HGWT yashirikiana na Serikali kutoa elimu namna ya kudhibiti vitendo vya ukatili wa kijinsia

NA FRESHA KINASA

SHIRIKA la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) lenye makao makuu yake Mugumu Wilaya ya Serengeti mkoani Mara linaloongozwa na Mkurugenzi wake, Rhobi Samwelly kwa kushirikiana na Dawati la Jinsia na Watoto, Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii wilayani humo wanaendelea na utoaji wa elimu ya madhara ya vitendo vya ukatili wa kijinsia katika shule za msingi sambamba na uundaji wa vilabu vya wanafunzi wa kupinga vitendo hivyo.
Hatua hiyo, ni sehemu pia ya maandalizi ya maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika ambayo huadhimishwa kila mwaka Juni 16 tangu mwaka 1991 ilipoteuliwa na Umoja wa Afrika. 

Ambapo, mataifa, jumuiya mbalimbali na jumuiya za kimataifa pamoja na wadau mbalimbali ukusanyika pamoja kwa ajili ya kujadili fursa na changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto katika Bara la Afrika na kutafuta njia sahihi na madhubuti za utatuzi wake, katika kuimarisha haki zao.

Elimu hiyo imeanza kutolewa kuanzia Mei 17, 2022 na itatolewa kwa wiki mbili mfululizo ambapo shule 40 za msingi zitafikiwa na wanafunzi wanaelimishwa juu ya madhara ya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji, ndoa za utotoni na aina mbalimbali za ukatili wa kijinsia.

Ili washiriki kikamilifu kutokomeza vitendo hivyo hasa mwaka huu ambao ni wa ukeketaji kwani unagawanyika kwa mbili hivyo koo nyingi zimejipanga kukeketa zikiwemo Wakenye, Walinchoka, Wairegi Wakira na Nyabasi.
Afisa Mwelimishaji Jamii Kutoka Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT), Emmanuel Goodluck akizungumza Mei 19, 2022 kwa nyakati tofauti na wanafunzi wa Shule ya Msingi Kwitete, Nyangwe, Masangura na Kichongo 'A' na 'B' zilizopo Kata ya Nyamoko Wilaya ya Serengeti walipofika kutoa elimu.

Ambapo amewataka wanafunzi wa shule hizo kutoa taarifa wanapoona viashiria vya ukeketaji katika maeneo yao kwenye vyombo vya dola, ofisi za Vijiji, kata ,Walimu, na Kituo cha Nyumba salama cha Shirika la (HGWT) kwa usaidizi na hifadhi.

Goodluck amesema, kupitia elimu hiyo na vilabu wanavyoanzisha katika shule hizo vitasaidia kuendeleza kasi ya kutokomeza vitendo hivyo na kuwafanya wawe mabalozi wa kushiriki kwa ufanisi kufanikisha juhudi za serikali na wadau mbalimbali wanaopinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Pia, ameishauri jamii kuwathamini na kuwaona watato wa kike wana nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii, hivyo wapewe fursa ya elimu na kuwekewa mazingira wezeshi kutimiza ndoto zao badala ya kukatishwa masomo yao na kufanywa kama kitega uchumi.
Paulina Edward ni Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti akitoa mada kuhusiana na haki za watoto amesema, watoto wana haki ya kulindwa na kila mtu usalama wao, haki ya kupata elimu bora, kupata matibabu, kufundishwa maadili mema.

Pia kupendwa na kushirikishwa katika masuala yanayowahusu na kutoa maoni kushiriki michezo mbalimbali. Hivyo wathaminiwe na kutofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo kutumikishwa katika kazi ngumu, kuteswa na kunyanyaswa.
Paulo Paresso ni Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Serengeti akitoa elimu kwa wanafunzi wa shule hizo amewataka wanafunzi hao na jamii kutambua kuwa, ukeketaji ni kosa kisheria hivyo atakayebainika kufanya vitendo hivyo ndani ya wilaya hiyo atakamatwa na kufikishwa mahakamani.

"Mkiona maandalizi ya ukeketaji toeni taarifa haraka kwa walimu, nyumba Salama (HGWT), Ofisi za serikali, Polisi. Tambueni madhara ya ukeketaji ni mabaya kuna kutokwa damu nyingi wakati wa kukeketwa, hatari ya kifo, madhara ya kisaikolojia kutokana na msongo wa mawazo, kuacha masomo kwa ajili ya kuozeshwa baada ya kukeketwa pia,"amesema.

"Madhara mengine ni kukosa kujiamini, hatari ya kupata magonjwa ya kuambukiza kutokana na kutumia kifaa kimoja wakati wa ukeketaji. Vijana wa kiume nendeni kupata tohara salama hospitalini sio kienyeji, waambieni wazazi ukeketaji kwa mabinti haufai bali washiriki kupinga mila hii mbaya,"amesema Parreso.

Neema Justine na Elizabeth Juma ni Wakazi wa Kata ya Nyamoko Wilaya ya Serengeti wakizungumzia zoezi hilo la utolewaji wa elimu wamelishukuru Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania pamoja na Serikali kwa uamuzi wa kutoa elimu hiyo shuleni katika kudhibiti vitendo vya ukeketaji huku wakiomba wanaofanya ukeketaji kama njia ya kujipatia kipato waache na kutafuta njia mbadala.

"Elimu ya Ukatili wa Kijinsia, iendelee kutolewa kwa makundi yote, wazee wa mila pia waendelee kupewa elimu kwani wananafasi kubwa ya kudhibiti ukeketaji kutokana na kuaminika katika koo zao na jamii. Pia kila mmoja awe tayari kuwafichua wanaofanya ukeketaji naamini wanafahamika kabisa kusudi wafikishwe kwenye vyombo vya sheria na mila zisizofaa ziachwe,"amesema Neema Justine.

Justine Marwa (73) ni mkazi wa Nyamoko amesema kuwa, baadhi ya watu ambao wamekuwa wakiendeleza ukeketaji wanaamini kuwa ukeketaji ni kitendo cha kutimiza taratibu za kimila na kiutamaduni, unaepusha mikosi, unaleta fahari kwenye familia, sehemu ya kusherehekea utamaduni, kumuandaa msichasa kuwa tayari kuolewa na ameonya kwamba, madai hayo hayana ukweli ndani yake hivyo watu waunge mkono juhudi za serikali kukomesha ukeketaji.

Post a Comment

0 Comments