradi ya maendeleo Zanzibar

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amezipongeza juhudi zinazochukuliwa na Ubalozi wa India nchini Tanzania kwa kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miradi mikubwa ya maji safi na salama.
https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2022/04/DSC_7667-scaled.jpg
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo katika mazungumzo kati yake na Balozi wa India katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Binaya Srikanta Pradhan, mazungumzo yaliofanyika Ikulu jijini Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi amesema kwamba katika kipindi kifupi tokea balozi huyo kuanza kazi zake katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameweza kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa Zanzibar kupitia nchi hiyo hatua ambayo inafaa kupongezwa.

Hivyo, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza haja ya kuendelea kufuatilia kwa karibu miradi hiyo ili iweze kutekelezwa kwa wakati uliopangwa ikiwemo miradi mikubwa ya maji safi na salama ambayo ujenzi wake unaendelea.

Akieleza kuhusu uendelezaji wa miradi mikubwa wa maji, Rais Dkt. Mwinyi alipongeza hatua zilizofikiwa katika uendelezaji wa miradi hiyo na kueleza matumaini yake ya kukamilika kwa wakati miradi hiyo ambayo inatekelezwa kwa mashirikiano ya pamoja kati ya Benki ya Exim ya India kwa njia ya mkopo wa masharti nafuu kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kwa upande wa utekelezaji wa rasilimali watu, Rais Dkt. Mwinyi aliupongeza mpango wa Serikali ya India wa kutoa nafasi za masomo kwa Tanzania ikiwemo Zanzibar ambapo nafasi hizo za masomo zitadhaminiwa na Serikali ya India.



Aidha, aliipongeza Serikali ya India kwa nia yake ya kuanzisha chuo cha amali kisiwani Pemba na kusema kwamba hatua hiyo itakuwa ni mchango mkubwa hasa kwa vijana walioshindwa kuendelea na elimu ya juu hapa Zanzibar.

Vile vile, alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kutoa ushirikiano wake katika azma iliyowekwa na Serikali ya India ya kuanzisha taasisi ya teknolojia ya habari hapa nchini kwani kuwepo kwa taasisi hiyo kutasaidia kuimarisha teknolojia ya habari na mawasiliano nchini.

Mapema, Balozi wa India katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Binaya Srikanta Pradhan, alimueleza Rais Dkt. Mwinyi hatua za makusudi zilizochukuliwa na Ubalozi wa nchi hiyo tokea alipokuja Ikulu Zanzibar kujitambulisha mnamo Septemba 16, mwaka jana.
https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2022/04/DSC_7643-scaled.jpg
Balozi Pradhan alimueleza Rais Dkt. Mwinyi kwamba Ubalozi wa India unathamini uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake na Zanzibar, hivyo utahakikisha unaisimamia vyema miradi yote inayotekelezwa na nchi hiyo.
 
Katika maelezo yake Balozi Pradhan alieleza matarajio yake makubwa na kumuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba miradi mikubwa wa maji safi na salama ambayo ujenzi wake unaendelea hivi sasa itakamilika kwa wakati uliopangwa.

Aidha, alitumia fursa hiyo kueleza azma ya Serikali ya India ya kuanzisha kwa chuo cha amali kisiwani Pemba hatua ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kutoa mafunzo ya amali kwa vijana.

Alieleza azma ya Serikali ya India ya kuimarisha uhushaino na ushirikiano wa kibiashara kati yake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku akieleza ujio mkubwa wa wafanyabiashara kutoka nchini humo mwezi Novemba mwaka huu kwa lengo la kuja kuangalia fursa zilizopo Tanzania.

Sambamba na hayo, alisifu ushirikiano mzuri uliopo kati ya India na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar na kueleza azma ya nchi hiyo ya kujenga kiwanda cha kutengenezea chanjo za maradhi kadhaa hapa nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news