Serikali yatoa maelekezo muhimu kwa watoa huduma za afya nchini

NA DIRAMAKINI

MGANGA Mkuu wa Serikali, Dkt.Aifello Sichalwe amewataka watoa huduma za afya nchini katika vituo vya binafsi na vya Serikali kutoa huduma kwa kufuata miongozo inayotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Afya ili kuboresha huduma kwa wananchi.
Dkt.Sichalwe amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa kujadili namna ya kuboresha utoaji huduma katika Sekta Binafsi ulioanza Aprili 12, 2022 jijini Dodoma.

"Mazoea ya kutoa huduma yanaweza kupelekea mazingira magumu sana ya kutoa huduma bora ndio maana Serikali ikakubali Sekta binafsi ishiriki kwenye kutoa huduma lakini kwa utaratibu wa kufuata miongozo inayotolewa na Wizara ya Afya,"amesema Dkt. Sichalwe.

Sambamba na kufuata miongozo kwa usahihi, Dkt. Sichalwe ameelekeza upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba na vitendanishi vyenye ubora ikiwa ni sehemu ya vichocheo vya kutoa huduma bora kwa wananchi wanaoenda kupata huduma katika vituo.

Aidha, Dkt.Sichalwe amesema huduma bora lazima ziendane na Watumishi wenye weledi wa kutosha, nidhamu, elimu na wanaofuata maadili ya taaluma yao kulingana na taratibu na Sheria za Mabaraza ya taaluma zao.

Kwa upande mwingine, Dkt. Sichalwe ameitaka Sekta binafsi kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa (survaillence) ili kutambua mapema magonjwa ya mlipuko na kuweka mikakati mizuri ya namna bora ya kupambana dhidi ya magonjwa hayo kwa kushirikiana na Serikali.

Hata hivyo, Dkt. Sichalwe ametoa wito kwa Sekta binafsi kuongeza ushirikiano kwa Serikali katika mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko pindi yanapoingia hali itakayoongeza kasi katika kudhibiti maambukizi kwa wananchi.

Nae Mkurugenzi wa Pharm Access,Dkt.Heri Marwa amesema, takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kwamba, udadi kubwa ya watu hufariki kwa kukosa huduma bora ukilinganisha idadi ya watu wanaoshindwa kwenda kupata huduma, hii inaonesha ni jinsi gani kama nchi tuna safari ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

Hata hivyo, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana na Sekta Binafsi katika kuwahudumia wananchi, hasa katika kipindi hiki ambacho kipaumbele cha Serikali kupitia Wizara ya Afya ni kutoa huduma bora kwa wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news