Dkt.Magembe amwakilisha Waziri wa Afya kikao muhimu jijini Geneva

NA OR-TAMISEMI

NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) anayeshughulikia Afya,Dkt.Grace Magembe tarehe 25, Mei ,2022 amemwakilisha Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Ally Mwalimu katika kikao cha kujadili utekelezaji na maeneo ya kipaumbele katika kukabiliana na kudhibiti maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na Kifua Kikuu kwa watoto.
Katika kikao hicho kilichofanyika jijini Geneva nchini Uswisi, Dkt.Magembe alieleza hatua kubwa iliyopigwa na Serikali ya Tanzania ikiwemo kuongeza vituo vya upimaji afya ya msingi zaidi ya 1,593 katika kipindi cha miaka sita.

Vituo ambavyo vimejengwa, kwa lengo la kuongeza vituo vya kutoa huduma za HIV na TB ikiwemo maabara na mashine za kupima magonjwa hayo kwa watoto wadogo, kutekeleza mkakati wa kupima watoto katika ngazi ya jamii, shule na kuwapa kinga ya kifua kikuu watoto wanaotoka kwenye familia zenye watu wazima wanaougua kifua kikuu kwa lengo la kuwakinga watoto wasipate maradhi hayo.
Aidha, ameongelea ushirikiano mkubwa uliopo kati ya Serikali, taasisi na mashirika ya dini katika kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kupima VVU na TB.

Ameeleza, mipango ya Serikali ya kuongeza upimaji kwenye ngazi ya afya ya msingi na jamii, kuongeza ushirikiano na taasisi za dini, wadau wa maendeleo na asasi za kiraia ili kuwapima watu wengi wakiwemo watoto kabla hawajapata madhara makubwa ya kiafya.

Pia ameongelea mkakati wa Serikali kuendelea kununua dawa zinazotibu kwa muda mfupi zaidi na rafiki kwa watoto kwa kuzingatia umri na uzito wao.
Hadi sasa asilimia 75 ya watoto chini ya miaka mitano ambao wanaishi kwenye familia zenye maambukizi ya kifua kikuu, wanapatiwa dawa kinga na Serikali na amewahakikishia wadau kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na jumuiya za kikanda na kimataifa katika kuboresha huduma za UKIMWI, Kifua Kikuu na magonjwa yasiyoambukiza ili kuepusha vifo visivyo vya lazima.

Post a Comment

0 Comments