Wataalam wa OR-TAMISEMI wazikumbusha jambo muhimu halmashauri kuepusha usumbufu

NA OR-TAMISEMI

TIMU ya Wataalam kutoka Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (0R-TAMISEMI) imezitaka halmashauri kutumia ramani na michoro ambayo imetolewa na mamlaka wakati wa utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya nchini.
Lengo likiwa ni kuepusha marekebisho yasiyo ya lazima ambayo yanachangia kuongezeka kwa gharama ya utekelezaji wa miradi.

Pia imewataka wajumbe wa Timu ya Usimamizi na Uendeshaji wa Shughuli za Afya Ngazi ya Halmashauri(CHMTS) kujua ramani ya majengo yatakayojengwa katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kama kuna mapungufu yoyote yabainishwe mapema kabla ya kuleta athari zaidi.

Wito huo umetolewa leo Aprili 29,2022 katika kikao kazi cha Timu ya Ufuatiliaji wa Shughuli za Afya kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Shughuli za Afya Mkoa wa Mwanza.
Akizungumza kwa niaba ya timu hiyo, Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt.Ntuli Kapologwe amesema, kutokujua ramani za majengo kunapelekea kufanya maboresho na marekebisho madogo madogo ambayo yanasababisha upotevu wa fedha ambazo zingetumika katika shughuli nyingine.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Dawa na Huduma za Afya za Kiuchunguzi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mathew Mganga amezitaka CHMTS kuwa wabunifu na kufungua maduka ya madawa ambayo yatakuwa chanzo kizuri cha mapato, lakini pia kamati hiyo iimarishe usimamizi wa mapato yatokanayo na huduma za maduka ya dawa hayo ili yatumike kuongeza mtaji na kuhudumia maeneo mingine ambayo hayazalishi fedha sambamba na shughuli nyingine za maendeleo.
Wakati huo huo,timu hiyo imetoa wito kwa wajumbe hao kuhakikisha wanaongeza kasi katika ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya hasa katika halmashauri ambazo bado zipo nyuma ya muda ili utekelezaji huo ukamiike kwa wakati.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news