Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) yasisitiza watoto wa kike wasaidiwe mahitaji yao

NA FRESHA KINASA

JAMII imeshauriwa kujenga utaratibu wa kuwasaidia watoto wa kike kupata mahitaji yao ikiwemo kuwatengenezea mazingira wezeshi kusudi waweze kufikia malengo yao.
Ambapo, kila mmoja akishiriki vyema kuwawekea mazingira wezeshi wana uwezo wa kufika mbali zaidi kielimu na kuja kuwa msaada kwa jamii pamoja na kutoa mchango wao katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii hapa nchini.

Kauli hiyo imetolewa Mei 28, 2022 na Emmanuel Goodluck ambaye ni Afisa Mwelimishaji Jamii kutoka Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia lenge makao makuu yake Mugumu wilayani Serengeti mkoani Mara wakati akizungimza na DIRAMAKINI.

Goodluck amesema,watoto wa kike wana nafasi kubwa ya kufanya mambo mengi ambayo yana tija katika jamii ikiwemo uzalishaji mali, kutoa malezi bora pamoja na kuchochea mabadiliko chanya katika jamii.Hivyo jamii ina wajibu wa kuhakikisha inawajali, kuwathamini na kuwapatia mahitani muhimu na kuwatia moyo wakati wote bila kuwakatisha tamaa.
"Kila mmoja kwa nafasi yake ana nafasi ya kuweka misingi madhubuti ya kuhakikisha watoto wa kike wanazidi kung'ara na kupiga hatua, hasa upande wa elimu wawezeshwe mahitaji yote ambayo yanawalenga kama ni taulo za kike wasaidiwe waweze kuhudhuria vipindi vyote vya masomo. Kama ni muda wa kujisomea wapate, na pia kufuatiliwa kwa karibu kuona namna gani wanaenenda jambo hili linahitaji nguvu ya pamoja ya wanajamii wote kusudi kuwa na taifa lenye usawa zaidi katika nyanja mbalimbali,"amesema Goodluck.

Ameongeza kuwa, hivi sasa ni jambo la kushukuru na kupongeza kutokana na Rais Samia Hassan tangu aingie madarakani mchango wa viongozi mbalimbali wanawake wanaohudumu nafasi mbalimbali za uongozi serikalini unazidi kuonekana na tena wakifanya vizuri katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo na hivyo ameomba watoto wa kike waendelee kuwezeshwa kwa nguvu zote na usawa uwepo baina ya watoto wa kiume na wa kike hususani katika elimu na fursa mbalimbali.
"Jamii itambue kwa dhati nia ya Serikali ni kuona kwamba haki na usawa vinatamalaki katika Ustawi wa Jamii. Kwa hiyo mila kandamizi dhidi ya watoto wa kike ziachwe, wapewe fursa ya kusoma na kusaidiwa kwa hali na mali, tunaye Rais wetu ambaye ni dira kuu katika nchi yetu ameuhakikishia umma wa Watanzania na dunia kuwa anaweza kwa kazi nzuri za kuliletea maendeleo taifa ambazo zinafanyika chini ya uongozi wake,"amesema Goodluck.

"Rais Samia aliandaliwa vyema na kikamilifu na ndio maana hivi sasa tunaona matunda mazuri ya uongozi wake katika Taifa letu. Na pia akiwainua wanawake na kuwapa heshima nao pia wanadhihirisha uwezo wao tunawaona wakipiga kazi kwa uhakika lazima jamii tuendelee kuwaandaa zaidi na zaidi kimaadili na kielimu kusudi waje kuonesha uwezo wao katika kuliletea taifa maendeleo,"amesema Goodluck.
Amesema Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania ( HGWT) chini ya Mkurugenzi wake, Rhobi Samwelly limeendelea kushirikiana na Serikali Wilaya ya Serengeti kutoa elimu ya madhara ya ukatili wa kijinsia katika shule mbalimbali wilayani humo.

Sambamba na kuunda klabu za wanafunzi wapinga ukatili wa kijinsia ili kuweka mazingiara mazuri kwa Watoto wa kike kufika mbali zaidi akaomba juhudi za kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia pia zifanywe na kila mmoja ikiwemo kuwafichua wanaofanya vitendo hivyo mbele ya vyombo vya sheria kwa hatua kali.

Amesema, Shirika hilo pia linaendelea kutoa hifadhi kwa wasichana wanaokimbia vitendo vya ukatili wa Kijinsia ikiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni katika Kituo Cha Hope Mugumu Nyumba Salama na Nyumba Salama Butiama ambapo pia linawaendeleza kielimu na wengine katika vyuo vya ufundi kusudi wapate maarifa na ujuzi utakaowasaidia kujikwamua kiuchumi.

Post a Comment

0 Comments