Awataka watafiti wa kilimo kuwapa matokeo wakulima waweze kujikita katika kilimo biashara badala ya kilimo cha kujikimu

NA DIRAMAKINI

MKOA wa Pwani umewataka watafiti wa kilimo nchini kuwapatia wakulima matokeo ya tafiti wanazofanya ziweze kuleta mabadiliko kwa wakulima ili waende kwenye kilimo biashara na siyo cha kujikimu.
Hayo yalisemwa na mkuu wa Wilaya ya Kibaha Sara Msafiri ambaye alimwakilisha mkuu wa mkoa wa Pwani wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mkulima yaliyoandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Kibaha.

Msafiri amesema kuwa, watafiti hao wanapaswa kutumia tafiti hizo kwa vitendo kwa wakulima ambapo serikali imetenga bajeti kubwa ambayo haijawahi kutokea na imeonyesha jinsi gani serikali ilivyotoa kipaumbele kwenye sekta ya kilimo ili ilete mapinduzi, kwani ikifanikiwa hata pato la mwananchi na nchi litaongezeka kwani uchumi unategemea kilimo.

Amesema kuwa, kilimo ni kila kitu endapo kila mhusika atatumia ujuzi na maarifa yake ambapo serikali kwa upande wake tayari imeshawezesha kwa masuala ya bajeti na wataalamu kwa kuwapatia vitendea kazi.

Amebainisha kuwa, kilimo ni sayansi hivyo watafiti wana nafasi kubwa ya kutumia sayansi hiyo ili kuboresha kilimo ambacho kwa sasa ndiyo sekta yenye manufaa makubwa ukilinganisha na sekta nyingine.

Naye mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa TARI Dkt. Juliana Mwakasendo alisema kuwa kupitia vituo vyake 17 vitaendelea kutekeleza maagizo ya serikali ili wakulima waweze kuongeze tija kwenye kilimo kwa kuhakikisha ubunifu wa mbegu zinazoendana na mabadiliko ya tabia nchi.

Kwa upande wake Meneja wa TARI Kibaha, Hildelitha Msita alisema kuwa maadhimisho hayo yalifanyika kwenye kituo hicho kwa kuwapatia mafunzo mbalimbali wakulima kutoka kwenye baadhi ya halmashauri za mkoa huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news