TPDC YAZIDI KUCHANJA MBUGA MICHEZO YA MEI MOSI 2022

NA DIRAMAKINI

KATIKA michezo ya maaadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani maarufu Mei Mosi 2022 inayoendelea mkoani Dodoma, timu za Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) zimeendelea kufanya vizuri katika michezo yao ya kuvuta kamba upande wa wanaume, wanawake pamoja na mpira wa miguu.
Wachezaji wa Timu ya Kamba ya Wanawake TPDC, Queen Monsters wakiwavuta wenzao wa Wizara ya Maji (hawapo pichani) katika mchezo uliomalizika kwa TPDC kushinda mivuto 2 kwa 0.

Katika michezo iliyochezwa Aprili 20,2022, timu ya mpira wa miguu ya TPDC maarufu TPDC Heroes iliisambaratisha Timu ya Halmashauri ya Kongwa kwa kuinyuka magoli mawili bila majibu katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri Mkoani Dodoma.

TPDC Heroes baada ya kuanza kwa kupoteza mechi ya kwanza dhidi ya Wizara ya Nishati, ilionekana kubadilika na kutandaza kandanda safi ambalo lilionekana kuwachanganya wapinzani wao hao kutoka Kongwa.

TPDC ilijipatia mabao yake kupitia kwa washambuliaji wake Patrick Kabwe aliyeunganisha kwa kichwa krosi iliyopigwa na beki Yoctan Robert. 

Baada ya goli hilo, Kongwa walionekana kuamka na kulisakama lango la TPDC, lakini hata hivyo TPDC HEROES ilifanikiwa kuandika goli lake la pili kupitia kiungo mshambuliaji Hans Kyando baada ya kugongeana pasi kadhaa na kisha kuusukumiza mpira wavuni.

Hadi mpira unamalizika, TPDC HEROES 2 Kongwa 0 na kwa matokeo hayo TPDC inafikisha alama 4 na kuzidi kuweka hai matumaini yake ya kusonga mbele.

Kwa upande wa michezo ya Kamba wanaume, timu ya TPDC maarufu the Monsters, ilifanikiwa kuwafurusha wenzao wa TANESCO kwa kuwavuta kwa mivuto yote miwili bila majibu. 

Kwa upande mwingine, timu ya Kamba ya wanawake ya TPDC “THE Queen Monsters” nayo ilifanikiwa kuwaondosha wapinzani wao kutoka ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuwavuta kwa mivuto yote miwili.

Aidha, katika michezo ya Aprili 21,2022, timu ya TPDC ya Kamba upande wa wanawake, iliendeleza upbabe wake kwa timu za Wizara ya Maji, baada ya kuwavuta kwa mivuto miwili bila majibu.

Akizungumzia matokeo hayo ya TPDC, Afisa Habari wa TPDC, Bwana Eugene Isaya alisema kuwa matokeo hayo yametokana na nidihamu, juhudi za mazoezi pamoja na kufuata maelekezo ya walimu wakati wa mazoeizi. 

“Tulionekana kuanza taratibu, lakini mazoezi, nidhamu ya mchezo vimetusaidia sana pamoja na kufanyia kazi maelekezo ya walimu,” alisema Bwana Eugene.

Bwana Isaya aliongeza kwamba, “TPDC inawachukulia wapinzani wote kwa uzito sawa, na haitadharau timu yoyote kwani lengo ni kushinda michezo yake yote na hivyo kujiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa vikombe.

TPDC itakuwa uwanjani tena Aprili 22,2022 kuwakabili wenzao kutoka Wizara ya Kilimo kwenye mchezo wa kuvuta kamba wanawake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news