Rais mstaafu Mwai Kibaki afariki

NA DIRAMAKINI

RAIS mstaafu Jamhuri ya Kenya, Mzee Mwai Kibaki aliyehudumu kati ya mwaka 2002 na 2013 amefariki dunia.

Taarifa ya kifo cha Mzee Kibaki imetangaza leo Aprili 22,2022 na Rais Uhuru Kenyatta katika hotuba kwa taifa.
Mzee bKibaki alikuwa Rais wa Tatu tangu Kenya ipate Uhuru mwaka 1963.

Rais Kenyatta amemtaja kama kiongozi aliyekuwa katika mstari wa mbele kuimarisha uchumi wa Kenya.

“Mwai Kibaki atakumbukwa kwa weledi wake na bidii yake kazini. Kwa mujibu wa mamlaka yangu kama Rais wa Kenya, ninaamuru kwamba bendera ya Kenya itapeperushwa nusu mlingoti nchini na katika balozi zote za Kenya katika mataifa ya kigeni kuanzia leo Ijumaa hadi Rais mstaafu Kibaki atakapozikwa,” amesema Rais Kenyatta.

Kibaki aliingia Ikulu kupitia kwa tiketi ya National Rainbow Coalition (NARC) na akaapishwa Desemba 30, 2002, kutumikia taifa kama Rais wa Tatu wa Jamhuri ya Kenya.

Aidha,alihudumu kama kiongozi wa Taifa na Serikali hadi Aprili 9, 2013, alipokabidhi mamlaka kwa Rais Uhuru Kenyatta.

Rais Kenyatta amesema japo taifa linaomboleza, lakini pia ni muhimu kukumbuka wakati ambapo Kibaki alitumikia taifa pamoja na wakati mzuri aliofurahia na mkewe Mama Lucy Kibaki ambaye naye alitangulia mbele ya haki 26 Aprili 26, 2016 huko South Kensington, London, Uingereza.

Kibaki ni nani?

Mzee Mwai Kibaki alizaliwa Novemba 15, 1931, alikuwa kitinda mimba cha familia ya watoto wanane kutoka kwa mkulima kwa jina Kibaki Githinji na mkewe Teresia Wanjiku.

Akiwa mzaliwa kutoka kabila kubwa la Wakikuyu , aliishi katika Kijiji cha Gatuyaini katika kaunti ya Nyeri.

Alionesha uwezo wa kipekee wa kusoma wakati wa miaka ya shule ya msingi na alitumwa kujiunga na Shule ya Upili ya Man'gu, moja ya shule bora za upili nchini Kenya.

Kibaki alisomea katika shule hiyo kati ya mwaka 1947 na 1950.Matokeo mazuri yalimsaidia kupata ufadhili wa masomo ambapo alijiunga na chuo kikuu cha Makerere nchini Uganda ambapo alisomea Uchumi, sayansi ya kisiasa na historia.

Uongozi wake ulionekana alipokuwa mwenyekiti wa Muungano wa Wanafunzi katika chuo kikuu cha Makerere kabla ya kuhitimu na shahada 1955.

Baada ya kuhudumu kama naibu meneja wa kampuni ya mafuta ya Shell nchini Uganda, Mwai Kibaki alipata ufadhili wa kusoma katika chuo cha uchumi cha London.

Alihitimu na Shahada ya Uchumi na ufadhili wa umma (Public Finance), na alitarajiwa kutumia maarifa yake nchini mwake aliporudi 1958.

Kibaki alikubali wadhifa wa mhadhiri msaidizi katika somo la uchumi katika Chuo Kikuu cha Makerere.

Mwaka 1960, alijiuzulu wadhfa wake na kujiunga na Chama cha KANU ambacho kilikuwa chama tawala nchini Kenya wakati huo.

Mabadiliko kadhaa miaka michache iliofuata yaliisaidia Kenya kujipatia Uhuru wake kutoka kwa Uingereza na miaka mitatu baadaye Mwai Kibaki alikumbatia dunia ya uanasiasa.

Mwaka 1963, alichaguliwa katika Bunge la Kenya na kuendelea kuhudumu katika nyadhfa tofauti hadi alipoteuliwa kuwa waziri wa fedha na mipango ya kiuchumi na mwanzilishi wa taifa la Kenya marehemu mzee Jomo Kenyatta mwaka 1969.

Baada ya kujipatia uzoefu na kujiwekea sifa nzuri katika miaka yake ya kwanza katika siasa na Serikali, Mwai Kibaki aliteuliwa kama Makamu wa Rais chini ya uongozi wa rais.

Daniel arap Moi mwaka 1978, aliyechukua madaraka baada ya mzee Jomo Kenyatta kufariki.

Katika baraza la Mawaziri la Rais Moi, Kibaki alikabidhiwa Wizara ya Fedha.

Akiwa Waziri wa Fedha, Kibaki alianzisha mikakati na mabadiliko ambayo yaliiletea Kenya maendeleo.

Mwaka 1982 aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani. Mfumo wa Moi wa kuongoza uliendelea kuwa ule wa ukandamizaji na alibadilisha kifungu cha katiba na kukifanya chama tawala cha KANU kuwa chama pekee cha kisiasa.

Moi alichukua madaraka yote, na kumuondoa Kibaki kama makamu wa rais kabla ya kumpeleka katika nafasi ya Waziri wa Afya 1988, hatua ilioonekana na wengi kama kumshusha madaraka.

Tofauti ya kimawazo kati ya Moi na Kibaki ilipelekea msomi huyo wa chuo kikuu cha Makerere kujiuzulu kutoka KANU 1991.

Wakati huo raia walianza kulalamika kuhusu ukandamizaji uliokuwepo hatua iliozaa upinzani mkali dhidi ya rais Moi na kumfanya kubadili kifungu cha sheria ambayo ilikuwa imekihalalisha chama cha KANU kama chama cha pekee.

Kibaki alijiuzulu na kuunda chama chake cha Democratic Party DP .

Hata hivyo utawala wa Moi uliendelea kuwa thabiti licha ya taifa kuonekana kutoa upinzani mkali dhidi ya uongozi wake.

Alidaiwa kutumia mbinu za kikabila na ghasia kusalia madarakani katika chaguzi mbili zilizofuata. (DIRAMAKINI/BBC)

Post a Comment

0 Comments