SERIKALI KUSOMESHA CHUO KIKUU WANAFUNZI WATAKAOFANYA VIZURI MASOMO YA SAYANSI

NA DIRAMAKINI

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda (Mb) amesema katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2022/23 Wizara imetenga fedha kwa ajili ya kutoa ufadhili wa elimu ya juu (scholarships) kwa wanafunzi watakaofanya vizuri katika masomo ya Sayansi.
Waziri Mkenda amesema hayo Jijini Dodoma alipokutana na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ambapo amesema ufadhili huo utatolewa kwa asilimia mia moja kwa wanafunzi wachache na watasomeshwa ndani na nje ya nchi.

Amesema lengo la Serikali ni kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya juu na kuhamasisha watoto wengi kupenda kusoma masomo ya Sayansi.
Pia ametoa agizo kwa Bodi hiyo kujipanga ili ifikapo mwaka wa fedha 2023/24 kuanza kutoa mikopo kwa wanafunzi watakaosoma masomo ya Ufundi na ujuzi kwa ngazi ya Diploma.

"Kilio cha watu wengi kwa sasa ni ajira na sehemu ambayo ajira ni rahisi zaidi ni kwenye ufundi na ujuzi hivyo ni vizuri kujiandaa. Hili tunalisema mapema ili wanafunzi watakaoomba katika kipindi hicho wajue pia katika vyuo vya ufundi kuna fursa ya kupata mikopo," amesema Prof. Mkenda.

Mhe. Mkenda ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza bajeti ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kutoka bilioni 464 hadi kufikia bilioni 570, kuondoa adhabu ya asilimia 10 ya wanaochelewa kurejesha mikopo na kufuta asilimia 6 ya kulinda thamani.

Aidha Waziri Mkenda ametoa wito kwa wanafunzi wanaoomba mikopo ya elimu juu kutoa taarifa zote zinazotakiwa kwa ukamilifu na kwa wakati ili waweze kupata mikopo hiyo bila changamoto.
"Mkopo unatolewa kulingana na taarifa anazotoa mwombaji, ukitoa taarifa ambazo sio kamili kunakuwa na changamoto hivyo toeni taarifa kamili na Bodi itaendelea kuchakata taarifa hizo ili wanaostahili kupata mikopo wapate," amefafanua Waziri Mkenda.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Eliamani Sedoyeka amesema kwa sasa Wizara imejipanga kuhakikisha Watanzania wengi wanapata fursa ya kusoma elimu ya juu kwa kuwezesha kufanya hivyo kulingana na malengo ya Taifa letu.
"Wote tunafahamu juhudi ambazo Serikali imeweka kwenye elimu msingi ambazo zimepelekea kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne na sita na wakiwa na ubora na kupelekea kuwa na vigezo vya kuendelea na elimu katika ngazi inayofuata hivyo kupekelea kuhitajika fedha kwa ajili ya kusomesha," amesema Prof. Sedoyeka.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Prof. Hamisi Dihenga amesema anatambua kuwa wana dhamana kubwa ya kuhakikisha utaratibu wa kutoa mikopo unaeleweka kwa Watanzania wote na unawasaidia wale wanaostahili kupata mikopo na kuahidi kushirikiana na Menejimenti ya Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu kuhakikisha hilo linafanikiwa.

Post a Comment

0 Comments