Polisi aliyefutwa kazi, kunusurika kifo kwa utumiaji dawa za kulevya alivyogeuka kuwa nuru kwa Waraibu Tanzania-3

NA GODFREY NNKO

CHAPISHO lililopita la Aprili 20, 2022 tuliona namna ambavyo safari mpya ya aliyekuwa askari wa Jeshi la Polisi ambaye baadaye alifutwa kazi na kufungwa jela, Bw.Twaha Amani alipoanza safari nyingine ya ajira ya ualimu baada ya msoto wa miaka kadhaa nyumbani.
"Basi nikiwa kijijini nilimaliza pesa zote, sikufungua cha akaunti na nikawa nimeishiwa pesa nikaanza kukopa kwa watu wakinipa naenda kuvuta unga Mwanza, hatimaye nikaanza kuishi huko Mwanza nikaacha kufundisha, nikaanza kuiba na kuvuta mpaka niliweka vyeti vyangu bondi kwa shilingi 30,000, Endelea chapisho la tatu…

Aacha kufundisha, aanza wizi

Bw.Amani anasema, baada ya kuacha kufundisha mkuu wa shule aliyemtaja kwa jina moja la Bw. Shitunduru alikuwa anaenda mjini kumuulizia huko Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.

“Wakati huo simu sina,nilipata matatizo nilienda kwenye nyumba za watu nikaiba ndoo ya rangi tupu huko Mwanza Mjini ilikuwa inauzwa elfu 15,000 walitumia kupimia mahindi na samaki halafu mimi naenda kuuza ili nipate fedha za kununulia unga (heroine).

“Siku hiyo nilikamatwa, nilipigwa sana akatokea askari mmoja alikuwa, Bw.Godfrey Babeto alikuwa anafanya kazi Tabora akahamishiwa Mwanza, nilimpa mtu akampigia simu alifika pale, lakini akashindwa kunitetea maana watu walikuwa wengi sana ila aliwazuia wasinipige ila wakanipeleka kituo cha polisi,nikiwa hapo kituoni nikamuona askari mmoja, Bw.Emanueli Mtui ninamfahamu kipindi ninamaliza Depo yeye alikuwa anaingia kipindi hicho cha nyuma.

“Nikamuelezea mkasa wangu wote, japo mwanzoni tulikuwa tunakutana mtaani Mwanza, namdanganya kwamba nipo ninafundisha yeye alikuwa hajui, kwa hiyo akajua kumbe nilikuwa namdanganya.

“Basi akawa ananiletea chakula kituoni maana ni rafiki yangu kama mdogo wangu, lakini akawa amewasiliana na ndugu zangu huko Moshi alikuwa anawafahamu, na kuwaeleza kwamba nipo huku na yuko polisi, basi wakamwambia tunakutumia pesa apambane nitoke, halafu nipelekwe Moshi moja kwa moja nisiende popote,"anasema.
 
Bw. Amani anasema, askari ambaye alimuokoa naye inasemekana alikuja kusimamishwa kazi kwa sababu ya ulevi wa pombe.

Arejeshwa nyumbani Moshi

“Lakini nilikaa jela kama siku 14 nikapelekwa mahakamani, basi nikakutana na huyo askari ni jamaa yangu akawa amemuelezea hakimu akamuomba aniachie, hakimu alikubali kwa masharti ya kutoonekana Mwanza, maana nimeshaharibu sana Mwanza, basi akanitoa akanifunga pingu akaniambia Twaha ndugu zako wameniambia nikusafirishe na tayari nina tiketi kwa hiyo nakupeleka mahali ukakae halafu kesho tuondoke.

“Basi akataka anipeleke kwake, lakini akaogopa akihisi ninaweza kutoroka basi akanipeleka Kituo cha Polisi Igogo, akawaeleza polisi wenzake kwamba namuacha huyu jamaa nitampitia kesho, basi akaniletea chakula nikawekwa ndani mpaka kesho yake asubuhi mapema akanipitia kunichukua tayari kuelekea Moshi .
 
Anasema, katika Kituo cha Igogo pia alimkuta kijana ambaye nae alikuwa antokea Moshi,"kumbe yule kijana alikuwa ni mwizi, kwa hiyo alikuwa amepigwa sana na wananchi na hali yake ilikuwa mbaya sana baada ya mimi kufika Moshi kama baada ya siku tatu nilikuja kusikia yule kijana alifariki,"anasema Bw. Amani.
 
Afungiwa ndani

“Lakini tukiwa bado hatujaanza safari, nikamuomba twende nilipokuwa nafundisha nichukue vyeti vyangu, akakataa kabisa akaniambia Twaha ndugu zako wamesema nikupeleke mguu kwa mguu basi tukaondoka kuelekea Moshi,alivyonifikisha tu nyumbani nikafungiwa ndani chumbani kama miezi sita,"anasema Bw. Amani.
 
Anasema, akiwa amefungiwa ndani nyumbani kuna mtoto wa Mjomba wake alikuwa akivuta bangi ambaye katika kipindi hicho alikuwa akimletea na kumpa kwa dirishani hivyo kuvuta,ila baadae huyo mtoto wa mjomba naye alikuja kuingia kwenye matumizi ya unga na hivi sasa yupo nae pia kwenye kituo chake anapata tiba.
 
"Ila baada ya hiyo miezi kufungiwa ndani na baadae kutolewa nje, kuna Anko wangu akawa ananipitia tunaenda kwenye mashamba yake ya mpunga huku akiangalia kama nimebadilika, lakini mimi nikaendelea kuvuta unga na baadae nikamtoroka nikaingia mtaani."

Wizi na kifo

“Nilikutana na jamaa ambaye alikuwa ananichoma sindano hapo awali, basi akaniambia kwa nini unaishi kwenye mapagale, njoo tukae wote nyumbani basi nikaanza kuishi kwao tukawa tunaenda kwenye mizunguko kuiba, kukaba watu ila yeye alikuwa ni mwizi wa usiku.
 
"Siku hiyo ilikuwa Jumamosi akanishawishi tuibe usiku, nikamwambia siibagi usiku, sijazoea kuvunja majumba ya watu ila akanishawishi sana ikabidi twende, tulikuwa watatu tukavunja nyumba ya kwanza, ya pili na ya tatu, watu wakatushtukia wakapiga kelele ya wezi, ndipo wakamkamata rafiki yangu wakampiga sana,wakamkata maskio,uume mpaka wakamuua, lakini na sisi akawa ametutaja.

“Basi habari zikawa zimesambaa wakapigiana simu. Mimi kulivyopambazuka nikaenda kutoa vitu tulivyoviiba nikavipeleka kuviuza, nikaenda nyumbani nikakutana na mama yangu akawa ananipigia kelele kwamba alinichukulia dawa kwa mganga wa kienyeji za kuacha kuvuta unga (heroine) basi nilioga tu, lakini akili haipo hapo, mama hajui kama kuna msanla umetokea usiku.

“Basi nilipomaliza nikarudi kwa yule jamaa mara ya pili kufuata vitu, nikakutana na watu wanalia na nikamuona mama yake mzazi akivuta sigara, kwa mara ya kwanza akawa ananiambia Twaha angalia nilimzuia mwenzako asiende mtaa ule usiku kuiba hakunisikiliza angalia sasa wamemuua.
 
"Hapo hajui kama tulikuwa wote usiku, basi nikachukua vitu na kwenda kuviuza, nikanunua unga (heroine) nikavuta unga nikaondoka zangu nyumbani moja kwa moja nilipofika nikakuta taarifa zimeshasambaa mtaani kwamba nilikuwa na huyo aliyeuawa usiku."

Awindwa auawe

“Basi ndugu zangu wakawa wananishawishi niende Arusha kwa ndugu, lakini Anko wangu akasema hata akipelekwa huko watamkamata ni karibu, bora apelekwe jela wakati huo huo watu walishazingira nyumbani, siwezi kutoroka tena.

“Likaja gari la Noah wakanipakiza humo, wakanunua mafuta ya petroli na kibiriti wakanipeleka mpaka Kituo cha Polisi, wakanirushia hapo na mafuta wakasema tulitaka kumchoma moto, siku hiyo nakumbuka ilikuwa Jumapili ya tarehe 14 siku wanamzika Mandela Rais wa Afrika Kusini mwaka 2013,nimekaa pale kituoni vikaletwa vile vitu tulivyoviiba usiku maana tuliviacha nje basi nikaendelea kukaa pale kituoni na mwili ukapelekwa mochwari Mawenzi,"anasema. 

Anasema,petroli waliyonunua pamoja na kibiriti ile ilikuwa ni kumsingizia kuwa alikuwa anataka achome moto nyumba wanayoishi kama gia tu ya kumpeleka jela. 

“Na mimi nilikaa pale mpaka Krisimasi ikanikutia pale maaana hapakuwa na mtu wa kuja kutoa maelezo, nikapelekwa Gereza la Karanga, nikakaa miezi sita ilikuwa 2013 nikatoka 2014 nikiwa nimependeza sana, maana huko jela nilikutana na waliotuhumiwa kumuua Erasto (Bilionea wa madini ya Tanzanite, marehemu Erasto Msuya) waliposikia naitwa Teacher."

 
ITAENDELEA

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news