Rais Dkt.Mwinyi ataja faida za kuhifadhi na kusoma Quran

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa, kufanya mashindano ya kuhifadhi na kusoma Quran katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ni fursa nyingine ya ibada na fadhila za kusoma Quran ndani ya mwezi huu.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj, Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi zawadi Mshindi wa Kwanza wa Mashindano ya Kimataifa ya Kuhifadhi Quran Zanzibar Juzuu 30 Tashjee,Nassir Rashid Seif na kulia kwa Rais ni Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi.(Picha na Ikulu).

Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo katika Masjid Zenjbar Mazizini katika fainali ya Mashindano ya Kimataifa ya kuhifadhi Quran yaliyozishirikisha nchi mbalimbali katika Bara la Afrika.

Katika hotuba yake, Alhaj Dkt. Mwinyi alieleza kwamba Uislamu unahimiza katika mwezi huu wa Ramadhani kufanyike jitihada katika kukithirisha kusoma sana Qur’an kwani huu ndiyo mwezi iliyoteremshwa katika usiku wa Laylatul Kadr.

Aliongeza kuwa, utaratibu huu wa mashindano ya kuhifadhi na kusoma Quran ni kuwaandaa Maulamaa na Masheikh wa baadae.

“Hili ni jambo jema linalojenga misingi mizuri ya Dini kwa vijana tangu wangali na umri mdogo na kuwafanya wakue wakiwa wameandaliwa vyema katika maisha ya ucha mungu na kufanya mambo ya kheri,”alisema Alhaj Dkt.Mwinyi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza katika hafla ya Mashindano ya Kimataifa ya Kuhifadhi Quran Zanzibar yaliofanyika katika Masjid Jamiu Zinjibar Mazizini Unguja Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Aidha, aliipongeza kwa dhati na kuishukuru sana Jumuiya ya Kuhifadhisha Quran Zanzibar kwa kuwa mstari wa mbele katika kuliendeleza jambo hilo la kheir tokea kuanzishwa kwa Jumuiya hii miaka 30 iliyopita.

Alitoa shukurani kwa Waislamu na wafadhili wote wanaohamasika kuchangia kwa namna moja au nyengine katika kuhakikisha mashindano ya kuhifadhi na kusoma Quran yanafanyika na kupata mafanikio kila mwaka.

Aliwapongeza wazazi kwa kuona umuhimu wa kuwasaidia vijana kushiriki katika mambo kama hayo ya kheri na kutoa shukurani maalum kwa walimu na Masheikh waliowaandaa kwa kuwasomesha vijana washiriki hadi wakaweza kufikia hatua hiyo ya fainali ya mashindano ya mwaka huu.

Sambamba na hayo, Alhaj Dkt. Mwinyi alitoa wito kwa Waislamu wote kujenga utamaduni wa kuchangia masuala mbali mbali yenye mnasaba wa kuimarisha Uislamu ikiwemo kusaidia ujenzi wa madrsa, misikiti pamoja na vituo vya Kiislamu.

Alhaj Dkt. Mwinyi pia, alipokea ombi la Jumuiya hiyo la kuwasaidia vijana waliohifadhi Juzuu 30 za Quran waliomaliza kidato cha Sita ambao wana sifa za kuendelea katika masomo ya chuo kikuu ambao hawakupata ufadhili wa masomo yao atawaunga mkono kwa kuwasaidia kuwatafutia wadhamini.

Pamoja na hayo, Alhaj Dkt. Mwinyi aliahidi kuiunga mkono Jumuiya hiyo katika ujenzi wa kituo chao cha mafunzo ya kuhifadhi Quran kinachotarajiwa kujengwa na Jumuiya hiyo.
Nae Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi alieleza umuhimu wa kuhifadhi Qur’an na kueleza imani aliyokuwa nayo kwa vijana hao ya kuuendeleza Uislamu katika nchi zao mbali mbali wanazotoka.
Mapema Amiri wa Jumuiya hiyo Sheikh Suleiman Omar Ahmed alitoa pongezi kwa Alhaj Dk. Mwinyi kwa kuungana nao katika mashindano hayo na kueleza uzoefu wa Jumuiya yao ambayo imetimiza miaka 30 tokea kuanzishwa kwake.

Alieleza kuwa matunda ya Jumuiya hiyo yanaonekana hivi sasa ambapo imepelekea kuzalisha vijana wengi waliohifadhi Quran pamoja na nchi nyingi katika Bara la Afrika kujitokeza kuja kushiriki katika mashindano hayo.

Pia, Sheikh Suleiman alitumia fursa hiyo kuwaombea vijana waliohifadhi Juzuu 30 za Qur’an waliomaliza kidato cha sita na wana sifa za kuendelea chuo kikuu kuwatafutia ufadhili ili wapate kujiendeleza katika elimu ya dini na dunia.

Katika mashindano hayo ya Juzuu 30 Hifdhi yaliwashirikisha wanafunzi 13 kutoka Zanzibar, Tanzania Bara, Kenya, Rwanda, Uganda, Burundi, Malawi, Niger, Msumbiji, Comoro, Nigeria na Chad.

Alhaj Dkt. Mwinyi alitoa zawadi kwa washindi na washiriki wote ambapo mshindi wa kwanza katika mashindano hayo alikuwa Hissein Youssouf Adam kutoka Chad na wa pili ni Saidi Doushimana kutoka Rwanda na mshindi wa tatu ni Hassane Djibrilla Oumarou kutoka Niger na wa nne ni Muslim Salum Seif kutoka Zanzibar.

Sambamba na hayo, mashindano mengine ya Juzuu 30 yalikuwa ni Tashjee Tahqiq yaliyowashirikisha washiriki wanne ambapo mshindi wa mwanzo alikuwa ni Nassir Rashid Seif kutoka Zanzibar na mshindi wa pili ni Rashid Hemed Rashid kutoka Zanzibar na wa tatu ni Mbarouk Mussa Juma kutoka Zanzibar na mshindi wa nne alikuwa ni Ahmad Kongo Kaginya kutoka Kenya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news