ANWANI ZA MAKAZI KUWEZESHA ZOEZI LA SENSA KIDIJITALI

NA DIRAMAKINI

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mohammed Khamis Abdulla amesema kuwa kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania zoezi la sensa ya watu na makazi kwa mwaka 2022 linakwenda kufanyika kidijitali kupitia mfumo wa Anwani za Makazi.
Akizungumza katika ziara yake ya kikazi ya kukagua na kuhamasisha utekelezaji wa mfumo wa Anwani za Makazi katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, Bwana Abdulla amesema kuwa ili zoezi la sensa lifanyike kwa ufanisi ni lazima mfumo wa utambuzi wa watu na makazi ukamilike kwa asilimia 100 ambao si mwingine ni Mfumo wa Anwani za Makazi.

“Sensa ya mwaka huu 2022 ni sensa ya kidijitali kwa kuwa itatumia Mfumo wa Anwani za Makazi na kufanikisha hili ni vema kuhakikisha taarifa zote za wakazi na makazi ziwe zimeingizwa kwenye mfumo wa utambuzi, kila nyumba iwe na namba na kila barabara na mtaa uwe umewekwa nguzo yenye jina ya barabara na mitaa,” amesisitiza Bwana Abdulla.

Ameongeza kuwa, zoezi la uwekaji wa miundombinu ya Anwani za Makazi linahitaji ubunifu zaidi kuliko wakandarasi, akitolea mfano wa kutumia rangi ya njano na nyeusi kuweka namba ya nyumba badala ya kutumia wakandarasi kuchonga kibao cha namba ya nyumba kwa gharama kubwa.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Makame Machano Haji amesema kuwa zoezi hilo limeendelea kufanyika kwa ushirikiano mkubwa kuanzia ngazi ya Wizara mpaka mabaraza ya vijana na masheha ambapo kazi ya kukusanya na kuingiza taarifa ya wakazi na makazi kwenye mfumo imefanyika kwa asilimia 111 na zoezi la uwekaji wa namba za nyumba na nguzo zenye majina ya barabara na mitaa linaendelea kufanyika.

Aidha, utekelezaji wa Mfumo huo kwa mkoa wa Kaskazini bado haujakamilika kwenye uwekaji wa nguzo zenye majina ya barabara na mitaa pamoja na namba za nyumba ambapo katika kikao cha Naibu Katibu Mkuu huyo na watendaji wa Mkoa wa Kaskazini waliafiki kwa pamoja kuwa ifikapo tarehe 15 ya mwezi Mei, 2022 zoezi hilo litakuwa limekamilika na tarehe 16 timu ya wataalamu itakwenda kuhakiki ukamilifu wa zoezi hilo.

Post a Comment

0 Comments