Jamii iachane na mila, desturi zenye madhara-Dkt.Timo Voipio

NA FRESHA KINASA

MKUU wa Ushirikiano wa Ubalozi wa Finland nchini Tanzania, Dkt.Timo Voipio amesema, jamii inapaswa kuachana na mila na desturi zenye madhara pamoja na vitendo vya ukatili wa kijinsia ambavyo vinakwamisha watoto wa kike kusoma na kufikia ndoto zao.
Amesisitiza wathaminiwe, kwani wakiwezeshwa wana mchango mkubwa katika kuleta maendeleo thabiti katika jamii na taifa kama anavyofanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Hassan Suluhu ambaye ni kiongozi Mkuu wa nchi na mwanamke anayefanya mambo makubwa ya maendeleo.

Ameyasema hayo Mei 25, 2022 alipofanya ziara ya kutembelea Kituo cha ATFGM MASANGA kinachotoa hifadhi kwa wasichana wanaokimbia vitendo vya ukatili kilichopo Wilaya ya Tarime Mkoani Mara ambapo pia amesisitiza usawa wa elimu kwa watoto wa kike na watu wenye ulemavu.

Amehimiza, mila zenye madhara ziachwe na pia kila mmoja awe sehemu ya kuwasaidia watoto wa kike ikiwemo kuwawekea mazingira wezeshi kusudi wafike mbali zaidi katika kuendelea kuchochea mabadiliko chanya Katika Jamii kupitia mchango wao akitolea mfano wa Rais Samia Hassan ambaye ni kielelezo bora kwa hatua kubwa kabisa ya uongozi na anafanya vyema katika kuwatumikia Watanzania. Kwa upande wake Warren Bright, Meneja Mawasiliano wa Shirika la Idadai ya Watu la Umoja wa Mataifa (UNFPA) kwa Tanzania  amesema kuwa, Programu ya Chaguo Langu ni Haki Yangu ni ya miaka mitatu na nusu (2021-2025) na unagharimu dola milioni 6.2 ambayo inatekelezwa na UNFPA kwa kushirikiana na Ubalozi wa Finland nchini Tanzania.

Warren amesema, malengo ya programu hiyo ni kuhakikisha haki za fursa za kuchagua kwa wanawake na wasichana hususani wenye ulemavu zinalindwa na kuimarishwa kupitia mwitikio wa Kisekta mbalimbali na wa kiujumla unaokabili unyanyasaji wa kijinsia (GBV) na mila kandamizi ikiwemo ndoa za kulazimishwa katika umri mdogo pamoja na ukeketaji wa wanawake na wasichana.

Ameongeza kuwa, utekelezwaji wa Programu hii, ni sehemu ya utekelezaji wa shughuli za Mpango wa kitaifa wa kutokomeza Ukatili wa Kijinsia dhidi ya wanawake na Watoto (NPA -VAWC) Tanzania bara (2016- 2017-2021/22)na Zanzibar (2017-2022).

"Wanufaika wa Mradi huo ni wasichana walio katika rika barehe na wasichana vijana hususani wanawake na wasichana wenye ulemavu, walio katika rika balehe wanaoishi Mikoa ya Shinyanga Wilaya ya Kishapu na Kahama, Mkoa wa Mara Wilaya ya Tarime na Butiama pamoja na Zanzibar Wilaya za Mjini Unguja na Chake chake pemba) ambao wako hatarini au ni waathirika wa ukatili wa Kijinsia (GBV) ukeketaji (FGM) na ndoa za utotoni,"amesema Warren.

Aidha amesema, wanufaika wasio wa moja kwa moja ni pamoja na familia zilizoathirika, Junuiya zinazolengwa na Taasisi za Kiserikali ambazo uwezo wao utaanishwa ili Kuzuia na kukabiliana na (GBV) na ukeketaji (FGM) na ndoa za utotoni na kudumisha haki za Wanawake na wasichana hasa walio na ulemavu.

Mradi huo una malengo makuu matano ikiwemo kuandaa na kutekeleza sheria, sera na Mipango ya kifaifa inayozuia ukatili wa Kijinsia (GBV) na mila potofu, kuwalinda Wanawake na wasichana hasa wenye ulemavu na waliokatika hatari na kushughilikia mahitaji ya wale walioathirika na ukatili wa Kijinsia.

Lengo la pili ni kuongeza kwa upatikanaji wa huduma za kisekta mbalimbali za Kuzuia ukatili wa Kijinsia unaojunuisha ulemavu, ukeketaji na huduma za Kuzuia na kupunguza ndoa za utotoni kwa wanawake na wasichana wenye ulemavu.

Lengo la tatu ni kuwashirikisha wasichana na vijana wa kike hasa Wanawake na wasichana wenye ulemavu ili kuweza kuleta mabadiliko ya Kijinsia na shughuli zinazowajengea ufahamu kwa kanuni na maadili ya Kijinsia na kuwajengea uwezo wa maarifa na ujuzi wa kudai haki zao na kukataa ukatili wa Kijinsia ukeketaji na ndoa za utotoni na kupata huduma za kisekta za kiafya, kijamii na huduma za ulinzi.
Lengo la nne ni kuongeza nafasi inayotekelezwa na jamii vikiwemo vikundi vya Kijamii, Viongozi wenye ushawishi na wanaume na wavulana. Kuongeza uhamasishaji wa Jamii Kuzuia na kukabiliana na ukatili wa Kijinsia, ndoa za utotoni na ukeketaji dhidi ya Wanawake na wasichana hususani wenye ulemavu.

Lengo la tano ni kuongeza upatikanaji wa takwimu, ushahidi, nyaraka na mafunzo kuhusu ukatili wa Kijinsia (GBV) ukeketaji (FGM) pamoja na hatari ya kuhusiana na kuongezeka kwa watu wenye ulemavu.

Valeriane Mgani ni Meneja Miradi Kutoka Shirika la ATFGM MASANGA amesema, wamekuwa wakitoa elimu juu ya madhara ya ukeketaji, ndoa za utotoni, vipigo, na aina mbalimbali za ukatili huku akisema kwa wiki wanapokea malalamiko ya ukatili kati ya 10 hadi 30 na kwa kipindi hiki na wameshinda kesi mahakamani zaidi ya 30 tangu mwaka 2006 shirika hilo lilipoanza.

Ameongeza kuwa, kupitia mradi huo watatekeleza Wilaya ya Tarime na Butiama na fedha zimetolewa na ubalozi wa Finland ambapo mradi unakuja kuimarisha miundombinu ambayo serikali imekwisha weka tayari watatoa elimu kwa watu wenye ulemavu wajue haki zao na sehemu ya kuripoti matukio na kutengeneza mtandao wao. Huku akisema kabla ya kuanza mradi watafanya utafiti kuwabaini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news