Diwani Josephine Gunda agawa taulo za kike kwa wanafunzi

NA ROTARY HAULE

DIWANI wa Viti maalum katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini iliyopo mkoani Pwani, Josephine Gunda ametoa msaada wa taulo za Kike kwa wanafunzi 168 wa Shule ya Sekondari Kwala na Magindu.
Gunda ametoa msaada huo katika ziara yake aliyoifanya wakati tofauti katika Kata ya Kwala na Magindu akiambatana na mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Erasto Makala.

Katika ziara hiyo, Gunda alitembelea Shule ya Sekondari Kwala na kutoa msaada wa taulo za kike 96 kwa wanafunzi wa shule hiyo na kisha kuendelea na ziara yake Shule ya Sekondari Magindu na kutoa taulo za kike 72 .

Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo, Gunda amesema kuwa, kutoa msaada huo ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake ya udiwani kama alivyoahidi wakati wa kugombea.

Amesema, wanafunzi wa kike huwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za kibaiolojia na kwamba taulo hizo ni sehemu ya mahitaji yao ndio maana aliona awasaidie ili ziweze kuwasitiri .
"Leo nimefanya ziara ya kutembelea Shule za Sekondari na Msingi zilizopo Kata ya Kwala na Magindu kwa kutoa misaada mbalimbali lakini kwa Shule za Sekondari niliona nitoe msaada wa Taulo za Kike kwa wanafunzi kwakuwa ndio mahitaji yao Muhimu,"amesema Gunda.

Gunda,amesema kuwa ziara hizo zitakuwa endelevu kwa kila Kata kwakuwa anaamini mahitaji ya wanafunzi hao bado ni makubwa huku akisema kuwa misaada hiyo ataitoa kulingana na mahitaji ya eneo husika.

Aidha,katika ziara hiyo Gunda,amewataka wanafunzi hao kuhakikisha wanaripoti kwa haraka matukio ya ukatili yanayotokea dhidi yao ili yaweze kushughulikiwa ipasavyo.
"Nawaomba wanafunzi wote mhakikishe mnaungana kupinga vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ,mkiona mnafanyiwa vitendo vibaya toeni taarifa mapema kwa mamlaka husika za Serikali na hata kwa Wakuu wa Shule,"amesema Gunda

Gunda ameongeza kuwa, wapo baadhi ya watu ambao wamekuwa wakiwafanyia vitendo vya ukatili wanafunzi wa kike lakini matukio hayo hayaripotiwi hivyo kwasasa lazima wawe mstari wa mbele kuripoti ili kusaidia kuweka mazingira mazuri ya kusoma.

Amewapongeza walimu wa Shule hizo kwa jitihada za kusimamia maadili na hata ufundishaji wa kujituma huku akiwaomba waendelee na juhudi hizo huku Serikali ikiendelea kutatua changamoto zao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini Erasto Makala,amepongeza juhudi za diwani huyo huku akisema msaada alioutoa ni mkubwa kwa wanafunzi hao.
"Nipongeze juhudi za diwani huyu wa Vitimaalum Josephine Gunda kwa kutoa msaada huu muhimu kwa wanafunzi wakike wa Kata hizi mbili naimani utawasaidia katika kukabiliana na changamoto zao,"amesema Makala

Hata hivyo,mmoja wa wanafunzi hao Fatuma Said, amemshukuru diwani huyo kwa msaada aliotoa huku akiomba aendelee kuwasaidia bila kuchoka kwakuwa mahitaji hayo ni endelevu.

Post a Comment

0 Comments