Tanzania kuzalisha Megawati 200 za umeme kupitia Jotoardhi

NA THERESIA MHAGAMA

SERIKALI imesema kuwa, Tanzania itazalisha umeme wa kiasi cha megawati 200 zinazotokana na Jotoardhi kabla ya mwaka 2025.
Watumishi mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC) wakigusa majimoto yanayotoka katika kisima kifupi cha utafiti cha Jotoardhi kilichochorongwa katika eneo la Kiejo-Mbaka wilayani Rungwe mkoani Mbeya. Wa Pili kutoka kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba na wa kwanza kulia ni Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi Mathew Mwangomba.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, alisema hayo wakati wa ziara yake ya kukagua vyanzo vya nishati ya Jotoardhi vya Kiejo-Mbaka na Ngozi mkoani Mbeya.

Alisema kuwa, Tanzania kuna jumla ya maeneo 52 yanayoweza kutoa nishati ya Jotoardhi ambayo tayari yameshatambuliwa.

Alieleza kuwa, kwa ujumla, Serikali ina mpango wa kuongeza megawati 1100 zinazotokana na Nishati Jadidifu kabla ya mwaka 2025 na hizo megawati zitatokana na vyanzo mbalimbali kama vile Jotoardhi, Jua na Upepo.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba ( wa Nne kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi katika eneo la Ngozi mkoani Mbeya ambapo kuna chanzo cha nishati ya Jotoardhi itakayozalisha umeme. Kulia kwake ni Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi Mathew Mwangomba.

Aliongeza kuwa, Wizara ya Nishati inaweka nguvu kubwa katika kuendeleza vyanzo vya nishati ya Jotoardhi kwa sababu vyanzo hivyo haviishi na hivyo ukaguzi alioufanya katika maeneo hayo ya Jaothemo utasaidia Serikali kuona hatua stahiki za kuchukua ili kuendeleza vyanzo hivyo.

“Kipindi cha ukame maji yanaweza kupungua, lakini Jotoardhi katika kipindi cha ukame au mvua, mvuke unaotoka chini ya ardhi uko palepale,"alisema Katibu Mkuu.

Alisema kuwa, nchi ya Kenya ina zaidi ya megawati 1100 zinazotokana na Jotoardhi na Tanzania kutokana na eneo lake kubwa kupitiwa na Bonde la Ufa kuna uwezekano wa kupata umeme mwingi zaidi unaotokana na nishati hiyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba akifungua valvu ili kuruhusu majimoto yanayotoka ardhini kupita katika kisima kifupi cha utafiti cha Jotoardhi kilichochorongwa katika eneo la Kiejo-Mbaka wilayani Rungwe mkoani Mbeya.

“Mfano hapa mkoani Mbeya katika eneo hili la Rungwe kumeonekana kuna uwezekano mkubwa wa kutoa nishati ya Jotoardhi kwa sababu tawi moja la Bonde la Ufa limeingia katika eneo hili na Tawi jingine limeelekea upande wa Malawi,"alieleza Mhandisi Mramba.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi Mathew Mwangomba alisema kuwa, eneo la Kiejo-Mbaka linaweza kuzalisha megawati 60 zinazotokana na Jotoardhi.

Alisema kuwa, Serikali imetoa takribani shilingi Bilioni 20 kwa ajili ya uendelezaji wa eneo hilo na sasa wamenunua mtambo wa kuchoronga eneo hilo, na kwamba, Wataalam wa TGDC na Wahisani wameshirikiana katika kufanya tafiti zote zinazotakiwa.
Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba akigusa maji ya moto yanayotoka katika kisima kifupi cha utafiti cha Jotoardhi kilichochorongwa katika eneo la Kiejo-Mbaka wilayani Rungwe mkoani Mbeya. Kulia kwake ni Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi Mathew Mwangomba.
Kisima kifupi cha utafiti cha Jotoardhi kilichochorongwa katika eneo la Kiejo-Mbaka wilayani Rungwe mkoani Mbeya,

Aliongeza kuwa katika eneo la Ngozi, inategemewa kuwa litazalisha megawati 70 zinazotokana na Jotoardhi na kwamba TGDC imejipanga vizuri katika kuhakikisha kuwa Tanzania inapata umeme kutoka kwenye nishati hiyo Jadidifu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news