Katibu Mkuu CCM aipa MSD mwezi mmoja kupeleka vifaa tiba Hospitali ya Wilaya ya Ushetu

NA DIRAMAKINI

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo ametoa muda wa mwezi mmoja kwa Bohari ya Dawa (MSD) kufanikisha upelekaji wa vifaa tiba katika Hospitali ya Wilaya ya Ushetu mkoani Shinyanga ili ianze kutoa huduma kwa wananchi.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo akikagua ujenzi wa jengo la utawala katika hospitali hiyo.(PICHA ZOTE NA MICHUZI JR-MMG).

Chongolo ametoa agizo hilo Mei 28,2022 wakati wa ziara yake ya kukagua jengo la hospitali hiyo ya Wilaya ya Ushetu ikiwa ni muendelezo wa ziara zake katika mikoa ya Shinyanga na Simiyu.

Amesema, atazungumza na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kuhusu MSD kuchelewesha uletaji wa vifaa tiba hivyo, lakini pia amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Sophia Mjema kumtafuta mhusika wa bohari ili aweze kukutana nae.
"Niagize ndani ya mwezi huu au mwezi ujayo, hivyo vifaa viwe vimefika hapa ili vianze kutoa tiba na huduma kwa wananchi wetu, haiwezekani Rais wetu mpendwa Samia Suluhu Hassan anashusha fedha nyingi huku kuja kutengeneza miundombinu ya kisasa halafu vifaa tiba inakuwa ni hadhithi, hili halivumiliki.

"Hatupo tayari kuona watu wachache wanakwamisha juhudi zinazofanywa za kuwahudumia wananchi wetu, CCM tuliahidi kupitia ilani yetu mwaka 2020 na tunatekeleza," amesema Chongolo.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Daniel Chongolo akitoa maelekezo kwa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu mkoani Shinyanga, Dkt.Nicodemus Senguo wakati alipokagua ujenzi wa majengo mapya ya hospitali ya wilaya hiyo inayojengwa katika Kijiji cha Mtonga Kata ya Nyamilangano.

Awali Mbunge wa Ushetu, Emmanuel Cherehani alimueleza Katibu Mkuu Chongolo kwamba walipokea shilingi Bilioni 3.2 kwa ajili ya hospitali hiyo, lakini licha ya majengo baadhi kukamilika bado hawajaletewa vifaa tiba na wahudumu kwa ajili ya kuhudumia wananchi wa wilaya hiyo.

"Tunaomba Katibu Mkuu utusaidie kutusemea Hospitali imeshakamilika ila vifaa tiba na wahudumu ndo changamoto, inatulazimu kuwapeleka wagonjwa zaidi ya kilomita 40 hadi Kahama,"amesema.Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Daniel Chongolo akzungumza jambo na msaidizi wake, Bw. Saleh Mhando mara baada ya kufanya ukaguzi wa ujenzi wa jengo la utawala katika hospitali hiyo.

"Majengo tayari, tunachoomba utusaidie vifaa tiba vifike pamoja na wahudumu wa afya ili wananchi hawa wa Ushetu wasiwe wanatembea umbali mrefu kufuata matibabu,"amesema Cherehani.

Ujenzi wa hospitali hiyo umetekelezwa kwa awamu tatu na ulianza Januari 2019 ambapo Serikali imepeleka fedha jumla ya shilingi Bilioni 3.2 kwa ajili ya kukamilisha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news