Waziri Bashungwa atoa maagizo kwa wakurugenzi wa halmashauri kuhusu utamaduni, sanaa na michezo

*Mheshimiwa Mchengerwa asema mambo mazuri yanakuja

NA OR- TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amewaelekeza wakurugenzi wote nchini kuhakikisha Kitengo cha Utamaduni, Sanaa na Michezo kinapewa kipaumbele sawa na vitengo vingine na kukiwezesha ili kiweze kuwahudumia Watanzania katika halmashari zote.
Waziri Bashungwa amesema hayo leo Aprili 6, 2022 jijini Dodoma wakati akifunga kikao kazi cha 13 cha Maafisa Utamaduni na Michezo ambapo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan kuridhia kuanzishwa Kitengo cha Utamaduni, Sanaa na Michezo na kumuagiza Katibu Mkuu OR-TAMISEMI kusimamia utekelezaji wa kuanzishwa kitengo hicho kipya cha utamaduni, sanaa na michezo.

Akifunga kikao kazi hicho, Waziri Bashungwa amewaelekeza watendaji wote wanaohusika na utekelezaji wa mabadiliko ya muundo wa kada za Maafisa Utamaduni na Maafisa Michezo ulioidhinishwa kutekelezwa haraka iwezekanavyo ifikapo Julai 1, 2022.
“Niwahakikishie, maelekezo ya Waziri Mkuu aliyayatoa hapa wakati wa kufungua kikao kazi hiki tutayatelekeza pamoja na maazimio yanayohusu utekelezaji kwa upande wa TAMISEMI ninaahidi yatafanyiwa kazi na kutolewa taarifa kila baada ya miezi minne kama ilivyo kwa taasisi nyingine ili tunapokutana katika kikao kazi kingine, tuwe na taarifa ya jumla ya utekelezaji na tusonge mbele zaidi,” amesema Waziri Bashungwa.
Katika kutekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri Bashungwa amewaagiza Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Katibu Mkuu OR-TAMISEMI kukaa mara moja na kuchambua maelekezo ya Waziri Mkuu ili yafanyiwe kazi kwa wakati kwa manufaa ya kuwahudumia Watanzania nchi nzima.

Kwa upande wake Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema, wizara yake inashirikiana kwa karibu na OR-TAMISEMI katika kutekeleza majukumu na maelekezo ya viongozi ili kufikia azma ya Serikali.
“Tunakwenda kufanya mapinduzi makubwa ya kiutendaji katika wizara hii, kila mmoja wetu aende kuchapa kazi tukawape furaha Watanzania, nendeni mkawe wanyenyekevu na muwe karibu na wananchi ili tufanikishe malengo ya Serikali. Jengeni mahusiano mazuri na wananchi ili tufanye mapinduzi ya kiutendaji katika sekta hizi muhimu kwa nchi, hii ni wizara ya raha na starehe,”amesema Waziri Mchengerwa.

Aidha, Waziri Mchengerwa amesema kuwa, wizara hiyo ni nguvu laini (soft power) ya nchi, hivyo maafisa hao wametakiwa kuweka uzalendo na utaifa mbele ili sekta hizo ziweze kuwa na tija kwa taifa na wananchi wake kwa maendeleo endelevu.
Kikao kazi cha Maafisa Utamaduni na Michezo ni cha 13 tangu kuanzishwa kwake 2009 na kinajumuisha maafisa hao kutoka mikoa yote Tanzania Bara pamoja na halmashauri zote nchini ambapo mwaka huu kimefanyika kwa siku tatu kuanzia Aprili 4-6, 2022 kwa kufunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news